• Pamoja na Imam Hasan al Mujtaba AS (kwa mnasaba wa siku ya kuzaliwa kwake)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji. Mwezi 15 Ramadhani ni siku inayosadifiana na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam Hasan al Mujtaba, mjukuu mpenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW.

Imam Hassan AS ni mtoto wa Bibi Fatimatuz Zahra SA na Imam Ali bin Abi Talib AS, na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Bwana Mtume SAW kuhamia katika mji mtakatifu wa Madina. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali AS. Leo tumekuandalieni makala maalumu ya kuangalia kwa muhtasari sira, mwenendo na mafundisho ya kimaneno na kimatendo ya mtukufu huyu, tukianza kwa kutoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa Waislamu wote ulimwengu kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa mjukuu huyo wa Bwana Mtume tukimuomba Allah azitakabalie funga na ibada zenu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

 

Tarehe 15 Ramadhani miaka 1433 iliyopita yaani mwaka wa tatu Hijria ilichomoza nuru katika nyumba ya Bibi Fatima na Imam Ali AS na kuiangazia nyumba hiyo tukufu baada ya kuzaliwa mtoto ambaye aliondokea kuwa dhihirisho la ukarimu na wema ulimwenguni. Katika siku hiyo Imam Ali na Bibi Fatma AS waliruzukiwa ua lao la kwanza lenye harufu nzuri yaani Imam Hasan al Mujtaba AS ambaye aliongeza joto la mapenzi baina ya watukufu hao. Imam Hassan alikuwa ishara na dhihirisho la moja ya ndoa tukufu kabisa na mjukuu wa kwanza wa Mtukufu Mtume Muhammad SAW. Baada ya Mtume SAW kuletewa habari ya kupata mjukuu wake wa kwanza alifurahi mno na uso wake ulionekana ukiwa na bashasha na furaha kubwa. Masahaba walimiminika kwa Bwana Mtume ili kumpongeza na kumpa mkono wa kheri na fanaka Bwana Mtume, pamoja na Imam Ali na Bibi Fatimatuz Zahra AS. Baada ya kuzaliwa mtoto huyo, Mtume SAW alimuadhinia katika sikio lake la kulia na kusoma iqama katika sikio lake la kushoto. Katika siku ya saba, Mtume SAW alimfanyia akika kwa kuchinja kondoo na kisha kuigawa nyama hiyo kwa masikini na wasiojiweza. Kuanzia siku hiyo ikawa ni sunna kwa Waislamu kumchinjia mtoto kondoo au mbuzi katika siku ya saba ya kuzaliwa kwake na sunna hiyo inajulikana kwa jina la akika. Mjukuu mkubwa wa Mtume Muhammad SAW alikuwa dhihirisho la wema, fadhila, hisani na ukamilifu na hakuwa na mithili katika sifa hizo wakati wa zama zake.Alikuwa na sifa tukufu na za ukamilifu wa kibinadamu, sifa ambazo alizirithi kutoka kwa babu yake Bwana Mtume Muhammad SAW. Sifa nyingine aali alizojipamba nazo Imam Hassan AS ni uchaji Mungu, kushikamana na ibada, unyenyekevu, ushujaa, na kusamehe. Alikuwa akiwahimiza sana watu kujipinda kwa ibada ya kujiongezea elimu na kukuza akili zao. Katika sehemu moja ya maneno yake, mtukufu huyo amenukuliwa akisema: "Nawastaajabu wale watu wanaofikiria kushibisha matumbo yao, lakini hawajisumbui hata chembe kufikiria mambo ya ibada na kujifunza na kuzikuza akili zao" Kwa hakika Imam Hassan AS aliondokea kupendwa mno na Mtume SAW. Mapenzi makubwa ya Mtume SAW yalidhihirika zaidi pale aliposema:"Ewe Mwenyezi Mungu! Mimi nampenda Hasan, Wewe pia mpende na kila mwenye kumpenda Hasan, basi Mwenyezi Mungu pia atampenda."

