• Utumiaji akili na hikima katika fikra za Imam Kadhim (as)

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Hamjambo wasikiliza wapenzi na karibuni kuwa nasi katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyozaliwa Imam Mussa Al Kadhim (as). Mwenyezi Mungu Mwenye hikima aliwatuma wajumbe wake kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu kuelekea kwenye saada na ufanisi wa dunia na Akhera.

Mitume na wajumbe hao wa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa vielelezo vya rehma na upendo wa Allah kwa waja wake. Watu hao adhimu walibeba bendera ya kuwaongoza wanadamu katika kipindi chote cha historia na kuwalingania watu waliopetea njia ya uongofu kuwaelekeza kwenye nuru na mwanga.

Mtume wa Uislamu Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu pia walibeba bendera hiyo ya kuwaongoza wanadamu katika kipindi cha giza kubwa la dhulma, ujinga na ukandamizaji na walikabiliana na machungu mengi katika njia hiyo. Walikuwa kama nahodha mahiri aliyeongoza jahazi za Umma wa Kiislamu katika bahari yenye mawimbi makali na kulifikisha kwenye pwani ya amani na usalama.

Katika kipindi chetu cha leo kunatupia jicho mmoja wa watu adhimu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) na kujifunza machache katika sira na maisha yake yaliyojaa ibra na mafunzo kuhusu umuhimu wa kutumia akili. karibuni  

 

Imam Mussa al Kadhim (as) alizaliwa tarehe 7 Safar mwaka 128 Hijria katika eneo la al Abwaa nje kidogo ya mji mtakatifu wa Madina. Wakati wa kuzaliwa kwake, baba yake yaani Imam Jaafar Swadiq (as) alisema: Mwenyezi Mungu SW amenitunuku mwanadamu bora.

Baada ya kufariki dunia baba yame, Imam Kadhim (as) alishika hatamu za Uimamu na kuongoza Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 35. Kipindi cha uimamu wake kilijaa misukosuko na mashaka mengi na kiliambatana na kuchanua utawala wa Bani Abbas. Watu kama Haroun Rashid walishika hatamu za uongozi wa Umma wa Kiislamu kwa kutumia hadaa na ujanja na kutenda dhulma kubwa dhidi ya Waislamu sambamba na kupotosha mafundisho sahihi ya dini hiyo. Walijidhihirisha kama wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw), lakini katika vitendo walikwenda kinyume kabisa na Ahlul Bait na kuwaweka katika hali ngumu na mashaka makubwa. Hata hivyo hali hiyo haikumzuia Imam Kadhim (as) kudumisha harakati yake ya kurekebisha fikra za Umma hususan wasomi na kuwaondoa watu katika upotofu wa kifikra na kiitikadi uliokuwa ukienezwa na watawala wa wakati huo. Juhudi za kielimu za Imam (as) ziliulinda Uislamu mbele ya wimbi kali la hujuma ya fikra potofu. Mtukufu huyo alifanya jitihada kubwa kuhakikisha kwamba, itikadi halisi za Uislamu zinalindwa. Alikuwa akiwahumiza Waislamu kuhudhuria vikao vya elimu na wasomi, na anasema katika mojawapo na nasaha zake kwa Waislamu kwamba: "Shirikini kwa wingi katika majlisi za wasomi hata kama mtalazimika kusimama juu ya vidole vya mikono yenu, kwani Mwenyezi Mungu huhuisha nyoyo zilizokufa kwa nuru ya elimu na hikima, kama anavyohuisha ardhi iliyokufa kwa maji ya mvua."

Hapana shaka kuwa akili ni miongoni mwa hiba kubwa za Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu. Mtume Muhammad (saw) anasema: "Kudumu kwa uhai wa mwanadamu kunafungamana na akili yake, na hana dini mtu asiye na akili."

Maana ya hadithi hiyo ya Mtume (saw) ni kuwa akili ina umuhimu mkubwa katika mafundisho ya Kiislamu kwa kadiri kwamba, imetambuliwa kuwa ndio wenzo muhimu wa kutambua misingi na mafundisho ya Uislamu. Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (saw) na Ahlul Bait (as) zinasisitiza kuwa utukufu wa mwandamu na hadhi yake ya kuwa Khalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi kunafungamana na ukamilifu wa akili yake. Uislamu na kitabu kitukufu cha Qur'ani vinasisitiza sana juu ya umuhimu wa kutumia akili na hekima. Aya za Qur'ani Tukufu daima zimetumia neno akili kwa sura ya kitendo na  si kwa sura ya jina ili kusisitiza kwamba, suala muhimu zaidi ni kutumia akili na hikima na si kuwa na akili isiyotumiwa.    

