• Kwa Mnasaba wa Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Imam Hadi (as)

Nyoyo za Waislamu ziling'ara na kufarijika kufiatia uzawa wa Imam wa Kumi wa Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw), al-Imam al-Hadi (as).

Imam Hadi (as) alizaliwa tarehe 15 Dhul Hijja  mwaka 212 Hijiria katika mji mtakatifu wa Madina. Alipewa lakabu ya al-Hadi kwa maana ya muongozaji. Mtukufu huyo aliufanya mji wa Madina kuwa makao makuu yake ya kutekelezea majukumu yake muhimu ya Uimamu na vilevile ya kuenezea mafundisho ya Kiislamu. Alitekeleza vyema jukumu hilo la kuongoza jamii ya Kiislamu kwa muda wa miaka 33. Katika zama hizo umashururi wa Imam Hadi (as) alienea kwa kasi katika maeneo yote ya karibu na mbali na kuwafanya watu waliokuwa na kiu kubwa ya kupata elimu na maarifa ya Kiislamu kukimbilia kwake mjini Madina kwa lengo la kunufaika na elimu kubwa aliyokuwa nayo katika uwanja huo. Muhammad bin Shahrashub ni mmoja wa wanahistoria wa Kiislamu ambaye amefanya utafiti na kuandika kwa mapana na marefu historia ya Ahlul Beit wa Mtume (saw). Anaandika katika kitabu chake cha Manaqib juu ya maadili mema na akhlaqi ya kuvutia ya Imam Hadi (as) kwa kusema: ''Alikuwa mtu aliyekuwa na roho mzuri na msema ukweli zaidi kati ya watu. Alipokaa kimya uso wake uling'ara kwa utukufu maalumu na alipozungumza maneno na shakhsia yake ilikuwa ikiwavutia wote.''


Imam Ali an-Naqi al-Hadi (as) ni mfano bora wa neema na rehema ya Mwenyezii Mungu ambayo amewajaalia waja wake kama Hoja kwao. Yeye ni nuru na taa ambayo imewekwa kwenye njia ya ukamilifu wa mwanadamu ili wale waliopotea na kukwama njiani waweze kuongozwa na taa hiyo kwenye njia nyoofu inayowaelekeza kwa Mola wao. Sira na mwenendo wake wa maisha pia ni mfano bora kwa wale wanaotafuta ukamilifu. Ni mmoja wa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) ambaye maneno na tabia zake zinamuainishia mwanadamu maisha bora na uwepo wake kuwa dhihirisho halisi  la thamani safi za mbinguni. Katika kuwaarifisha Ahlul Beit wa Mtume Mtukufu (saw), Imam Hadi (as) anasema: ''Maimamu ni madini ya rehema, hazina ya elimu, kilele cha uvumilifu na huruma, misingi ya utukufu, wachujwa na wateule wa Mitume, taa za giza.... na Hoja za Mwenyezi Mungu kwa walimwengu.''

Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Hadi (as) alishika hatamu za Uimamu mwaka 220 Hijiria alipokuwa na umri wa miaka minane tu. Katika zama za uongozi wake utawala wa Bani Abbas ilikuwa ukidhoofika taratibu na kuelekea ukingoni. Ayashi na Migsari walikuwa watawala wawili dhalimu wa Bani Abbas ambao dhulma na mateso yao dhidi ya watu yalikuwa yamewapelekea kuwachukia sana na kuwafanya wawakimbilie Ahlul Beit (as). Kama walivyokuwa babu zake, tabia na maadili bora na safi ya Imam Hadi (as) yaliwapelekea watu hao waliokuwa wamechoshwa na dhulma na uonevu wa watawala dhalimu wa Bani Abbas kupokea kwa moyo mkunjufu tabia hizo njema na za mapenzi na huruma za Imam Hadi (as). Hali hiyo pamoja na zuhudi kubwa aliyokuwa nayo Imam iliwavutia sana watu hao na hivyo kufanya wapenzi na wafuasi wa Ahlul Beit (as) kuongezeka siku baada ya nyingine. Tabia hiyo njema ya Imam (as), ambaye aliweza kuishi na makhalifa sita wa Bani Abbas, iliwafanya watu kufuatia njia sahihi, yaani mafundisho halisi ya Uislamu. Watawala hao waovu walisumbua na kumtesa sana Imam katika kipindi cha uongozi wake wa Umma wa Kiislamu. Hatimaye wa mwisho wao yaani Mu'tassim, alimpa sumu na kumuua shahidi Imam (as). Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba licha ya watawala hao dhalimu kuwa katika kilele cha nguvu za kidhahiri humu duniani lakini waliishi na kuaga dunia kwa madhila makubwa ambapo wanakumbukwa katika historia kuwa watawala waliotawala kwa dhulma na ukatili mkubwa. Katika upande wa pili Imam  (as) licha ya kudhulumiwa na kuteswa na madhalimu hao lakini aliweza kufanikisha Uislamu kuenea kwa kasi  katika pembe tofauti za dunia na kuongeza idadi ya Waislamu katika maeneo hayo.

