• Kwa Mnasaba wa Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Imam Musa Al-Kadhim (as)

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Wasikilizaji wapenzi, tuko kwenye siku ya maadhimisho ya kuzaliwa Imam Musa Al-Kadhim (as) mmoja wa wajukuu vipenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Imam Kadhim (as) ni shakhsia mkubwa ambaye mengi mno yamesimuliwa kuhusu sifa na utukufu wake kwenye vitabu vya Kishia na pia vya Kisuni.

Miongoni mwa waliomzungumzia Imam huyo mtukufu ni Ibn Talha, alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kisuni ambaye amesema: "Yeye ni Imam mwenye hadhi kubwa, utukufu adhimu, mkithirishaji ibada za usiku, mwenye idili kubwa katika mambo, mtu ambaye alikuwa mashuhuri kwa karama na ufanyaji ibada na kujichunga katika kumtii Allah. Usiku akiupitisha kwa kisimamo na kusujudu na mchana kwa saumu na utoaji sadaka. Na akaitwa Kadhim kwa upole na usamehevu mkubwa mno aliokuwa nao kwa waliomkosea. Mtu aliyemtendea ubaya alikuwa akimlipa kwa kumtunukia wema na ihsani. Waliokuwa wakimtendea jinai akiamiliana nao kwa usamehevu. Na kutokana na kukithirisha kufanya ibada alipewa jina la Abdus-Salih, yaani mja mwema; na katika ardhi ya Iraq alikuwa maarufu kwa lakabu ya "Babul-hawaij"; kwa sababu watu waliokuwa wakitasawali kwa Mwenyezi Mungu Mola Mweza kupitia kwake, walikuwa wakikidhiwa haja zao. Karama zake zinazishangaza akili za watu"…

Tukiwa tumo kwenye maadhimisho ya kuzaliwa Imam Musa Al-Kadhim (as) kabla ya kuendelea mbele na mazungumzo yetu tunaashiria kwanza hadithi hii tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW pale mtukufu huyo aliposema:

انی تارک فیکم الثقلین کتاب الله و عترتی اهل بیتی ما إن تمسکتم بهما لن تضلوا و إنهما لن یفترقا حتی یردا علی الحوض

Hakika mimi ninakuachieni nyinyi vizito viwili, Kitabu cha Allah na kizazi changu watu wa Nyumba Yangu ambavyo kama mtashikamana navyo katu hamtapotea; navyo havitatengana mpaka vitakapoingia nami katika hodhi".

Katika siku hii tukufu, nasi pia tunanyoosha mikono yetu kushikamana na kamba ya Imam Musa Al-Kadhim (as), kwani kushikamana na vyote viwili, yaani Qur'ani na Ahlul-Bayt wa Bwana Mtume SAW ndiko kutakotuepusha na kupotoka na kukengeuka njia ya uongofu. Tab'an maana ya kushikamana na vizito viwili hivyo si kuvipenda na kuviheshimu tu au kuviitakidi kuwa ni vitu vitakatifu. Kushikamana na Qur'ani, maana yake si kuushika msahafu kwa heshima tu na kuubusu kisha kuutafutia pahala pazuri pa kuuhifadhi usiingie vumbi. Au kushikamana na kumpenda Imam si, mathalan kama ingekuwepo, kuchukua picha yake tukaitia fremu kisha tukaitundika ukutani. La hasha. Kushikamana na vizito viwili hivyo ni kufuata na kutekeleza kivitendo maamrisho ya Qur'ani na sira za viongozi hao wateule na kuvifanya kuwa ndio kigezo na dira ya kufuata katika maisha yetu ya kila siku.

Wapenzi wasikilizaji, ninachukua fursa hii kukupeni mkono wa heri na baraka kwa mnasaba huu mtukufu wa kuadhimisha kuzaliwa Imam wa saba wa wafuasi wa Ahlul-Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Imam Musa Al-Kadhim (as) na kukukaribisheni kusikiliza machache niliyokuandalieni kuhusu maisha na sira ya mtukufu huyo.

Imam Musa Kadhim (as) alizaliwa katikati ya mwezi wa Mfunguo Tatu Dhilhijjah mwaka 128 hijria katika kijiji cha Abwaa kilichoko baina ya Makka na Madina. Alipotimia miaka 20 na baada ya kufa shahidi baba yake, yaani Imam Jaafar As-Sadiq (as), mtukufu huyo alibeba jukumu na mas-ulia ya kuongoza umma wa Kiislamu. Katika kipindi cha miaka 35 ya Uimamu wake, kuanzia mwaka 148 hadi 183 hijria, Imam Musa Al-Kadhim alikuwa akiwabainishia watu kwa njia na sura tofauti mfumo matulubu wa kisiasa na kijamii wa Uislamu.

