• Imam Baqir AS dhihirisho la mwanadamu aliye kamili

Bismillahir Rahmanir Rahim. Karibuni wasikilizaji wapenzi katika kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam Baqir AS, mmoja wa Maimamu watukufu kutoka katika kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume Muhammad SAW. Tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba huo. Karibuni.

Katika siku ya kwanza ya mwezi uliojaa baraka wa Rajab mwaka wa 57 Hijria, mji uliojaa utulivu na ukimya wa Madina ulishitukizwa na mwanga wa nuru kubwa katika nyumba ya udongo ya Imam Sajjad, Aliyyu bnil Husain, Zaynul Abidin AS. Chemchemu ya elimu inayotiririka na kupasua njia ya taalimu katika kubainisha elimu na maarifa ilitiririka na kushibisha kiu za nyoyo za watafuta elimu na maarifa kwa maji yake yaliyojaa baraka. Mwana aliyejaa baraka ambaye mara nyingi Bwana Mtume Muhammad SAW alibashiri kuzaliwa kwake, alizaliwa. Huyo ni yule mwana ambaye alilandana sana na Mtume wa Allah kwa sura yake iliyojaa baraka na rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Bishara ya Bwana Mtume ilitimia kwa kuzaliwa Imam Muhammad Baqir AS.

Jina tukufu la Imam Baqir ni sawa na la Bwana Mtume, ni Muhammad, na lakabu yake maarufu zaidi ilikuwa ni Baqirul Ulum, mtu aliyebobea katika elimu. Imam Baqir alikuwa na sifa mbili kuu zilizompambanua na Maimamu wengine AS. Moja ni kuwa babu yake mzaa baba alikuwa ni Imam Husain AS na babu yake mzaa mama alikuwa ni Imam Hasan AS, mabwana wa vijana wa peponi. Sifa nyingine ya kipekee aliyokuwa nayo Imam Baqir AS ni kuweka kwake msingi wa mapinduzi ya kiutamaduni kwa ajili ya wafuasi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW.

Ijapokuwa mwanawe Imam Jafar Sadiq AS ndiye anayetajwa sana katika uenezaji wa mafundisho ya Kishia na ya Ahlul Bayt AS lakini msingi wa mapinduzi hayo uliwekwa na Imam Baqir AS. Nafasi muhimu ya kidini na kielimu ya Imam Baqir AS ni miongoni mwa mambo yanayokita sana katika mijadala inayomuhusu mtukufu huyo. Kila mmoja kati ya Maimamu wa Ahul Bayt AS alikuwa na sifa yake maalumu kulingana na zama na mahitaji ya kiutamaduni na kisiasa ya zama alizoishi.

Katika zama za Imam Baqir AS mazingira ya kisiasa na kijamii yalikuwa kwa namna ambayo yalimpa fursa Imam ya kubainisha mafundisho ya kidini na kiitikadi na kulinda hadithi sahihi za Bwana Mtume Muhammad SAW. Imam alikuwa na sifa hizo sambamba na ucha Mungu wa hali ya juu, ikhlasi na sifa nyingine bora za kimaadili zilizomfanya kuwa shakhsia wa kipekee ya mwanadamu aliyekamilika katika sifa zote za kibinadamu.

Imam Baqir AS aliwalingania watu kufuata mafundisho ya Qur’ani Tukufu na aliiandalia jamii ya Waislamu nafasi kubwa ya elimu na maarifa na elimu nyinginezo zilizohitajika katika maisha yao. Mtukufu huyo amenukuliwa akisema: Mwanachuoni ambaye anainufaisha jamii kwa elimu yake, ni bora kuliko watu elfu sabini wanaojibidiisha kufanya ibada za mchana na usiku.

Kwa kweli hakuna dini yoyote isipokuwa Uislamu inayowahimiza watu kiasi chote hiki kuhusu wajibu wa kutafuta elimu. Tab’an inabidi tutilie maanani pia hapa kwamba, sisitizo hilo limetoka kwa mtu ambaye alikuwa katika kilele cha ucha Mungu na kunyenyekea kwa Mola wake Mlezi na hayakutoka kwa mtu ambaye alikuwa hajui chochote kuhusu dini au mtu ambaye anathamini zaidi elimu na ana uadui na matukufu ya kidini.

Kwa maneno yake hayo Imam Baqir alitaka kuusisitizia umma wa Kiislamu kwamba ujiepusha na ibada zisizo na taqwa, au amali bila ya elimu na ibada za juu juu zisizo na utambuzi, bali wasome na wajibidiishe kutafuta elimu ili wanapofanya ibada wawe wanafanya ibada hizo kwa elimu kamili na kujua vyema wanachokifanya.