*******

Moja ya sifa za wazi za Imam Hassan AS ambazo ni ruwaza njema kwa vipenzi vyake ni ukarimu wake wa hali ya juu. Imam Hassan alikuwa akimfanyia ukarimu mwenye kuhitaji mpaka anajiweza na kutokuwa mhitaji. Historia inaonyesha kuwa, mara mbili Imam Hassan alitoa kila alichokuwa nacho na mara tatu alitoa nusu ya mali yake katika njia ya Mwenyezi Mungu ili kuwafanyia ihsani watu wengine.Imenukuliwa kwamba, Imam Hassan al Mujtaba hakuwa akimrejesha mikono mitupu mtu yeyote aliyemuomba na katu hakuwa akimnyima aliyeomba bali daima alikuwa akitoa na kufanya ukarimu. Siku moja aliulizwa, inakuwaje, wakati wote humrejeshi mikono mitupu yeyote anayekuja kwako akitaradhia hali yake, mtukufu huyo alijibu kwa kusema: Mimi mwenyewe ni mwenye kumuomba Allah na mwenye matarajio kutoka Kwake Muumba. Ninaona vibaya sana kumrejesha mikono mitupu mwenye kuniomba, ilhali mimi mwenyewe ninataradhia hali yangu kwa Allah wakati wote. Mwenyezi Mungu amenizoesha kunipatia ujazi na neema Zake na mimi nimezoea mkabala wake kuwazingatia waja Wake na kugawana nao neema ninazopewa na Allah. Kisha Imam akaendelea kusema, pindi mwombaji na mhitaji anapokuja kwangu humwambia, ahlan wasahlan ewe ambaye umenipa fursa ya kutenda hisani na wema. Ninamuheshimu sana mtu huyo kwani hunipa fursa ya kutenda wema. Siku bora kabisa ya muungwana ni siku ambayo huja mtu kumuomba kitu na yeye akamkidhia haja yake.Katika kipindi chote cha maisha yake yaliyojaa baraka, Imam Hassan AS daima alikuwa akijishughulisha na kuwaongoza watu kuelekea katika njia ya haki. Muamala wake na watu wa kawaida hata maadui ulikuwa mzuri mno kiasi kwamba aliweza kumvutia kila mtu. Katika mafundisho ya Uislamu, matajiri wana majukumu mazito mbele ya wanaohitaji na wasiojiweza na wanapaswa kujitahidi kukidhi mahitaji ya wasiojiweza katika jamii.

 

Wapenzi wasikilizaji, haya ni matangazo ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kilichoko hewani ni kipindi maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Hasan al Mujtaba, mmoja wa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW.Kwa hakika Mitume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu katika mawaidha na vitendo vyao, walikuwa mfano wa kuigwa kuhusu masuala ya kuwapenda na kuwahudumia wanaadamu wenzao. Miongoni mwa hawa, Imam Hassan Mujtaba AS alikuwa na nafasi ya juu kwa mtazamo wa elimu, taqwa, fadhila na ibada. Katika suala la kuwasaidia na kuwahudumia mafukara na wasiojiweza, Imam Hassan alikuwa mashuhuri sana hadi kufika kiasi cha kupewa lakabu ya "Karim Ahlul Bayt" kutokana na ukarimu wake mkubwa.Uwepo uliojaa baraka wa mtukufu huyo ni jambo ambalo lilileta utulivu kwa watu maskini, mafukara na wasiojiweza. Imam Hassan AS alikuwa kimbilio la waliokumbwa na masaibu ya kila namna na nui, alikuwa tumaini la wanyonge na wasiojiweza na mtulizaji nyoyo za wenye hangaiko. Kama tulivyosema, haikuwahi kushuhudiwa hata mara moja, mwenye haja kwenda kwa mtukufu huyo na kurejea akiwa mikono mitupu.Zamakhshari ameandika katika kitabu chake cha Rabiul Abrar akinukuu hadithi kutoka kwa Anas bin Malik ya kwamba, siku moja mimi nilikuwa kwa Imam Hassan bin Ali AS, mara akaja kijakazi na kumpa zawadi ya maua Imam Hassan. Baada ya Imam Hassan kupokea maua yale akasema, uko huru katika njia ya Mwenyezi Mungu. Baada ya Anas bin Malik kushuhudia hayo akamwambia Imam kwa mshangao: Kijakazi huyu amekupa maua tu ambayo hayana thamani yoyote na wewe umemuachia huru? Imam alisema kumjibu Anas bin Malik kwamba: Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu alivyotufundisha. Allah anasema katika aya ya 86 ya Suratun Nisaa kwamba:"Na mnapoamkiwa kwa maamkio yoyote, basi nanyi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo..." Hivyo basi, jibu bora la wema wa kijakazi huyo ni kumuachia huru." Aidha imekuliwa katika vitabu vya historia kisa kifuatacho. Pamoja na kwamba Imam Hasan al Mujtaba AS alikuwa mkarimu sana, lakini pia alikuwa akihimiza watu wajitegemee na waongeze juhudi katika maisha yao ili wasihitajie misaada isipokuwa wakati wa dharura sana. Siku moja Bwana mmoja alikwenda kwa Imam Hassan AS na kumuomba amsaidie fedha. Alimkuta Imam Hasan akiwa pamoja na ndugu yake Imam Husain AS. Imam Hassan al Mujtaba akamwambia yule bwana: Haijuzu kuwaomba watu isipokuwa katika mambo matatu. Kuwa na wajibu wa kulipa dia, lakini mtu akawa hawezi kulipa, au deni ambalo mtu hana uwezo wa kulilipa au masikini ambaye hana uwezo wa kukidhi mahitaji yake. Je wewe unataka tukusaidie lipi katika ya haya matatu? Bwana yule akasema, shida yangu ni moja kati ya mambo haya matatu. Imam Hassan akatoa dinar 50 na kumpa yule bwana kwa heshima na taadhima. Imam Hussein kwa upande wake kwa heshima ya kaka yake akampatia bwana yule dinari 49 ambazo zilimkidhia haja yote aliyokuwa nayo. Kisa hiki kinatufunza pamoja na mambo mengine kwamba, tunapomsaidia mwenye haja na ikawa hali inaturuhusu, basi tumsaidie kiwango cha kukidhi haja yake, ili mtu huyo asilazimike kwenda kuomba kwa wengine.