Kipindi cha maisha ya Imam Musa Kadhim (as) kilisadifiana na tawala za makhalifa kadhaa wa Bani Abbas, zama ambazo uimla na udhalimu wa watawala wa Bani Abbas ulifikia kilele. Imam hakunyamazia kimya dhulma na uonevu uliokuwa ukifanywa na makhalifa wa Bani Abbas, na akawa anazipinga tawala zao kwa njia mbalimbali. Na hilo ndilo lililomfanya mtukufu huyo apitishe sehemu kubwa ya maisha yake mbali na watu akiwa gerezani au uhamishoni! Hata hivyo dhulma na jinai zisizo na hesabu alizofanyiwa Imam Musa Al Kadhim (as) hazikumfanya asite kutekeleza jukumu lake la uelimishaji na kuuonyesha umma njia ya uongofu. Kila alipopata fursa mwafaka, mtukufu huyo aliwafikishia watawala hao madhalimu ujumbe na wito wa mwamko. Katika moja ya barua za indhari na tanbihi ambayo Imam Musa Kadhim (as) aliiandika akiwa jela na kuituma kwenye kasri la utawala wa Harun Al-Rashid, mtukufu huyo aliandika hivi: "Kila siku moja ipitayo kati ya masiku yangu haya ya tabu, inapita pia siku moja kati ya siku zako za raha, mpaka itafika siku ambayo mimi na wewe tutakutana mahala pamoja. Huko, watu wa batili watabainikiwa na hasara ya amali zao".

Jina la Imam Musa Al-Kadhim (as) kwenye ukuta wa Masjidu-Nabiy, Madina

Harun Al-Rashid, alikuwa mmoja wa makhalifa madhalimu na wenye kutakabari wa ukoo wa Bani Abbas, ambaye utawala wake ulienea na kufika hadi maeneo mengi ya mbali. Kwa dhulma laisal-kiyasi alizokuwa akiwafanyia watu, Harun alitaka kujionyesha kuwa yeye ni mtawala mwenye nguvu na mamlaka imara. Alikuwa akilielekea jua na kuliambia: Ewe jua, kokote kule unakotaka kuangaza, angaza. Kote huko yako mamlaka na utawala wangu! Lakini ukweli ni kwamba Harun Al-Rashid hakupendeza wala hakuwa na nafasi yoyote ndani ya nyoyo za watu zaidi ya kutawala viwiliwili vyao tu. Imesimuliwa kuwa "siku moja Imam Musa Al-Kadhim (as) alikuwa amekaa kando ya Al-Kaaba. Wakati Harun alipomwona Imam alimwambia: Wewe ndiye mtu ambaye watu wanakupa mkono wa bai'a kwa kificho? Imam aliitikia kwa kutikisa kichwa taratibu, kisha akamwambia: "Mimi ni Imam wa nyoyo na wewe ni Imam wa viwiliwili".

Mapenzi makubwa mno kwa Imam Kadhim (as) yalikuwa yamejaa ndani ya nyoyo za watu wa matabaka tofauti. Mtufuku huyo ambaye alitokana na kizazi cha Bwana Mtume SAW akiwa amebeba hazina adhimu ya elimu na maarifa, alifanya kazi kubwa ya kuwaongoza na kuwaelekeza watu kwenye uongofu. Duara la mvuto na ushawishi wa Imam Musa Al Kadhim (as) lilikuwa pana, kiasi kwamba wakati mwengine, hata baadhi ya wakuu wa utawala wa Harun walikuwa wakienda kwa siri kwa mtukufu huyo ili kumkabidhi mafungu yao ya malipo ya Zaka na Khumsi pamoja na misaada yao ya sadaka. Naye Imam akawa anazigawa mali hizo kuwapatia watu hasa wanyonge na masikini.

