• Qur'ani Tukufu na Imam Hussein AS

Assalam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii maalumu niliyokuandalieni kwa munasaba wa siku hizi 10 za kwanza za Mwezi wa Muharram ambapo Waislamu na wapenda haki kote duniani wanaomboleza kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS. Katika makala yetu ya leo tutaangazia mada ya Qur'ani Tukufu na Imam Hussein AS.

Qur'ani Tukufu ni kitabu chenye kumjenga na kumlea mwanadamu na ni kitabu ambacho kinamuongoza mwanadamu kuelekea katika saada na ukamilifu. Imam Hussein AS si tu kuwa alikuwa mwanafunzi wa chuo cha Qur'ani bali ni muadilifu mwenye kufungamana na Qur'ani Tukufu.

Mfungamno huu usiotenganishika  wa Imam Hussein AS na Qur'ani Tukufu  unabainika katika Hadithi maarufu ya Thaqalayn au Vizito Viwili ambapo Mtume Muhammad SAW katika kauli iliyo bayana kabisa alisema: "Nanawaachieni Vizito Viwili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Watu wa Nyumba Yangu (Ahul Bayt). Viwili hivi katu havitatengana hadi wakati wa kukutana nami katika Hodhi ya Kauthar. Maadamu mtashikamana na Viwili hivi, hamtapotea wala kuterereka."

Katika hadithi hii tukufu ya Thaqalyan tunajifunza kuwa kuna mshikamano na malengo ya pamoja katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahul Bayt. Vizito Viwili hivyo vinamuongoza mwanadamu kuelekea katika hali na njia iliyonyooka na hakuna upotofu au kukengeuka mkondo kwa mwenye kufuata Thaqalayn.

Ni kwa msingi huo ndio katika Qur'ani Tukufu tunasoma hivi katika Suuratul Azzumar aya ya 28: "Qur'ani ya Kiarabu isiyo na upogo, ili wamche Mungu".

Katika wasifu wa Imam Hussein AS pia tunasoma kuwa hata kwa lahadha moja hakuwahi kuondoka katika haki. Kama ambavyo Qur'ani Tukufu inamuongoza mwanadamu kuelekea katika njia ya haki na sahidi ndivyo Imam Hussein AS pia alivyokuwa akiwaongoza wanadamu kuelekea katika imani sahihi na uchaji Mungu.

Tokea mwanzo wa harakati na safari yake ya kutoka Madina kuelekea Karbala alikuwa akitafakari tu kuhusu kuwaongoza wanadamu wala hakuwa akifuata ukubwa au faida za kidunia. Katika kila sehemu, wakati na kwa kila njia iliyowezekana, Imam Hussein AS alikuwa akiwaongoza watu kuelekea katika njia ya haki na saada. Katika lahadha zote za maisha yake hadi wakati alipouawa shahidi katika mapambano yake ya kishujaa dhidi ya watu waovu wa utawala wa Bani Ummaya, alikuwa akitetea haki na kupambana na batili. Qur'ani ni muujiza wa kudumu. Ni kitabu chenye dalili za wazi za muongozo wa kutoka kwa Mwenyezi Mungu SWT kama ambavyo tunasoma katika Qur'ani Tukufu,  tunasoma sehemu ya aya ya 157 ya Suurat An'aam inayosema: "Au mkasema: Lau kuwa tumeteremshiwa sisi Kitabu tungelikuwa waongofu zaidi kuliko wao. Basi imekufikieni bayana kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu, na rehema."

Imam Hussein AS naye alikuwa ni dalili bayana na ya kudumu ya muongozo wa Mwenyezi Mungu SWT. Huu ni muongozo ambao kamwe hautasahaulika au kupotea.

Qur'ani Tukufu imeashiria katika aya kadhaa kuhusu suala la kigezo. Katika Surat Al-Ah'zab aya ya 21 tunasoma: "Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana."

Imam Hussein AS naye pia kama babu yake, Mtume SAW, alikuwa kigezo na ruwaza njema toka mwanzo wa harakati na mwamko wake. Alikuwa kigezo chema kivitendo na kwa maneneo na hivyo akaweka msingi imara wa mwamko wake mkubwa ambao sasa umekuwa kigezo kwa wapenda uhuru kote duniani. Alipokuwa katika njia yake ya kuelekea Karbala, alisema: "Harakati yangu pia ni kigezo na ruwaza njema". Kimsingi ni kuwa, wakati Imam Hussein AS alipokataa kumbai Yazid, alitia dosari kubwa ukhalifa wake na hapo ikabainika wazi kuwa harakati adhimu haingemruhusu Imam Hussein AS kubai utawala mbovu wa Yazid. Kigezo hiki kilichowekwa na Imam Hussein ni cha kila zama na mahala na kinaweka msingi muhimu kwamba wanadamu huru hawapaswi kukubali kutawaliwa na madhalimu.

