Waislamu wengi katika pembe mbalimbali za dunia wanakumbana na ubaguzi na aina mbalimbali za ukatili wa kidini, kikaumu na kikabila.

Picha inaooneshwa kuhusu Uislamu katika nchi mbalimbali za dunia pia ni taswira ya dini inayofundisha na kueneza ukatili, utumiaji wa mabavu na misimamo mikali. Wakati huo huo Waislamu huko Ulaya, katika nchi zilizokumbwa na migogoro za Afrika, Marekani na katika baadhi ya nchi za mashariki mwa Asia wanaendelea kuwa wahanga wa makundi yenye misimamo ya kufurutu ada na ya kikatili. Kwa kutilia maanani hali hiyo tunaweza kusema kuwa, Waislamu wa sasa ni wafuasi wa dini inayodhulumiwa zaidi ya Mwenyezi Mungu. 

Katika upande mmoja kutokana na ufahamu potofu na usio sahihi wa makundi kama ya Kiwahabi kuhusu mafundisho ya Uislamu unaotetea uadilifu na kueneza ubinadamu na maadili mema, wafusi wa dini hiyo wamekuwa wakilengwa na kuuawa kwa umati na makundi ya kigaidi na yanayokufurisha Waislamu kama Daesh katika nchi za Iraq, Syria, Somalia, Nigeria, Libya na Lebanon. Vilevile Waislamu wanabughudhiwa, kubaguliwa na hata kuuawa katika nchi nyingi zikiwemo za Ulaya na Marekani kwa sababu tu ya Uislamu wao. Hii ni licha ya kwamba, Waislamu wanaoishi katika nchi zisizo za Kiislamu wanatambuliwa kuwa watu watulivu na wanaoheshimu na kushikamana zaidi na sheria na kanuni za nchi husika kuliko jamii yoyote nyingine. Jamii hizo za Waislamu katika nchi zisizo za Waislamu hufanya jitihada kubwa za kulinda utambulisho wao na kustawisha nchi zao. 

Waislamu wa Myanmar ni moja kati ya jamii zinazodhulumiwa zaidi katika dunia ya sasa. Umoja wa Mataifa pia umethibitisha ukweli huo na kutangaza kwamba, Waislamu wa Rohingya ni moja kati jamii za wachache zinazokabiliwa na dhulma ambayo ni nadra sana kushuhudiwa duniani. Serikali ya Myanmar haiwatambui rasmi Waislamu hao waliowachache nchini humo na inadai ni wahajiri haramu! Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 19 mhajiri wa Kiislamu kutoka Myanmar anasimulia maisha yake ya kusikitisha sana akisema: "Nimezaliwa Myanmar lakini serikali imesema mimi si raia wa nchi hiyo. Nimekulia Banghladesh na hapa pia serikali inasema siwezi kubakia hapai. Mimi kama Mrohingya ninadhani kwamba nimenaswa kati ya nyoka, mijusi kafiri na machura".  

Picha na filamu za mashambulizi na ukatili wa kutisha unaofanyika dhidi ya Waislamu wa Myanmar ni waraka usio na shaka wa mashaka yanayoipa jamii hiyo ya waliowachache nchini Myanmar katika karne hii ya 21.

Serikali ya Myanmar sawa katika kipindi cha utawala wa kijeshi au seikali ya kiraia ya sasa, imekuwa ikishirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mipaka kwa ajili ya kuangamiza kizazi cha Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo. Wakati huo huo Aung San Suu Kyi mwanasiasa mashuhuri zaidi wa Myanmar na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ambaye anatambuliwa kuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika serikali ya sasa ya nchi hiyo, anaendelea kunyamazia kimya muaji, ubaguzi na dhulma zinazofanyika dhidi ya Waislamu hao. Serikali ya Myanmar imekuwa ikizuia hata waandishi habar kuingi katika maeneo ya Waislamu ili kushuhudia na kuripoti kwa karibu yanayojiri katika eneo hilo. Hata hivyo katika siku za hivi karibuni watawala wa nchi hiyo walilemewa na mashinikizo ya walimwengu na kuwaruhusu kwa muda waandishi habari kuingia katika jimbo la Rakhine. Hatua hiyo nadra ilikuwa fursa ya dhahabu ya Waislamu wa eneo hilo kutoa ya moyoni na kueleza maafa na mashaka makubwa wanayokumbana nayo. Wanawake wa Kiislamu wa jamii ya Rohingya walieleza jinsi wanavyobakwa na kunajisiwa, watoto na waume zao kuchukuliwa kusikojulikana kwa madai kuwa ni magaidi na waasi na nyumba na vijiji vyao kuteketezwa kwa moto.

Makazi ya Waislamu yanachomwa moto Myanmar

Ripoti za hivi karibuni zinasema kuwa, Waislamu wa Rohingya karibu laki tatu wamelazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh kutokana na ukatili na mauaji yanayofanywa na Madhudha wa Myanmar wakishirikiana na jeshi la serikali ya nchi hiyo. Baadhi ya wakimbizi hao wamekuwa wakifariki dunia wakiwa njiani kwa kughariki kwenye mito, maradhi, njaa na kadhalika. Shirika la Mpango wa Chkula la Umoja wa Mataifa (WFP) pia limeripoti kuwa, maelfu ya watoto wa Waislamu wa Rohingya huko magharibi mwa Myanmar wanasumbuliwa na utapiamlo na kwamba, wanahitajia misaada ya haraka.