Akiwa ni Imam na kiongozi halisi wa watu, Imam Kadhim (as) alifanya kazi ya kuwaelimisha na kuwapa miongozo ya uongofu watu hao waliokuwa na kiu na shauku ya kubainishiwa mafundisho safi na asili ya Uislamu. Mtukufu huyo alikataa kuwa na ushirikiano wa aina yoyote na utawala dhalimu uliokuwepo katika zama zake, kwa sababu kushirikiana nao kungeipa nguvu na kuiimarisha misingi ya dhulma na uonevu. Lakini pamoja na hayo, zilikuwepo kesi na hali maalumu ambazo zilimfanya Imam aafiki baadhi ya wafuasi wake mahsusi kushika nyadhifa katika utawala wa Bani Abbas. Kwa kutoa mfano, Ali bin Yaqtin alishika wadhifa wa kuwa waziri wa Harun Ar-Rashid kwa ridhaa ya Imam Kadhim (as) ili kwa njia hiyo aweze kulinda na kunusuru maisha na mali za wafuasi wa Ahlul-Bayt wa Bwana Mtume SAW. Imam alikuwa akimwambia Ibn Yaqtin: "Ndani ya mjumuiko wa madhalimu, Mwenyezi Mungu huwa na mawalii wake pia, ambao kupitia kwao wao huwasaidia na kuwahami waja wake wema. Huenda kupitia kwako wewe, Mwenyezi Mungu atawaepushia masahibu zako moto wa fitna wa wapinzani". Ali bin Yaqtin alikuwa akichukua hatua mbalimbali pia za kuwasaidia watu wanyonge waliokuwa wafuasi wa Ahlul-Bayt wa Bwana Mtume SAW. Moja ya hatua hizo ni kwamba kutokana na ushawishi aliokuwa nao katika kasri la utawala wa Bani Abbas, kwa idhini ya Imam Kadhim (as), Ali Ibn Yaqtin alikuwa kila mwaka akiwapeleka Hija baadhi ya watu wanyonge na kutumia kisingizio hicho kuwasaidia kifedha. Vilevile alikuwa akizichukua fedha za kodi ambazo utawala wa Bani Abbas ulikuwa ukiwatoza watu wanyonge na wasio na uwezo na kuwarejeshea wenyewe kwa kisirisiri.

Imam alipewa lakabu la "Kadhim" kwa sababu alikuwa kila mara akizuia na kudhibiti ghadhabu zake. Sira na maisha ya Imam Musa Al Kadhim (as) yanaonyesha kuwa kila lilipohusu suala la kulinda na kuihami dini, mtukufu huyo alikuwa tayari kufa shahidi na wala hakukubali kufikia maridhiano na mapatano ya namna yoyote na mtu yeyote yule. Kwa hivyo inapozungumziwa sifa ya kudhibiti ghadhabu na kusamehe katika maisha ya Imam Musa al Kadhim (as) na ambayo ilimfanya mtukufu huyo awe maarufu kwa lakabu ya "Kadhim" yaani mwenye kudhibiti hasira, hilo linahusiana na maisha ya binafsi katika kuwasamehe watu na kujitolea kwa ajili yao. Uungawana, akhlaqi njema na tabia nzuri yenye mvuto mkubwa aliyokuwa nayo Imam Kadhim (as) ilikuwa ya namna ambayo iliwaathiri hata walinzi wa jela ya utawala wa Bani Abbas licha ya kuwa na nyoyo katili na za ukhabithi. Mmoja wa walinzi wa jela ya Basra alisimulia haya yafuatayo kuwaeleza wakubwa wake: "Nimejitahidi sana kufuatilia nyendo na hali zote za Musa Ibn Kadhim. Mpaka nimefikia hadi ya kutegea sikio kwa siri na kusikiliza dua anazoomba. Lakini licha ya shida na tabu zote za jela, yeye muda wote alikuwa akivumilia na kuonyesha subira huku akiomba rehma na maghufira tu kwa Mwenyezi Mungu".

Wapenzi wasikilizaji, kwa mara nyengine tena nachukua fursa hii kukupeni mkono wa heri, baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuadhimisha kuzaliwa kwa Imam Musa Al Kadhim (as) na tunahitimisha kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba huo kwa kunukuu maneno matukufu ya Imam huyo mwema aliposema: "Kuwa na uelewa na utambuzi wa dini ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu kufahamu hukumu na maamrisho ya Mwenyezi Mungu ndio ufunguo wa kuwa na basira, kukufanya uwe na ukamilifu katika ibada na kufikia cheo na daraja ya juu ya dini na ya dunia". Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Sep 10, 2017 07:35 UTC
Maoni