 

Kwa hakika suala la kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuwasaidia wasiojiweza ni jambo ambalo limetiliwa mkazo mno katika dini tukufu ya Kiislamu na katika Qur'ani Tukufu. Aya nyingi za Qur'ani Tukufu zinabainisha namna wanaowasaidia wengine wanavyopata ujira mkubwa ambao ni ujira wa kudumu na kubakia milele. Kwa mtazmo wa Qur'ani ni kuwa, moja ya majukumu muhimu ya watu katika jamii ya Kiislamu ni kuwasaidia wahitaji na wenye shida. Kila mtu anapaswa kusaidia kulingana na uwezo wake. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 274 ya Surat al-Baqara kwamba:"Wale wanaotoa mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhaahiri, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika."Imam Hassan al-Mujtaba AS akiwa kiongozi mkubwa wa Waislamu alikuwa mstari wa mbele katika kutoa na kuwatatulia shida zao wahitaji na watu wasiojiweza. Alikuwa akiwasaidia na kuwapa utulivu na matumaini katika nyoyo zao. Si hayo tu, lakini pia alikuwa akikaa pamoja na maskini, akila nao, akiamiliana nao kwa wema n.k kama kinavyosema kisa hiki kifuatacho kutoka kwa mtukufu huyo:

*******

Kitanga kidogo cha chakula cha watoto mafakiri kilikuwa kimetandikwa chini ya kivuli cha mitende ya mji wa Madina. Watoto hao waliokuwa wamechangamka na wenye furaha walikizunguka kitanga chao hicho, na mkono kwa mkono wakawa wanakula chakula chao cha kinyonge cha vipande vya mikate mikavu na maganda ya mbatata yaliyokaushwa. Sauti ya upepo mwanana uliokuwa ukivuma na kuyasukuma matawi na majani ya mitende huku na huko, ikichanganyika na sauti za vicheko za watoto hao pamoja na zile za ndege waliokuwa wakizunguka huku na kule angani zilitoa mandhari yenye haiba na uzuri wa aina yake, uliomfanya kila aliyekuwa akipita njia kando ya watoto hao masikini, avutiwe na kuihusudu dunia ya watoto hao ambao hawakuonyesha hata chembe ya ghamu na huzuni kwa sababu ya umasikini wao. Hata hivyo hakuna hata mmoja kati ya wapita njia hao aliyekuwa tayari kukaribia kitanga cha watoto hao na kula chakula pamoja nao. Hata hivyo watoto hao hasa yule aliyekuwa mdogo kabisa kati yao aliyekuwa akiitwa Said hakuacha utaratibu wao wa kumwalika kula pamoja nao kila aliyekuwa akipita karibu yao. Siku moja walipokuwa wameshatandika kitanga chao tayari kujumuika pamoja kwa ajili ya chakula cha mchana, Said na wenzake walimwona kwa mbali mtu aliyepanda farasi akielekea upande wao. Wakati alipowakaribia, mmoja kati ya watoto hao alisema: "Mie namjua Bwana huyu! Baba yangu amesema hakuna mtu yeyote Madina aliye mfano wake. Yeye ni mwana wa Mtume". Mtoto mwingine alidakia na kusema: "Mimi nna hakika kama tutamkaribisha hatokubali kula nasi". Wote walinyamaza kimya. Said aliwatazama wenzake kisha akamsogelea yule bwana, na kwa sauti nzuri ya kitoto akamwambia:" Sayidi yangu! Tutafurahi kama utakuja kula na sisi". Bwana mpanda farasi hakuwa mtu mwingine bali Imam Hassan Mujtaba AS, mjukuu mpenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Alijibu ombi la Said kwa tabasamu. Alishika hatamu ya farasi wake na kwenda kumfunga kwenye kiguzo cha mtende. Wale watoto ambao walikuwa wameduwaa wakiwa hawaamini macho yao kwa kukubaliwa mwaliko waliotoa, walikimbilia kwenye kitanga chao cha chakula na wakaanza kuvikusanya haraka haraka vipande vikavu vya mikate na maganda ya mbatata na kuvitupilia mbali. Wakati Imam Hassan aliporudi kwenye mjumuiko wa watoto hao, wote kwa pamoja walitaka kuinuka. Said alikitupia jicho kitanga cha chakula kilichokuwa takriban kitupu vikiwa