• Kwa mnasaba wa kufa shahidi Imam Hadi (AS), nuru ya uongofu na utaalamishaji

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Wapenzi wasikilizaji, tumo kwenye masiku ya mwezi mtukufu wa Rajab ambapo tarehe 3 ya mwezi huu mwaka 254 hijria ni siku aliyokufa shahidi mwana mwengine mtoharifu wa Bwana Mtume Muhammad (SAW).

Katika siku kama hii wakati jua lilipochomoza na miale yake kuangaza ardhini, ilitangazwa habari iliyowahuzunisha na kuwatia majonzi wengi ya kufa shahidi Imam Ali An-Naqi (as).  Imam mtukufu ambaye ni maarufu kwa lakabu ya "Hadi" yaani muongozaji kuelekea uongofu. Katika siku hii ya kukumbuka kufa shahidi kwa Imam huyo raufu, tunachukua fursa hii kutoa mkono wa pole kwenu nyinyi wasikilizaji wapenzi na kuzungumzia machache kuhusu maisha yake yaliyojaa kheri na baraka. Lakini kabla ya jambo lolote tunafikisha kwanza maamkizi yetu kwa heshima na taadhima kwa Imam Hadi (as) kwa kusema: "Amani na rehma za Allah ziwe juu yako ewe Abal Hassan, ewe muongozaji kuelekea uongofu na nuru ya Allah ing'aayo. Tunashuhudia kwamba wewe ni hoja ya Allah kwa viumbe wa ulimwengu. Wewe ni ile nguzo na mlinzi wa dini na kimbilio na marejeo ya waja."

Imam Hadi (as) alizaliwa mwezi 15 Dhulhijjah mwaka 212 hijria katika viunga vya mji wa Madina. Baada ya kufa shahidi baba yake, yaani Imam Jawad (as), Imam Hadi alibeba jukumu la kuuongoza umma wa Waislamu kwa muda wa miaka 33. Katika zama zake, zilishamiri madhehebu na matapo tofauti ya kiitikadi, na shubha na utata wa kidini ulitanda katika Ulimwengu wa Kiislamu. Shubha na utata ambao ulikuwa ukipenyezwa na kuenezwa ndani ya jamii ya Kiislamu na kikundi cha watu walioghilibiwa, wenye tamaa na kujali maslahi tu. Tab'an makhalifa wa Bani Abbasi nao pia walikitumia kikundi hicho na harakati yao kama silaha ya kudhoofisha misingi ya kifikra na kiitikadi ya Waislamu kwa manufaa yao. Kwa hivyo kuenea anuai za shubha za kifikra na kiitikadi ni mojawapo ya mambo muhimu yaliyokuwepo katika zama za Imam Hadi (as). Imam Hadi pia, kama walivyokuwa Maimamu wengine watoharifu ambao kwa kuzingatia matukio na mabadiliko ya kijamii, kisiasa na kiitikadi walichukua hatua makini mno kwa ajili ya kuwaongoza Waislamu na kuulinda Uislamu halisi na wa asili, yeye pia alifanya vivyo hivyo na akaipanga misingi ya kielimu ya mafundisho ya Ahlulbayt kwa namna ambayo yaliweza kukidhi mahitaji ya kifikra na kisiasa, si ya watu wa zama zake tu bali pia wa zama za baada yake.