Katika miongozo yake mingine, Imam Baqir AS amenukuliwa akisema: Elimu ni silaha ya kukabiliana na maadui. Katika sehemu nyingine amenukuliwa akisema: Maimamu na viongozi wateule wa Mwenyezi Mungu walikuwa na sifa hiyo yenye thamani kubwa ndio maana waliweza kuwa juu ya wengine na wengine nao wakalazimika kuwafuata.

 

Maisha ya Imam Baqir AS yalikuwa ni kioo kinachoonesha vipengee vyote vya maisha ya mwanadamu aliyekamilika katika uanadamu wake. Moja ya sifa za kipekee alizokuwa nazo Imam AS ni kuingiliana kwake sana na watu. Kuzingatia kwake sana elimu hakukumuweka mbali hata kidogo na masuala ya kimaadili na tabia njema. Kuzingatia kwake sana masuala ya kimaanawi, kumcha Mwenyezi Mungu na kunyenyekea Kwake, hakukumzuia kuendelea na maisha yake ya kawaida na kuwa na uhusiano mzuri na jamii na kufanya jitihada za kuleta marekebisho katika umma wa Kiislamu.

Tunapoyatupia jicho maisha ya Imam Baqir AS tutaona kwamba alikuwa ruwaza na kigezo cha kufuatwa katika chanjaa na vipengee vyote vya maisha.  Katika upande wa kielimu, Imam Baqir AS alikuwa katika daraja za juu kabisa za kielimu kiasi kwamba maulamaa wote wa zama zake, wawe maulamaa wa Kisunni au maulamaa wa Imammiyyah wote walikubaliana kwamba Imam Baqir AS alikuwa ndiye mbora wa elimu katika zama zake.

Katika upande wa uchaji Mungu na kufanya ibada pia, alikuwa mchaji Mungu mkubwa zaidi kuliko watu wengine katika zama zake. Mwanachuoni mkubwa na mcha Mungu sana wa Kisunni, Attar Nishaburi  katika kitabu chake cha “Tadhkiratul Awliyaa” amemtaja Imam Baqir AS kwa jina la “Imam Awladin Nabi” yaani Imam wa Wana wa Mtume na pia anamtaja kwa jina la “Chaguo la Wana wa Ali.”

Katika mlango wa namna Imam Baqir AS alivyokuwa anasali, imeandikwa, wakati mtukufu huyo alipokuwa anasimama kusali, baadhi ya wakati rangi ya uso wake uliojaa baraka ilikuwa ikibadilika na kupiga wekundu, na baadhi ya wakati ulikuwa unabadilika na kuwa wa njano na alikuwa akimuabudu Mola wake kwa hofu na unyenyekevu mkubwa kana kwamba alikuwa anamuona kwa jicho lake.

Baadhi ya watu waliomuona Imam Baqir AS katika safari yake ya Hija wamenukuu yafuatayo: Imam alioga na kuingia miguu chini sehemu ya Ihram na alipofika katika Masjidul Haram, aliiangalia al Qaaba na kuanza kulia kwa sauti kubwa. Baadaye alitufu na baada ya kusali alisujudu muda mrefu na aliponyanyua kichwa chake kutoka kwenye sijda, eneo alilosujudu lililonekana limejaa machozi.

Amma jambo la kuvutia hapa ni kwamba, licha ya kuwa Imam Baqir AS alikuwa katika kilele cha juu cha ucha Mungu na taqwa, na alikuwa katika daraja za juu kabisa za waja wema wa Mwenyezi Mungu, lakini alikuwa pia mtu aliyejibidiisha mno kufanya kazi na alijiepusha kikamilifu kuwategemea watu wengine katika kudhamini mahitaji ya maisha yake. Katika upande wa pili pia, kila alipofikiwa na mtu kuombwa msaada, alikuwa akitoa msaada huo kwa moyo msafi na uso ulijaa bashasha.

Ukarimu wa Imam Baqir AS ulikuwa mkubwa kiasi kwamba kumenukuliwa maneno yafuatayo kutoka kwa wapokezi wa hadithi kwamba kamwe haikuwahi kusikika ikisemwa kwamba mtu amekwenda na haja kwa mtukufu huyo akarudi mikono mitupu.

Katika upande mwingine na licha ya kwamba Imam Baqir AS alikuwa akifanya bidii kubwa ya kutafuta maisha, lakini kamwe hakuyafanya maisha yake yawe yote ni ya kutafuta maisha tu. Bali hima yake kubwa ilikuwa ni kuitengeneza jamii na kuitumikia. Imam Baqir AS alitoa taathira kubwa sana ya kielimu na kivitendo kwa jamii ya zama zake.

