•  Watu wa Asili, Tabaka Lililokandamizwa Zaidi katika Dunia ya Leo

Tarehe 23 Disemba mwaka 1994 Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe 9 Agosti kila mwaka kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Watu wa Asili (Indigenous). Siku hiyo ilitangazwa rasmi ili kukumbuka na kutetea haki za zaidi ya watu milioni 370 wa asili katika nchi 90 duniani.

Tangu wakati huo siku hii imekuwa ikiadhimishwa kwa ajili ya kuwakumbuka maelfu ya wanaume na wanawake wa asili wanaoshikamana na mila, tamaduni na desturi zao.  

Siku ya Kimataifa ya Watu wa Asili

Siku hiyo iliainishwa kwa mara ya kwanza kabisa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Disemba 1994 kwa mnasaba wa mkutano wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na watu wa asilia uliofanyika mwaka 1982. Kwa mnasaba wa siku hiyo ya kimataifa, Umoja wa Mataifa hutayarisha masomo na warsha katika nchi mbalimbali duniani ili kuwatanabahisha walimwengu kuhusu haki za watu wa asili. Katika nchi kama Venezuela, Peru, Bolivia, Ecuador, Paraguay, Mexico na nchi nyingine za America ya Latini na Caribia, siku hii ya kimataifa huadhimishwa kwa mahfali na sherehe za aina yake.

Watu wa asili (Indigenous) ni makundi na mataifa ambayo yanadai kuwa, yana mfungamano makhsusi wa kihistoria na kiutamaduni na jamii za ardhi au eneo lao la asili. Neno hili hutumika kumaanisha wakazi wa awali na wenyeji wa kila nchi. 

Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa asili lililopasishwa tarehe 13 Disemba 2007 linasema kuwa, watu wa asili ni watu wenye utamaduni, mila na desturi makhsusi zinazotajirisha utamaduni na ustaarabu wa walimwengu, na kutokana na mfungamano wao na ardhi na mazingira yao, wana kanuni makhsusi za kulinda mila na utamaduni wao. Watu hawa kama yalivyo mataifa mengine, wana haki zao za kibinadamu na hawapasi kubaguliwa na kunyimwa haki hizo.

Hii leo inakadiriwa kuwa, kuna watu  wa asili (Indigenous) karibu milioni 370 katika nchi 90 duniani. Hii ina maana kwamba, asilimia 5 ya jamii ya watu wote duniani inaundwa na watu wa asili (Indigenous). Hata hivyo watu hawa wanahesabiwa kuwa ni sehemu ya asilimia 25 ya watu masikini zaidi duniani. Utafiti wa filolojia au taaluma ya kukua kwa lugha umeonesha kuwa, watu wa asili wana lugha karibu elfu saba (7000) na wanawakilisha tamaduni elfu tano (5000) tofauti na makhsusi.

Watu wa asili wana utamaduni maksusi na uhusiano wa aina yake na mazingira yao. Wana sifa zao za kiutamaduni, kiuchumi, kijamii na kisiasa ingawa wote katika meneo mbalimbali ya duniani wanashirikiana kuhusu matatizo yanayowapata na ukiukwaji mkubwa wa haki zao.

Watu wa asili kwa miaka mingi sasa wamekuwa wakifanya jitihada za kutambuliwa rasmi utambulisho wao, aina na mtindo wa maisha, haki zao kwenye ardhi na maeneo yao ya asili na kihistoria, mazingira na maliasili zao na wanapambana kwa ajili ya haki hizo. Katika kipindi kirefu cha historia haki za binadamu na za kimsingi za watu hawa zimekuwa zikikanyagwa na kukandamizwa. Ni kwa msingi huo ndiyo maana jamii ya kimataifa ikaweka vigezo na nyenzo maalumu za kuinisha haki za watu wa asili ili kuweza kulinda haki, tamaduni na mtindo wao wa maisha.

Azimio lililopasishwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watu wa asili ni miongoni mwa nyaraka muhimu za kimataifa kuhusu haki za tabaka hili la wanadamu na linajumuisha mwafaka wa kimataifa kuhusu haki hizo ikiwa ni pamoja na kuainisha vigezo vya kulinda uhai, utukufu na huduma bora kwa wanadamu hawa.

Utekelezaji wa azimio hilo katika muongo uliopita umeboresha kwa kiwango fulani hali ya watu wa asili katika ngazi ya kitaifa, kikanda na hata kimataifa. Hata hivyo bado kuna baadhi ya nchi ambazo hazijafikia viwango vya kimataifa na vinavyotakikana kuhusu masuala ya kuwatambua rasmi watu wa asili na haki zao.

