• Vazi la Staha la Hijab

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum. Msikilizaji mpenzi, tarehe 21 Tir kwa mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na tarehe 12 Julai mwaka wa Milaadia, ni siku ya staha na hijabu nchini Iran.

Chimbuko la siku hiyo inayoadhimishwa kila mwaka humu nchini, ni kukumbuka siku mfalme wa Iran Reza Khan alipotekeleza njama dhidi ya vazi la staha la Hijabu kwa msaada kamili wa mkoloni Muingereza. Tukio hilo lilitokea Mash’had, kaskazini mwa Iran baada ya askari wa mfalme huyo wa Kipahlavi kuwaua kwa umati Waislamu waliokusanyika katika msikiti wa Guhershad kupinga amri ya kutovaliwa vazi la Hijabu nchini Iran. Naam, moja ya matukio maovu kabisa dhidi ya Uislamu katika historia ya hivi karibuni ya Iran ni kupigwa marufuku vazi la Hijab na mfalme Reza Khan ambaye alirejeshwa madarakani baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 22 Februari 1921 yaliyoongozwa na Uingereza alikusudia kutekeleza sharia ya kupiga vita Uislamu na kupandikiza mila na desturi za Magharibi nchini Iran.

Wanawake wa Iran katika semina ya umuhimu wa vazi la staha la Hijab

 

Moja ya matukio makubwa ya wakati huo ni amri ya kupiga marufuku vazi la staha la Hijab. Hivyo katika kuandaa mazingira ya kupiga marufuku vazi la staha la Hijab, mfalme huyo wa Iran kibaraka wa Uingereza tarehe sita Dei 1307 iliyosadifiana na tarehe 27 Disemba 1928 alitumia bunge kupasisha amri yake ya kubadilisha mavazi ya wananchi wa Iran. Kwa mujibu wa sharia hizo, mavazi ya suti, tai na kofia za kizungu yalifanywa kuwa mavazi ya lazima kwa wananchi wanaume wa Iran. Waislamu wa Iran waliokuwa wanaona mbali walipinga vikali njama hizo za mfalme wa Iran dhidi ya Uislamu. Walipoonesha upinzani wao, askari wa mfalme huyo walitumia mkono wa chuma kuwaua kwa umati Waislamu hao huko Mash’had, kaskazini mashariki mwa Iran tarehe 12 Julai 1935. Aliyeongoza harakati hizo za kulinda na kutetea Hijab alikuwa ni mwanachuoni mkubwa Qommi. Tab’an njama hizo za kupiga marufuku vazi la Hijabu nchini Iran zilifeli. Siku hiyo leo hii inaadhimishwa kila mwaka hapa Iran kwa jina la Siku ya Hijabu. Sasa swali linalojitokeza hapa ni kwamba, kwa nini Waislamu wa Iran wa tangu zama hizo walisimama imara na kuwa tayari kumwaga damu zao kwa ajili ya kulinda vazi la staha la Hijabu? Leo hii wakati Waislamu kote ulimwenguni wanaposimama imara kulinda vazi hilo, wanafanya hivyo kwa nini? Majibu yako wazi, nayo ni kwa sababu dini yao tukufu ya Kiislamu imewaamrisha kufanya hivyo. Ni kwa sababu vazi la staha la Hijabu ni moja ya misingi muhimu ya dini hii ya Mwenyezi Mungu. Hapa chini tutagusia kidogo namna Uislamu na viongozi watukufu wa dini hii wanavyosema kuhusu Hijabu na staha ambayo haiwahusu wanawake tu, bali ni wajibu pia kwa wanaume. Karibuni.

Vazi la staha la Hijab halimzuii mwanamke kufanya kazi zake kwa ufanisi

 

Katika aya za 30 na 32 za sura ya 24 ya an Nur, Qur’ani tukufu inatoa amri kwa Bwana Mtume Muhammad SAW kwa kusema: Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za wanayoyafanya.

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyokhusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.