Kushiriki katika mikusanyiko ya kielimu na kuitisha mikutaniko ya kiutamaduni ndiyo mbinu kubwa iliyotumiwa na mtukufu huyo katika kuutumikia umma wa Kiislamu. Alikuwa anahimiza sana kwamba ukamilifu wa kifikra na kiutamaduni ndio unaoleta ukamilifu wa kijamii katika masuala ya kimaadili, kimaanawi na kiuchumi. Katika kubainisha nafasi muhimu mno ya Imam Baqir AS katika jamii ya Kiislamu, inatosha kutaja nukta hii kuhusu Imam Baqir AS na baada yake Imam Sadiq AS muasisi wa Chuo Kikuu cha Ahlul Bayt AS ambacho kiliorodhesha karibu risala 6000 za kielimu kutoka kwa wanafunzi waliohitimu masomo yao kwenye chuo hicho.

Kutokana na welewa mkubwa mno aliokuwa nao kuhusu mafundisho ya Qur’ani Tukufu na sunna za Bwana Mtume Muhammad SAW, Imam Baqir alielimisha idadi kubwa ya watu elimu za kila namna na kuwaondoa kwenye kiza cha ujinga kwa kuwaongoza kwenye nuru ya elimu tukufu zenye manufaa.

 

Abu Hamza ath Thumali, mmoja wa wafuasi wa karibu sana wa Imam Baqir AS anasema: “Nilikuwa nimekaa ndani ya Msikiti wa Mtume, mara akanijia mtu na baada ya kunitolea salamu aliniuliza akisema: Je unamtambua Abu Jaafar, Muhammad bin Ali? Nikajibu ndio, je una kazi na haja gani na mtukufu huyo? Akasema: Nimekusanya maswali yangu 40 nataka nimuulize, hapo hapo Imam Baqir AS akaingia msikitini huku kundi la watu wa Khurasan na watu wengine wakiwa wamemzingira wakitaka kumuuliza maswali kuhusu Hija. Yule mtu naye akaenda karibu na Imam, akakaa karibu naye na kumueleza haja yake, na hapo hapo Imam akamjibu maswali yake yote arubaini bila ya kumuakhirisha hata kidogo.

Mapenzi kwa watoto na watu wa familia, yaliyojaa uchungaji wa matukufu ya kidni na ya Mwenyezi Mungu yanapatikana kwa njia sahihi mno katika chuo cha Ahlul Bayt AS. Imam alikuwa akizingatia hata haki ndogo kabisa ambazo kwa watu wa kawaida zinaonekana ni kitu kidogo katika kuamiliana na wake zao na watoto wao.

Hasan al Basri anahadithia kisa kimoja alichokishuhudia yeye na rafiki yake wakati walipokwenda kwa Imam Baqir AS kuuliza maswali na kuongeza elimu. Muhtasari wa kisa hicho ni kuwa, Hasan al Basri anasema siku moja walikwenda nyumbani kwa Imam Baqir AS wakamkuta katika chumba kilichokuwa na mapambo mbalimbali ya zama hizo na vitu vingine vilivyoonesha hali tofauti na walivyozoea kumuona nayo Imam. Hawakusema kitu, bali waliuliza maswali yao na kuomba ruhusa ya kuondoka. Kabla ya kuondoka Imam aliwataka waje tena siku ya pili.  

Siku ya pili ilipofika, wakaenda tena kwa Imam, mara hii lakini walimkuta katika mazingira waliyozoea kumuona kila siku, chumba alichokuwa amekaa hakikuwa na kitu chochote na nguo alizovaa zilikuwa zimechakaa kabisa. Imam akamwambia rafiki wa Hasan al Basri kwamba, ndugu yangu kutoka Basra! Nataraji uliyoyaona jana hayajakutia kinyongo na kudhania mambo isivyo. Chumba mlichokiona jana ni cha mke wangu ambaye nilimuoa jana na vile vitu vyote mlivyoviona vilikuwa ni vitu vyake alivyokuja navyo. Hasan al Basri anaendelea kuhadithia akisema: Yule rafiki yangu akasema: Naapa kwa Mwenyezi Mungu, jana niliingia kinyongo, lakini kwa hali niliyoiona leo, kinyongo changu kimeyeyuka kabisa.

Tunachojifunza katika kisa hiki ni kuwa Imam licha ya kwamba alikuwa anajiepusha kabisa na masuala ya anasa, lakini alikuwa anazingatia pia haki za wake zake na za wanawe. Maimamu hawakuwa wakijiharamishia mambo mazuri waliyohalalishiwa na Mola wao na wala hawakuwa wakijiweka mbali na jamii.

Kwa mara nyingine tunatoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Baqir AS na tunamuomba Allah atuongoze katika njia iliyojaa nuru ya Bwana Mtume Muhammad SAW na Ahlul Bayt wake AS.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.      

 

Mar 29, 2017 15:11 UTC
Maoni