Uzingatiaji wa lakabu ya Imam Ali an-Naqi (as) yaani al-Hadi unaweka wazi hakika nyingi mno. Neno 'hidaya' Katika lugha ya Kiarabu lina maana ya kuonyesha njia na kufikisha mahala panapokusudiwa, ambapo kwa kawaida huwa ni mahala pazuri na chanya. Katika utamaduni wa Quráni na maarifa ya Ahlul Beit (as) neno hili lina maana ya kina zaidi kuliko makusudio ya kidhahiri na kijiografia tu. Kuijua vyema njia, mahala pa kufikia, kuelewa umma na walio kwenye msafara, kutambua vikwazo na matatizo ya njiani, kuhamasisha wasafiri kwa ajili ya kufanya harakati, kuhamasisha moyo wa ukakamavu miongoni mwa wasafiri na kuonyesha njia na kuongoza msafara ni sehemu ya maana ya neno 'hadi' katika utamaduni wa Kiislamu. Imam Hadi (as) alikuwa jua lililongára ambalo katika miaka ya 220 hadi 254 Hijiria alichukua usukuani wa kuongoza Umma mkubwa wa Kiislamu ambapo kwa kipindi cha karibu miaka 34 alikuwa nahodha shupavu wa meli ya Kiislamu katika mawimbi makali na ya kutisha ya zama za watawala dhalimu wa Bani Abbas.


Kama ilivyokuwa katika zama za mababu zake watukufu, kipindi cha Imam Hadi (as) kilikuwa chanzo cha hekima na madini ya elimu na maarifa. Fikra nyingi za kiitikadi zilijitokeza pamoja na nadharia tofauti kuhusiana na misingi ya itikadi ya Kiislamu, nadharia potovu ambazo kwa hakika zilikuwa zinahatarisha na kupotosha fikra halisi za Uislamu. Kutokana na kipawa chake kikubwa cha maarifa ya Kiislamu, nuru ya hidaya na mwongozo wake, Imam Hadi (as) aliweza kufunga milango mingi ya upotovu huo na wakati huo huo kubainisha kwa usahihi na uwazi mkubwa fikra halisi za Uislamu, na hivyo kudhoofisha na kuzifanya kutokuwa na maana fikra batili zilizokuwa zikienezwa na maadui wa Uislamu.

Mbali na kuhuisha mafundisho na maarifa ya Kiislamu, Imam alikuwa mstari wa mbele katika kushugulikia masuala mbalimbali ya kijamii na kutatua matatizo ya watu, kwa kadiri kwamba hakuna mtu yoyote aliyetoka nyumbani kwake hali ya kuwa amekata tamaa.

Wakati wa kuabudu na kumuomba Muumba wake, Imam Hadi (as) alikuwa akionyesha unyenyekevu mkubwa kwake. Alionyesha utiifu na utegemezi mkubwa kwa Mola wake maishani kwa kadiri kwamba wanazuoni wakubwa wa Kiislamu kama Ibn Kathir wanamsifu Imam huyo kwa kusema: "Alikuwa mcha Mungu mwenye takwa na zuhudi kubwa. Mawasiliano na Mwenyezi Mungu humpa mwanadamu utukufu, heshima na adhama maalumu. Viongozi wa mbinguni ambao huzama kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu hupata nguvu ya kimaanawi na ushawishi mkubwa. Mapenzi yao hupenya kwenye nyoyo za watu na maneno yao kulainisha nyoyo na kuzitayarisha.''

Kuwaongoza wanadamu na kuwaelekeza kwenye mambo mema huhitajia maarifa mengi na ya hali ya juu, ambayo hujumuisha pande zote za maisha yao. Viongozi wote maasumu walikuwa na maarifa hayo. Katika moja ya matamshi yake ya kuvutia Imam Hadi (as) anasema: ''Jina Tukufu (Ism  al A'dham) la Mweyezi Mungu lina herufi 73 ambapo Asif ibn Barkhiya alikuwa akijua herufi moja tu kati ya herufi hizo. Alitamka herufi hiyo na ardhi kati yake na Saba ikafunguka na hivyo kumuwezesha kumletea Nabii Suleiman (as) kiti cha enzi cha Malkia Bilqis katika muda mfupi sana ulio chini ya kupepesa jicho. Herufi 72 kati ya hizo tunazo sisi na Mwenyezi Mungu amejiwekea herufi moja ambayo inahusiana na elimu ya gheib.''

Kustawi na kukamilika kwa shakhsia ya watu pamoja na kusifika kwa sifa bora za kiutu ni jambo lililokuwa na umuhimu na thamani kubwa kwa Imam Hadi (as). Kwa msingi huo alikuwa akiwafundisha watu njia na mbinu za kuishi maisha bora humu duniani. Alikuwa akisema: ''Tahadhari na mtu ambaye hajijali wala kutambua thamani yake.'' Pia akisema: ''Uhasidi, huharibu mambo mema na uongo kuleta uadui."

Kwa mara nyingine tena wapenzi wasikilizaji, tunakupeni mkono wa hongera, pongezi na fanaka kwa mnasaba huu adhimu wa kukumbuka uzawa wa Imam wetu Mtukufu al-Imam Ali an-Naqi (as). Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Sep 05, 2017 17:30 UTC
Maoni