vimesalia vipande viwili vitatu tu vya mikate mikavu. Aliinamisha uso chini kwa aibu. Imam Hassan AS aliwataka watoto wakae. Kisha yeye mwenyewe akapinda goti na kuketi kando ya Said. Alichukua kipande kimoja cha mkate, na wakati yeye anaendelea kula, Said alisema: "Ingekuwa vizuri zaidi kama ungekuja mapema". Imam alimtazama mtoto mmoja mmoja kwa jicho la huruma kisha akainuka na kuwaambia: "Sasa nyote inukeni na twendeni kwangu ili muwe wageni wangu". Watoto hawakuyaamini masikio yao, kusikia kwamba shakhsiya mtukufu wa Madina anawaalika nyumbani kwake. Wakati Imam Hassan alipoinuka na kumshika mkono Said ili waanze safari yao mtoto huyo alijaribu kuificha sehemu iliyoraruka ya nguo aliyokuwa amevaa. Imam na Said walitangulia mbele na watoto waliobakia walifuata nyuma. Wakati Imam Hassan na wageni wake walipowasili nyumbani, watoto hao walichukuliwa hadi kwenye chumba kimoja ambacho dirisha lake lilikuwa linafungukia uwani. Walimsikia Imam Hassan akiwaambia wajakazi wake wapike kile chakula kitamu kabisa kwa ajili ya wageni wake. Watoto hawakuweza kutulia chumbani kwa furaha, kwani muda si muda harufu nzuri ya chakula kilichokuwa kikiandaliwa ilihanikiza kwenye anga ya chumba kizima. Muda si mrefu baadaye kitanga cha rangi mbali mbali kilitandikwa chumbani, na watoto wakakusanyika pamoja kula shibe yao chakula kitamu walichotayarishiwa. Baada ya kula walikaa kitako kumsubiri Imam Hassan AS. Baada ya kupita kama saa moja hivi Imam alirejea akiwa amefuatana na mtu aliyekuwa ameshika kikapu kikubwa mkononi. Walipomwona Imam Hassan watoto waliinuka kwa heshima na kumwamkia kwa pamoja yeye na mgeni aliyekuja naye. Yule mtu ambaye alikuwa ni fundi charahani mshonaji wa nguo alianza kutoa nguo za kupendeza za rangi mbali mbali zilizokuwemo ndani ya kikapu chake. Imam Hassan alitabasamu, kisha akamwita Said aliyekuwa mdogo zaidi kati ya watoto wote. Fundi charahani alitoa nguo moja ya rangi ya samawati na kumpimisha Said. Alipoona kuwa inamfaa alimtaka aende kwenye kona ya chumba na kubadilisha na ile ya mararu aliyokuwa amevaa. Alifanya vivyo hivyo kwa watoto waliobakia. Kwa hakika watoto wote walifurahi sana. Kwa moyo wa upendo na huruma Imam Hassan AS aliagana nao na kuwataka wasiache kwenda kumtembelea tena siku nyingine. Watoto walianza kuondoka mmoja mmoja na Said akawa ndiye wa mwisho kufanya hivyo. Imam Hassan alimwekea mkono kichwani na kuzipuna nywele zake kwa upendo kisha akaagana naye. Ama yule fundi mshoni ambaye alikuwa akiwaangalia kwa dirishani watoto wale waliokuwa wakienda zao huku wakiwa na furaha tele, alimgeukia Imam Hassan AS na kumwambia:" Ee Sayyid yangu hakika umewafanyia wema mkubwa watoto hawa. Imam ambaye kwa uso wa bashasha alikuwa akiendelea kuwapungia mkono watoto wale kuwaaga alimwambia fundi charahani: "Ukarimu wa watoto hawa kwangu ulikuwa mkubwa zaidi, kwani wao walinipa kile chote walichokuwa nacho, hali ya kuwa mimi nina zaidi ya kile nilichowapa wao." Fundi charahani alitikisa kichwa tu kuajabia ukarimu wa Imam Hassan. Alibeba kikapu chake, akapokea malipo ya nguo alizouza, na kuagana na Imam Hassan AS.

 

Naam wapenzi wasikilizaji, hiyo ni sehemu ndogo tu ya ukarimu wa Watu wa Nyumba wa Mtume wa Rehma, Muhammad al Mustafa, SAW. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa Waislamu wote ulimwenguni kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa mjukuu huyo wa Bwana Mtume, Imam Hassan bin Ali al Mujtaba AS, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Jun 10, 2017 03:10 UTC
Maoni