Katika zama za Imam Hadi (as), Muutazilah na Ash'ari zilikuwa miongoni mwa fikra za kiitikadi ambazo kutokana na mitazamo yao mikuu kuhusu masuala kama Jabr na Ikhtiyar, kuwezekana au kutowezekana kuonekana Mwenyezi Mungu na kuwa na umbo Yeye Mola, zilikanganya na kuchemsha akili na fikra za watu katika jamii. Kwa sababu hiyo, ili kutoa mwongozo na kuonesha watu uongofu, Imam Hadi (as) alifanya midahalo na kutoa maandiko ya hoja wadhiha na za wazi za kuibainishia jamii ya Kiislamu mafundisho asili ya Uislamu yasiyo hata na chembe ya doa la upotofu. Kwa kutoa mfano tunaweza kutaja hapa waraka mrefu wa Imam ambao ndani yake alitoa ufafanuzi wa hoja kuhusu Qur'ani na Ahlulbayt, kuvitambulisha vizito hivyo viwili na ulazima wa kushikamana navyo na kubainisha kwa hoja makini na wadhiha za ukosoaji wa kielimu kuhusu maudhui ya jabr na ikhtiyar, ambayo ni mojawapo ya maudhui tata zaidi za masuala ya itikadi yaani Ilimul-kalam. Fitna kuhusu Qur'ani kama imeumbwa au la, ni moja ya harakati nyengine muhimu ya kifikra iliyokuwepo katika zama za Imam Hadi (as), ambayo ilishughulisha akili za Waislamu kwa muda mrefu hata kufikia hadi ya watu wengi kuteswa na kuwekwa gerezani au hata kuuawa kwa sababu ya kuwa na msimamo huu au ule kuhusiana na suala hilo.

Imam Hadi (as) aliyekuwa na jukumu la kuongoza fikra za Kiislamu, kwanza alikuelezea kuibuka kwa hitilafu hizo na kuzipalilia kuwa ni kuwanufaisha maadui wa Uislamu na kubainisha kwamba kujadiliana juu ya suala hilo ni kuzusha bid'a katika dini; hivyo akawatahadharisha wafuasi wake na kujishughulisha na mijadala ya aina hiyo kwa kuwaambia: "Kujadiliana na kubishana kuhusu Qur'ani ( kama ni mahuluku au si mahuluku, ni ya tangu azali au la) ni bid'a ambayo inamhusisha muulizaji na mtoaji jawabu, kwa sababu muulizaji atapata kitu asicho laiki na mtoaji jawabu atajitia tabu na mashaka bila ya sababu kwa jambo asiloliweza. Hakuna muumbaji isipokuwa Mwenyezi Mungu; Yeye ameumba kila kitu, na Qur'ani ni maneno ya Mwenyezi Mungu, hivyo usijiwekee jina kuhusiana nayo na kukufanya uwe miongoni mwa waliopotoka".

Shubha nyengine muhimu ya kifikra na kiitikadi ambayo ilikuwa imeenea katika zama za Imam Hadi (as) na kukoroga itikadi za watu ilikuwa ni ya kumuitakidi Mwenyezi Mungu kuwa na mwili. Kwa msimamo thabiti wa hoja na burhani, Imam aliivunja imani hiyo kwa kusema: "Wafuasi wa Ahlulbayt hawaamini juu ya Mwenyezi Mungu kuwa na umbo kwa sababu sharti la kumshabihisha Mwenyezi Mungu na vitu vingine ni kumtawasari kuwa na mwili; na kitu ambacho ni mwili, chenyewe huwa kimetokana na kitu kingine, yaani maalul; na utukufu wa Mwenyezi Mungu uko mbali na umithilishaji huu; kwa sababu kuwa na mwili kunaambatana na kufungika na mipaka ya mahala na zama na athari nyenginezo kama kuzeeka, kuchakaa n.k. Ilhali dhati ya Mwenyezi Mungu imetakasika na ulinganishaji huu". Kwa hakika itikadi hiyo ni sawa na ile iliyosababisha kuzuka imani ya Utatu katika Ukristo na kuwafanya Manasara wamuitakidi Mwenyezi Mungu kuwa na mshirika.