Mwenyezi Mungu SWA ni Azizi; Qur'ani Tukufu, Mtume wa Mwenyezi Mungu na masahaba zake pia ni azizi: Katika aya ya 21 ya Surat Fussilat tunasoma: "Kwa hakika wanaoyakataa mawaidha haya yanapowajia (wataangamia), na haya bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu (azizi)."

Imam Hussein AS pia likuwa mwanadamu mwenye nguvu na mwanamapambano asiyechoka na wote walisikia kilio chake aliposema: "Naapa Kwa Mwenyezi Mungu, Sitawapa nyingi mkondo wa udhalili na wala sitatoroka kama watumwa" Katika siku ya Ashura pia wakati Ibn Ziyad alipomtaka asalimu amri alisema: "Udhalili uko mbali nasi"

Ibn Abi al Hadid, msomi mkubwa wa Ahul Sunna anasema: "Hussein bin Ali AS ni kiongozi wa wasiokubali madhalimu duniani ambaye alitoa funzo na kuchagua kifo kuliko kuishi katika udhalili. Yeye na wafuasi wake katu hawakukubali udhalilishaji."

Qur'ani Tukufu imesisitiza mara kadhaa kuhusu ulazima wa kuamrisha mema na kukataza mabaya au maovu. Katika sehemu ya  Aya ya 71 ya Suratut Tawba tunasomea kuwa: " Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na husimamisha Sala, na hutoa Zaka, na humt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake."

Imam Hussein AS kama kiongozi wa umma, alitumia umri wake uliojaa baraka katika kuamrisha mema na kukataza maovu. Aliamrisha kwa kuanza na moyo wake, ulimi wake na kisha akatekeleza kivitendo amri hiyo ya Mwenyezi Mungu SWT. Katika kuamrisha mema kivitendo, Imam Hussein AS alifika kilele ambacho mwanadamu anaweza kufika nacho ni kuuawa Shahidi. Si tu kuwa katika hotuba zake alifichua jinai na maovu ya watawala wa Bani Ummaya, bali pia alichukua upanga wa haki na kusimama kupambana kidete hadi kuuawa shahidi. Imam Hussein AS aliitaja harakati yake kuwa ni ya "Kuamrisha mema na kukataza maovu na kuleta marekebisho katika jamii." Katika kauli zake, Imam Hussein AS daima alikuwa akikumbusha kuhusu faradhi hii kubwa ya kuamrisha mema na kukataza mabaya na kusema ndio lengo kuu la harakati hiyo. Ni kwa msingi huo ndio maana Imam Hussein AS baada ya kuhakikisha kuwa harakati yake haina hata chembe ya matamanio ya kidunia kama vile kutaka madaraka alisema: ""Mimi nimetoka kwa ajili ya kufanya marekebisho katika umma wa babu yangu Muhammad SAW na ninataka kuamrisha mema na kukataza maovu, na kufanya kama alivyofanya babu yangu Muhammad SAW na baba yangu Ali bin Abi Talib AS."

Wapenzi wasikilizaji kama ambavyo Qur'ani Tukufu ni muujiza wa kudumu wa Mwenyezi Mungu na ni kitabu ambacho kimeteremshwa kwa ajili ya wanadamu katika zama zote zilizopita, za sasa na za baadaye, Imam Hussein AS pia ni mwenye kudumu kwani si tu kuwa kamwe walimwengu hawatasahau malengo ya mwamko wake bali pia kila siku malengo hayo yanazidi kubainika na kubakia hai. Kwa hivyo tukio la Ashura litabakia hai katika kila zama na wakati. Tunakamilisha makala yetu kwa kunukulu Hadithi ya Mtume Muhammad SAW aliposema:  ''Kwa hakika kifo (shahada) cha (Imam) Husayn AS kitaamsha mori (harara) katika nyoyo za waumini ambao hautapoa milele."

 

 

Tags

Sep 21, 2017 08:10 UTC
Maoni