 

Imam Kadhim (as) kama walivyokuwa Maimamu wengine maasumu katika kizazi cha Bwana Mtume (saw), alifanya jitihada kubwa za kubainisha na kuweka wazi nafasi halisi ya akili na hikima katika mtazamo wa Uislamu na kwa sababu hiyo alimtambua mtu asiyetumia akili kuwa hana dini. Daima alikuwa akisema: "Tafuteni maarifa ya dini ya Mwenyezi Mungu, kwani kuelewa sheria za dini ya Mwenyezi Mungu ndio ufunguo wa kufikia daraja za juu za dini na dunia."

Katika maagizo ya Imam Kadhim kunaonekana suala jingine muhimu nalo ni kuwa dini inadhamini saada na ufanisi wa dunia na Akhera kwa sharti kwamba ifahamike na kueleweka vyema na kwa njia sahihi. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana mtukufu huyo alisisitiza sana juu ya umuhimu wa kutumia akili na hikima. Akiweka wazi nafasi na mchango wa akili, Imam Kadhim (as) anasema: Mwenyezi Mungu ana huja mbili, huja ya wazi na dhahiri, na huja ya batini na isiyo wazi. Huja ya wazi ni Mitume, Manabii na Maimamu, na huja ya batini ni akili." Ni kwa kutilia maanani hadithi kama hii ndiyo maana wanazuoni wa fiqhi ya Kiislamu wakaitambua akili kuwa ni mojawapo ya vyanzo vinavyotumiwa katika unyambuzi wa sheria za Kiislamu baada ya Qur'ani na Suna za Mtume (saw). Imam Kadhim (as) alikuwa akisisitiza kuwa dini na mafundisho ya Mwenyezi Mungu haiwezi kueleweka vyema bila ya kuwa na akili timamu na kwa sababu hiyo kutumia akili ipasavyo ni sharti la mtu kuwa na dini na hapana shaka kuwa dini haiwezi kufahamika isipokuwa kwa kutumia akili.

Wapenzi wasikilizaji ni akili na hekima ndiyo inayoweza kupambanua baina ya sahihi na lisilokuwa sahihi na hata kusadikisha au kukadhibisha yanayosemwa na Mitume wa Mwenyezi Mungu. Kutumia akili na hekima kumepewa umuhimu mkubwa sana katika maneno na mafundisho ya Imam Kadhim (as) kwa kadiri kwamba, mtukufu huyo  anafungamanisha saada ya dunia na akhera na utumiaji wa akili. Mtukufu huyo anawausia wanadamu kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya akili akisema: "Mtu anayetaka kujitosheleza bila ya kuwa na utajiri, kuwa na utulivu wa moyo bila ya kuhusudiwa na watu wengine na anayetaka usalama katika dini yake, anapaswa kumwomba Allah akamilishe akili yake."

Wasikilizaji wapenzi utumiaji wa akili, kama ilivyo katika amali nyingine, unahitaji mazoezi na juhudi kubwa. Ili kuweza kutayarisha uwanja mzuri wa kutumia akili na hekima, mwanadamu anapaswa kufanya mambo kadhaa maishani ikiwa ni pamoja na kuketi na maulamaa na wanahekima na busara na kushauriana nao mara kwa mara. Kuhusu suala hilo Imam Kadhim (as) anasema: "Kuketi na watu wenye dini humpa mtu sharafu na heshima ya dunia na Akhera na kushauriana na watu wenye busara na hekima huzidisha baraka, ustawi na taufiki ya Mwenyezi Mungu..." Wakati huo huo Imam Mussa al Kadhim (as) alikuwa akiwamihiza Waislamu kujiepusha kuketi na kusuhubiana na watu majahili na wajinga, akisisitiza kwamba suala hilo linamweka mtu mbali na njia ya haki na ufanisi. Anasema: Jiepushe kuketi na kusuhubiana na wajinga na wakimbie kama unavyokimbia mnyama mkali anayewinda wanadamu."  

Haram tukufu ya Imam Musa al Kadhim AS nchini Iraq

 

Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi chetu unaelekea ukingoni. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Mussa al Kadhim (as) tukimuomba Allah aturuzuku shafaa ya mjukuu huyo wa Mtume wetu Muhamamd (saw). Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. 

Sep 10, 2017 18:24 UTC
Maoni