• Siku ya Mwanamke Duniani, Nara Tupu au Hakika?

Tarehe 8 Machi kila mwaka iliainishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Mwanamke Duniani.

Siku hii kwa hakika inakumbusha historia ya mapambano ya muda mrefu ya kisiasa na kijamii ya wanawake na watetezi wa haki zao dhidi ya ubaguzi na kutaka kuwepo mazingira mazuri na bora zaidi ya sehemu hiyo ya jamii ya mwanadamu. Hata hivyo tunapochunguza hali ya mwanamke wa sasa tunakumbana na uhakika mwingine.  

Pamoja na kwamba kwa makumi ya miaka sasa jumuiya na mashirika mbalimbali kote duniani yamekuwa yakifanya jitihada kubwa za kutetea na kulinda haki na utukufu wa kibinadamu wa wanawake, lakini bado kunashuhudiwa dhulma na ubaguzi mkubwa dhidi ya wanawake katika aghlabu ya nchi za dunia. Kwa mfano tu, tunaweza kuashiria hali ya kiwango cha elimu baina ya wanawake katika nchi mbalimbali za dunia. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, kiwango cha wanawake wasiojua kusoma wala kuandika kiko juu sana baina ya wanawake katika nchi mbalimbali za dunia na kwamba kuna ubaguzi mkubwa dhidi ya wanawake katika uwanja huo. Kwa mfano katika nchi ya Mali idadi ya wanawake wanaojua kusoma ni asilimia 25 tu na kiwango hicho ni asilimia 43 kati ya wanaume. Hali kama hiyo inashuhudiwa pia katika nchi ya Chad ambako wanawake wanaojua kusoma na kuandika ni asilimia 28 tu na wanaume ni 47. Katika nchi hiyo hiyo ya Chad asilimia 55 tu ya wasichana wanaomaliza shule za msingi ndio wanaosajiliwa kuendelea na masomo ya sekondari na kwa msingi huo Chad inatambuliwa kuwa nchi mbaya zaidi duniani katika uwanja huo. Baada ya Chad zinafuatia nchi za Ivory Coast, Pakistan na Yemen ambako kunashuhudiwa ufa na tofauti kubwa baina ya wasichana na wavulana wanaofanikiwa kuendelea na shule za sekondari baada ya kumaliza shule za msingi. Jambo la kushangaza zaidi ni kuwa, hata katika nchi zilizoendelea ambako inasemekana idadi ya wanawake waliopata elimu ya chuo kikuu ni kubwa zaidi kuliko ile ya wanaume, wanawake bado wanakabiliwa na ubaguzi mkubwa katika sekta ya ajira na kazi ikilinganishwa na wenzao wanaume.  

Takwimu za Jukwaa la Uchumi Duniani zinaonesha kuwa, wanawake katika nchi nyingi duniani wananyimwa kazi katika idara mbalimbali licha ya kuwa na vyeti vya masomo na elimu sawa na wenzao wanaume. Katika nchi hizo asilimia 80 ya nafasi za wafanyakazi wa idara na taasisi mbalimbali zinashikwa na wanaume. Vilevile kunashuhudiwa tofauti kubwa sana baina ya wanawake na wanaume katika kiwango cha fusra za kiuchumi na kibiashara katika nchi ambazo hali ya usawa wa kijinsia si nzuri wala ya kuridhisha. Katika nchi hizo nguvu kazi unayojishughulisha na masuala ya uchumi na uzalishaji ya wanaume kwa uchache ni mara tatu zaidi ya wanawake. Zaidi ni kuwa katika nchi hizo aghlabu ya wanawake wanaofanya kazi hupata mishahara ya chini zaidi ikilinganishwa na ya wenzao wanaume.

Hali hii inazihusu nchi zote zikiwemo zile zilizostawi. Katika kitabu chake alichokipa jina la Vita dhidi ya Wanawake, mwandishi Marilyn French ametoa habari za kutiliwa maanani sana kuhusu hali ya kikazi na wanawake katika nchi za Magharibi. Anaandika kuwa: Nchini Marekani licha ya kwamba asilimia 55 ya wanawake wanapata mshahara kutokana na kufanyakazi lakini wote hao bado wanakabiliwa na ubaguzi.  

Ruth Pearson ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza anasema: Japokuwa wafanyakazi wa kike wanajihisi kuwa na uhuru wa mtu binafsi unaotokana na kuwa na pato na kwamba wanajitegemea kiuchumi lakini katika upande mwingine wote wanaelewa kuwa, mshahara wanaopewa ni mdogo sana ukilinganishwa na ule wanaopewa wanaume. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, bado kuna ufa na tofauti kubwa baina ya wanawake na wanaume katika soko la kazi na ajira. Takwimu za mwaka 2015 zinaonesha kuwa, asilimia 50 ya wanawake waliofikia umri wa kufanya kazi (miaka 15 na kuendelea) kote dunia wanafanya kazi, wakati upande wa wanaume kiwango hicho ni asilimia 77.