Ushahidi unaonesha kuwa, licha ya maazimio, mikataba na makubaliano yote ya kimataifa kuhusu udharura wa kulindwa watu wa asili lakini kunashuhudiwa ukiukwaji mkubwa wa haki zao hususan katika nchi za kaskazini mwa Amerika na Australia. Kwa mfano tu watu wa asili katika nchi ya Canada hususan wanawake wanasumbuliwa na ukiukwaji mkubwa na unaofanyika kwa mpangilio maalumu wa haki za binadamu, suala ambalo limekabiliwa na upinzani na malalamiko makubwa ya jumuiya za kutetea haki za binadamu na Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa. Kipindi fulani pia Wahindi Wekundu wa Marekani walikuwa wakikabiliwa na dhulma na ukiukwaji mkubwa wa haki zao. Huko Australia pia watu wa asili wanasumbuliwa na vitendo vya ukandamizaji na ukiukwaji wa haki zao, na vizazi vya watu hao daima vimekuwa vikisulubiwa na kukandamizwa.

Ripoti iliyotolewa na Amnesty International inasema kuwa: Watu wa asili katika nchi mbalimbali duniani wanasumbuliwa na ubaguzi, vitisho, ubakaji na mienendo mibaya. Mwaka huu katika sherehe za kuadhimisha miaka mia moja ya uhuru na kujitawala Canada, wakati wananchi walipokuwa katika sherehe za uhuru, jamii ya watu wa asili ya nchi hiyo ilifanya mandamano kulalamikia miaka 150 ya ukandamizaji wa serikali na mauaji ya kizazi chao yanayofanywa na vyombo vya dola.

Maandamano ya watu wa asili wa Canada

Ripoti zinaonesha kwamba, nchini Canada katika miaka mitano iliyopita idadi ya wafungwa wa jamii ya watu asili wa nchi hiyo imeongezeka sana. Ripoti hizo zinasema, ongezeko la asilimia 43 la watu wa asili katika jela za Canada limewafanywa wafungwa wa jamii hiyo katika jela za nchi hiyo kufikia asilimia 23 ya wafungwa wote nchini humo. Hii ni pamoja na kuwa, jamii ya watu wa asili ni asilimia 4 tu ya watu wote wa Canada!

Nukta ya kutiliwa maanani hapa ni kuwa, katika muongo uliopita, kiwango cha wafungwa wa kike wa jamii ya watu wa asili nchini Canada kimeongezeka kwa asilimia 80 na wengi wao wanakabiliana na mwenendo mbaya. Mfungwa mmoja wa kike kati ya kila watano wao ana umri wa juu ya miaka 50. Wastani wa kiwango cha elimu cha wafungwa hao ni darasa la nane, asilimia 80 ya wafungwa hao ni waraibu wa dawa za kulevya na asimia 80 miongoni mwa wafungwa hao wa kike wa asili wa Canada wamebakwa na kunajisiwa. Vilevile takwimu zinonesha kuwa, asilimia 31 miongoni mwao wameambukizwa ama maradhi ya hepatitis c yaani homa ya ini aina na c, au Ukiwi, na zaidi ya nusu yao wanahitaji huduma za madaktari wa elimu nafsi na saikolojia.

Inasikitisha kuona kwamba, idadi ya wafungwa wa jamii za waliowachache nchini Canada imeongezeka katika muongo uliopita kwa asilimia 75 na kiwango cha wafungwa wa kike wa jamii ya watu wa asili kimeongezeka kwa asilimia 80.

Takwimu ya Idara ya Wafungwa na Magereza ya Canada zinaonesha kuwa, idadi ya wafungwa wanaowekwa katika seli za mtu mmoja mmoja imeongezeka katika magereza ya nchi hiyo na kwamba, idadi hiyo ilifikia wafungwa elfu 8,221 katika mwaka 2012 na 2013. Kiwango kikubwa zaidi cha wafungwa wanaoshikiliwa katika seli za mtu mmoja kimeripotiwa katika majimbo ya Ontario, Québec na Prairies. Takwimu hizo zinasema kuwa, thuluthi mbili ya wafungwa wa baadhi ya magereza za nchi hiyo ni watu wa asili (Indigenous) na kumetolewa wito wa kuachiwa huru watu wa jamii hiyo kwa sababu wengi wao sio tishio kwa jamii ya Canada.  

Maandamano ya kupinga mateso dhidi ya wafungwa katika jela za Canada

Wapenzi wasikilizaji Siku ya Kimataifa ya Watu wa Asili (Indigenous) inaadhimishwa kuwakumbuka na kuwaenzi watu wanoshikamana na kuheshimu mila, ada na desturi zao za jadi katika nchi mbalimbali kote duniani. Siku hii ni fursa nzuri ya kupaza sauti za kutetea haki za watu wa tabaka hilo kote duniani ambao mbali na kupigania haki zao, wanafanya jitihada kubwa za kulinda na kuboresha dunia yetu ikiwa ni pamoja na mazingira tunamoishi.

Aug 09, 2017 18:38 UTC
Maoni