Naam wa kwanza kabisa kupewa amri hiyo ni wanaume kwamba wao nao ni wajibu wao kuchunga staha na kuinamisha macho yao na kulinda tupu zao kwani huo ndio utakaso. Lakini vile vile wanawake nao ni wajibu sambamba na kuinamisha nyuso na kulindatupu zao, waihifadhi pia miili yao na hiyo ni amri ya Mwenyezi Mungu ili pia waweze kupambanuka wanawake wenye heshima zao na wale wasio na heshima. Wakati hiyo ni amri, hivyo ni wajibu kwa kila Muislamu kusimama imara kuilinda na kuitetea kwa nguvu zote. Halafu staha na Hijab haimalizikii tu kwenye mavazi bali taqwa na ucha Mungu ndilo vazi bora kabisa. Katika aya ya ya 26 ya Sura ya Saba ya al Aaraf, Qur’ani Tukufu inasema: Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na nguo za pambo. Na nguo za uchamngu ndio bora.

Maadhimisho ya siku ya vazi la staha la hijab, Tehran, Iran

 

Hivyo vazi la staha na la Hijab kwa mujibu wa mafundisho ya Qur’ani Tukufu lina maana pana sana. Kujistahi na kuwa wacha Mungu ni katika hijabu bora kabisa. Katika makala hii fupi mbali na amri hiyo ya Qur’ani tutanukuu pia mafundisho ya viongozi watukufu wa Kiislamu kuhusiana na Hijabu kwa maana yake pana yaani

Kwa kuzingatia kwamba, wanawake wanaunda nusu ya watu wa jamii na wana nafasi muhimu katika kuleta na kueneza haya, staha, usafi na maadili katika jamii ya mwanadamu, viongozi wa dini tukufu ya Kiislamu wamelipa umuhimu mkubwa suala la staha na haya kwa wanawake kama ilivyokuja katika hadithi nyingi tofauti. Katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume (saw) inasema: Haya ni jambo zuri, lakini kwa wanawake ni jambo zuri zaidi.

Imam Ja’afar Swadiq AS amenukuliwa akisema kuhusiana na staha na haya kwamba: Haya ina vipengee kumi na vipengee tisa kati ya hivyo kumi vinapatikana kwa wanawake na kipengee kimoja kilichobakia kiko kwa wanaume.

Kwa hakika hadithi hizi zinabainisha kwamba, sehemu kubwa ya majukumu ya kuhifadhi hijabu, staha na maadili katika jamii iko mikononi mwa wanawake. Kwa kuzingatia uhakika huo, wanawake wanapaswa kuwa makini zaidi kuliko wanaume katika kuhifadhi hijabu, namna ya kuzungumza na hata katika utembeaji wao.

Tayari tumekunukulieni hapo juu aya ya 31 ya Surat Nur ambapo katika sehemu moja ya aya hiyo Mwenyezi Mungu anasema: Wala (wanawake) wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.

Maana ya amri hiyo ya Mwenyezi Mungu ni wanawake wa Kiislamu kujistiri kikamilifu na hilo ni jambo ambalo limeashiriwa katika aya iliyotangulia na wanawake wametakiwa kuiambatanisha pamoja miamala yao na kuona haya na soni. Kutoonesha uzuri wao kwa watu wasio maharimu kwao kwa wanawake waumini ni ishara na athari ya kuona haya na kuwa na staha na hiyo ndiyo maana halisi ya Hijab.

Hijab ni kwa ajili ya kuonyesha heshima na hadhi ya mwanamke wa Kiislamu

 

Mtume Muhammad (saw) anabainisha na kutambulisha mavazi ya wanawake kwa wanaume ambao si maharimu wao kwamba, ni kigezo cha ubora wa mwanamke. Anasema: Wanawake wenu walio wabora ni wanawake wenye staha, ambao hujipamba kwa ajili ya waume zao tu, na hujistiri kikamilifu kwa wasiokuwa waume zao.

Siku moja Bwana Mtume (saw) alisema: Je nikuambieni wanawake wabaya kabisa kwenu nyinyi ni wepi? Kisha akasema: Wanawake wenu walio wabaya kabisa ni wale wanaojipamba mbele ya wengine lakini hujifunika na hawaoni ulazima wa kujipamba mbele ya waume zao.

 

Jul 12, 2017 10:19 UTC
Maoni