Zama za Uimamu wa Imam Hadi (as) zilichanganyika muda wote na mbinyo mkubwa na mashinikizo mengi ya watawala wa Bani Abbasi na hata mawasiliano ya Imam na watu yalikabiliwa na tabu na misukosuko mingi. Kwa sababu hiyo mtukufu huyo aliandaa mipango na tadbiri kadhaa, mojawapo ikiwa ni kuanzisha mtandao wa mawakili na wawakilishi wake ambao ulikuwa maarufu kwa jina la taasisi ya uwakili. Taasisi hiyo ya siri ilianzishwa tangu zama za Imam Jaafar Sadiq (as) na ikaanza harakati zake kwa kificho. Lakini katika zama za Imam Hadi (as) ikawa ni chombo rasmi na cha kisasa zaidi chenye sifa na madhihirisho maalumu. Kwa upande wa kielimu na kifiqhi, taasisi hiyo muhimu iliweza kukidhi mahitaji ya waumini ambao hawakuweza kuifikia chemchemi kuu ya maarifa; ambapo kuondoa shubha za kiitikadi na kifikra yalikuwa miongoni mwa masuala ya msingi iliyoyashughulikia. Katika zama hizo, Imam Hadi (as) aliweza kuwa na mawasiliano ya kudumu na wafuasi wake katika nchi za Iran, Iraq, Yemen na Misri kupitia mawakili na wajumbe wake na kwa njia ya uandishi wa risala na barua mbalimbali. Katika kudhamini ufanisi wa mawakili wake hao, mtukufu huyo alikuwa kila baada ya muda akifanya uteuzi mbalimbali na kuwapa maelekezo mawakili hao kupitia miongozo aliyokuwa akitoa. Mawakili na wawakilishi wa Imam Hadi (as) walikuwa na nafasi muhimu sana katika masuala ya kiitikadi na kifiqhi. Kuna wakati mawakili hao walikuwa wakigunduliwa na maajenti wa utawala na hivyo kukamatwa na kutiwa gerezani ambako waliadhibiwa na kuteswa na hata baadhi yao kufariki dunia kwa mateso hayo. Tab'an wakati mwengine baadhi ya mawakili hao walikengeuka njia sahihi ya Imam (as), na kwa tadbiri yake na bila ya kuchelewa, mtukufu akawauzulu na kuwateua wawakilishi wengine badala yao.

Utukufu na karama za Imam Hadi (as) katika umri na uhai wake wote uliojaa baraka zilikuwa za kiwango na upeo wa juu kabisa kiasi kwamba watawala dhalimu wa Bani Abbasi walishindwa kuivumilia nuru hiyo ya uongofu licha ya hatua chungu nzima za mbinyo na mashinikizo walizokuwa wakichukua dhidi yake. Makhalifa wa Bani Abbas walijaribu kuiweka mbali jamii ya Kiislamu na fikra na mafundisho ya uongofu ya Imam Hadi (as) ili kufungua njia ya kueneza bid'a na fikra potofu ndani ya jamii na kwa njia hiyo kuweza kulinda utawala wao.  Mkabala na hayo, Imam naye alikuwa kila mara akifichua njama na kuweka hadharani mbinu za watawala hao za kujaribu kuwahadaa watu, ambapo katika fursa na minasaba tofauti alikifunua kizoro kilichoficha sura halisi ya kidhalimu ya watawala waonevu wa Bani Abbasi. Kwa sababu hiyo makhalifa hao wakawa wanauchukulia uwepo wa Imam Hadi (as) kuwa ni kizuizi na kizingiti kikubwa kinachowazuia kufikia makusudio na malengo yao ya uchu na ulafi wa madaraka. Walidhihirisha chuki na kinyongo walichokuwa nacho na Imam kwa namna mbalimbali; mpaka ikafikia hadi ya Mu'tazz, khalifa wa wakati huo wa Bani Abbasi kupanga njama maalumu ya kumwondoa moja kwa moja Imam, ambapo katika siku kama ya leo mwaka 254 hijria aliitekeleza kivitendo njama na kusudio lake hilo ovu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../  

 

 

Apr 01, 2017 06:30 UTC
Maoni