Ukosefu wa usawa katika mishahara baina ya wanawake na wanaume

Ubaguzi na ukosefu wa usawa wa kijinsia pia unashuhudiwa katika suala la uongozi. Matokeo ya uchunguzi wa kimataifa uliofanyika mwaka 2013 yanaonesha kuwa, asilimia 24 tu ya wanawake ndio wanaofanyakazi kama mudiri na na wakurugenzi duniani. Idadi hiyo katika nchi za kundi la G8 zilizostawi na tajri zaidi duniani ni silimia 16 tu! Katika nchi kama Brazil, Russia na India kiwango cha wanawake wenye nafasi za juu za uongozi ni asilimia  26. Huko Japan watu 93 kati ya kila 100 wanaofanyakazi kama wakurugenzi na viongozi wa vyeo na nafasi za juu ni wananaume na huko Marekani idadi hiyo inafikia watu 80. Nchini China pekee ndiko idadi ya wanawake wenye vyeo na nafasi za juu za uongozi inazidi ile ya wanaume. Nukta ya kustaajabisha ni kuwa, nchi kama Sweden na Norway ambazo zilipasisha sheria ya usawa wa kijinsia miaka mingi iliyopita zinashika nafasi ya 22 na 27 duniani katika uwanja huo.  

Wanawake wanakabiliwa na ukatili wa kingono katika maeneo ya kazi

Wanawake wanaofanya kazi si tu kwamba wanakabiliwa na ubaguzi wa kijinsia katika mishahara ya kazi sawa na zile zinazofanywa na wanaume na katika kupandishwa vyeo na daraja makazini, vilevile wanasumbuliwa na ukatili wa kimwili na kinafsi katika maeneo ya kazi. Taarifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) imetangaza kuwa, ukatili wa kingono ni miongoni mwa manyanyaso na ubaguzi wa kijinsia unaofanywa dhidi ya wanawake katika maeneo ya kazi. Ripoti za shirika hilo zinasema kuwa, asilimia 40 hadi 50 ya wanawake katika nchi za Umoja wa Ulaya wana historia ya kukumbwa na ukatili na manyanyaso ya kijinsia au mahusiano ya kingono bila ya ridhaa zao katika maeneo ya kazi. Vilevile kumeripotiwa visa na ukatili wa aina mbalimbali wa kijinsia kama manyanyaso ya maneno, ngono na kadhalika kati ya asilimia 30 hadi 40 kati ya wanawake wa Asia na Pasific.

Uchunguzi uliofanyika katika nchi 11 za Ulaya umeonesha kuwa, asilimia 30 hadi 50 ya wanawake wamekumbana na maudhi na manyanyaso ya aina mbalimbali katika mazingira na maeneo ya kazi. Kiwango hicho ni asilimia 10 upande wa wanaume. Manyanyaso ya wanawake katika maeneo ya kazi nchini Uingereza ni asilimia 54 na Marekani asilimia 44 kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Ukatili na manyanyaso dhidi ya wanawake hauishii katika mazingira ya kazi pekee bali hii leo manyanyaso na maudhi wanayokabiliana nayo wanawake majumbani ni miongoni mwa mambo yanayohatarisha usalama na amani ya wanawake katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan katika nchi za Magharibi zinazodai kuwa mstari wa mbele kutetea haki za binadamu. Kwa mfano tu Ripoti iliyotolewa hivi karibuni barani Ulaya chini ya anwani ya Ukatili Sugu dhidi ya Wanawake wa Ulaya" imeashiria takwimu za kushtua kuhusu manyanyaso na ukatili mkubwa unaofanyika dhidi ya wanawakwe katika nchi wanachama kwenye Umoja wa Ulaya. Uchunguzi huo uliofanyika kwa kuwahoji wanawake 42,000 katika nchi 28 wanachama katika umoja huo umebaini kuwa, asilia 55 ya wanawake katika nchi hizo wanakumbwa na ukatili wa kijinsia, kimwili na kinafsi.

Ukatili dhidi ya wanawake unapaswa kukomeshwa

Nukta ya kutiliwa maanani ni kuwa ukatili dhidi ya wanawake katika nchi za ulimwengu wa tatu unashabihiana na ule unaofanyika katika nchi zilizoendelea. Matokeo ya uchunguzi 500 uliofanyika kuhusu ukatili unaofanywa dhidi ya wanawake katika pembe mbalimbali za dunia umeonesha kuwa, manyanyaso na ukatili dhidi ya wanawake nchini Marekani unafanana na ule unaofanyika dhidi ya wanawake katika nchi kama Zimbabwe na Cambodia.

Sambamba na matatizo hayo yote pia tunaweza kuashiria ongezeko kubwa la kiwango cha talaka, kudhoofika kwa taasisi ya familia, kuongezeka idadi ya familia zenye mzazi mmoja, kuavya na kutolea mimba baina ya wasichana na umaskini mkubwa wa tabaka la wanawake. Hivyo basi wka sasa dunia inasherehekea Siku ya Mwanamke Duniani huku idadi kubwa ya wanawake ikiendelea kutaabika na kusumbuliwa na matatizo mengi yanayopaswa kushughulikiwa ili kuboresha maisha si ya tabaka la wanawake pekee bali wanadamu wote kwa ujumla.    

Mar 12, 2017 11:17 UTC
Maoni