Ripoti zinasema kuwa, jinai na ukatli unaofanywa na Mabudha wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya zinashindana na zile zinazofanywa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh katika nchi kama Iraq na Syria. Mabudha wa Myanmar pia wanawaua Waislamu hao kwa kuwakata vichwa, kuwachoma moto au kuwazika wakiwa hai na kadhalika. Kwa mfano tu mkanda wa video wa siku kadhaa zilizopita unawaonesha Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mipaka wakimtesa mototo mdogo mwenye umri wa miaka mitatu wa Kiislamu kwa kutumia nyaya za umeme. Tukio hili la kinyama limezigusa na kuziumiza nyoyo wa wengi kote duniani.

Inasikitisha kwamba, matukio kama haya ya kikatili na kinyama bado hayajaziamsha wala kutikisa nyoyo za viongozi wa madola ya Kimagharibi. Hata hivyo si ajabu kwa nchi za kiliberali za Magharibi kuchukua msimamo kama huu pale zinapomfanya mtu kama San Suu Kyi kuwa kigezo na mizani ya kupimia haki za binadamu. Katika mfumo wa kiliberali wa Magharibi, haki za binadamu huwa wenzo na chombo kinachotumiwa kupeleka mbele malengo yao ya kisiasa, kiuchumi na kibeberu. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana nchi za Magharibi zilitumia wenzo huo wa haki za binadamu kuishinikiza serikali ya kijeshi ya Myanmar na kumtetea Aung San Suu Kyi aliyekuwa akipambana na serikali hiyo. Itakumbukwa kwamba, San Suu Kyi pia ana uraia wa Uingereza, na Wamagharibi wamekuwa wakimtangaza kuwa ni nembo ya kupigania uhuru dhidi ya utawala wa zamani wa kijeshi wa Myanmar. Kwa sababu hiyo pia walimtunuku Tuzo ya Amani ya Nobel. Kwa sasa nembo hiyo ya kupigania uhuru na haki za binadamu katika mtazamo wa nchi za Maghaibi inanyamazia kimya na hata kuhalalisha ukatili na mauaji ya kimbari yanayoanyika nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya kwa ajili ya kulinda nafasi yake ya kisiasa. Yapata miaka mine iliyopita Jose Manuel Barosso mwenyekiti wa wakati huo wa Umoja wa Ulaya alikutana na San Suu Kyi na kueleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu ukatili unaofanyika nchini Myanmar dhidi ya Waislamu. Wakati huo San Suu Kyi alimjibu kwa kusema kwamba, hawezi kusema lolote kuhusu sula la kuwalinda Waislamu hao. Aung San Suu Kyi aliyasema hayo zikiwa zimepita wiki mbili tu baada ya Waislamu zaidi ya laki moja kufukuzwa katika makazi yao na viji vyote na miji minne ya Waislamu katika jimbo la Rakhine ikateketezwa kwa moto.

Aung San Suu Kyi

Ni kutokana na misimamo kama hii ya San Suu Kyi ndiyo maana watetezi wa haki za binadamu wanahoji vigezo vinavyotumika katika kutoa tuzo mbalimbli za Nobel kama ile liyopewa mwanasiasa huyo anaendelea kuwa shetani bubu mbele ya mauaji ya kimbari yanayofanyika dhidi ya Waislamu nchini Myanmar. Jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu pia zinasisitiza kuwa, Aung San Suu Kyi anapaswa kupokonywa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa sababu amaepoteza sifa na ustahiki.

Alaa kulli hal, tunasisitiza hapa kwamba, yanayofanywa na Mabudha huko Myanmar si tu kwamba ni kinyume na ubinadamu bali pia yanakinzana na mafundisho ya Ubudha wenyewe unaotilia mkazo mwenendo wa kati na kati katika maisha na kujiepusha kutoa roho ya kiumbe au kuchukua kusicho chako. Haya yanaonekana katika mafundisho ya Budha, mwanamfalme wa Kihindi aiyetengana na maisha ya anasa ndani ya kasri la baba yake na akastahamili mashaka na tabu nyingi katika kutafuta njia ya haki na kweli.

Ripoti na picha chache sana za muaji ya kimbari zinazorushwa kutoka Myanmar zinabainisha kuwa, pale misimamo ya kufurutu mipaka inapowakumba wafuasi wa dini au dhehebu lolote huwafanywa wafuasi wa kundi hilo wasahau na hata kukanyaga misingi na mafundisho ya dini au madhehebu hiyo. Uhakika huu unaonekana waziwazi tunapowaona watawala wa Kibudha wakiwa mstari wa mbele kuwahamasisha wafuasi wao kuua, kubaka wanawake na kutesa hata watoto wadogo malaki wa Mwenyezi Mungu…..    

Watawala wa Kibudha wakihamasisha mauaji dhidi ya Waislamu

 

Tags

Sep 20, 2017 07:48 UTC
Maoni