• Al-Kaaba na Imam Hussein (as)

Kaaba ni jina kongwe, tukufu na linalovutia zaidi la nyumba ya ibada ya Mwenyezi Mungu ambayo inapatikana katika mji mtakatifu wa Makka na katika ardhi ya Hijaz.

Pembeni mwa al Kabaa kuna msikiti mtukufu unaojulikana kwa jin la Masjidul Haram. Kaaba ni Masjidul Haram na maeneo mengine matakatifu ya pembeni kama vile Arafa, Mashár na Mina yote hayo yanapatikana mjini Makka na pambizoni mwake na ndio maana mji huo mtakatifu mara nyingine hujilikana kwa jina la Haran na Baladul Amin. Hii ni sehemu ambayo Waislamu wote wanawajibika kuiheshimu. Imam Hussein (as) aliingia katika mji wa Makaa mwezi wa Shaaban na kukaa hapo hadi mwezi mtukufu wa Dhul Haj ulipofika ambapo alivaa vazi tukufu la Ihram kwa ajili ya kutekeleza ibada tukufu ya Hija. Lakini alipopata habari kwamba askari wa Bani Ummayyia walikuwa wameingia mjini hapo kwa lengo la kutaka kumuua wakiwa wamejificha kwenye vazi tukufu la Ihram, Imam Hussein kwa amri ya Mwenyezi Mungu alibadilisha Hija yake na kuwa Umra na baada ya kutekeleza ibada hiyo tukufu aliondoka na kuiaga Kaaba kabla ya siku ya Arafa. Aliamua kuondoka mjini Makka ili kuepusha kuvinjiwa heshima al-Kaaba Tukufu kwa kumwagwa damu humo. Imam Hussein aliamua kulinda heshima ya Kaaba kwa ajili ya Mwenyezi Mungu naye Mwenyezi Mungu akampa malipo yake kwa kumpa utukufu zaidi kuliko al-Kaaba.

Kaaba Tukufu

Kidhahiri Kaaba ni Nyumba ya Mwenyezi Mungu lakini kwa hakika nyumba ya Mwenyezi Mungu ni nyoyo za waja wake wenye imani.

Kuhusiana na hilo kuna Hadithi Quds inayosema: ''Sio ardhi na mbingu zinaweza kunidiriki bali ni nyoyo za waja ndizo zinaweza kunidiri.'' Hii ni kwa sababu nyoyo za wanaompwekesha Mwenyezi Mungu ni mahala panapoteremkia mapenzi ya Mwenyezi Mungu na ni kituo cha imani, irfani na ikhlasi yake. Kuna riwaya nyingine inayosema kuwa Mwenyezi Mungu alimteremshia Wahyi Mtume wake Dawoud akimwambia: 'Ewe Dawoud! nitayarishie nyumba ili niifanye kuwa maskani yangu.'' (Nabii Dawoud (as)) Akasema: ''Ewe Mwenyezi Mungu! Wewe ni mtukufu na uko juu ya zama na sehemu! Akaambiwa kupitia Wahyi: ''Tayarisha moyo wako na kutenga wakati wako kwa ajili yangu.'' Kwa msingi huo moyo wa mwanadamu ambao una imani, irfan maadili bora kwa hakika ni nyumba ya Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu huwa umesafika na kujitenga na kila aina ya mafungamano na madhihirisho yasiyokuwa ya Kiungu. Na bila shaka moyo wa Imam Hussein ni nyumba halisi ya Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu alisafisha na kuutakasa moyo wake kwa namna ambayo hukuacha humo aina yoyote ya mafungamano yasiyokuwa ya Mwenyezi Mungu. Alifumbia macho mapumziko (starehe) na utulivu, nyumba na familia, watoto na ndugu, jamaa na wafuasi na mambo mengine yote yanayouvutia macho na badala yake kusafisha moyo na kuutayarisha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu, ambapo aliyatoa muhanga mambo hayo yote wakiwemo watoto na jamaa zake kwa ajili ya kumridhisha Mwenyezi Mungu. Aliamua kuwatoa shahidi wapenzi wake hao na kuwacha wengine washikwe mateka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Ni kutokana na kujitolea huko kote kwa njia ya Mwenyezi Mungu ndipo maana halisi ya Aya ya 3 ya Surat Aal Imran inayosema; Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa mwenye kuweza njia ya kuiendea, ikathibiti. Ni kwa kutilia maanani ukweli huo ndipo tunapofamu maneno ya Mtume Mtukufu (saw) aliposema: '' Kila mtu anayemzuru Imam Hussein kwa irfani na ikhlasi huwa ni kana kwamba amemzuru Mwenyezi Mungu kwenye Arshi Yake."

Assalaam Aleika Ya Aba Abdillahi al-Hussein (as)

Nam! Mwenyezi Mungu ameipa Haram ya Imam Hussein (as) utukufu uleule alioipa Haram Yake mjini Makka kutokana na heshima na utukufu ulioonyeshwa na Imam Hussein kwa Haram hiyo. Mwenyezi Mungu ameipa Haram ya Imam Hussein utukufu mkubwa kadiri kwamba inaweza kudhaniwa kuwa Karbala ndio moyo wa Kaaba. Mwenyezi Mungu alimuamuru Mtume wake Ibrahim al-Khalil awaamuru watu waelekea kwenye Kaaba. Anamwambia katika Aya ya 27 ya Surat al-Haj: ''Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.'' Hapo ndipo alipopanda juu ya paa la al-Kaaba na kuwaalika watu kwenye Hija. Ama kuhusiana na Imam Hussein (as) Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume Wake wa Mwisho Muhammad (saw) katika Aya ya 23 ya Surat al- Shura kwa kwa kusema: ''Sikuombeni malipo yoyote kwenu isipokuwa mapenzi katika ndugu.'' Wakati huohuo Mtume Mtukufu huyo alipanda Mimbar mara nyingi na kuwaambia bayana Waislamu kwamba alikuwa ameacha miongoni mwao vitu viwili vyenye uzito na thamani kubwa ambavyo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Quráni Tukufu na Ahlul Beit wake (as). Aliwataka katika nyakati tofauti kupenda na kumsaidia Imam Hussein (as). Miongoni mwa maneno ya Mtume (saw) kumuhusu Imam Hussein (as) ni: "Hussein ni katika mimi na mimi ni katika Hussein, Mwenyezi Mungu ampende kila anayempenda Hussein!''

"Hussein ni katika mimi na mimi ni katika Hussein''

Kaaba inapatikana katika maeneo mengine matakatifu kama vile Swafaa, Marwa, Arafa, Mashár na Mina. Pembeni mwa kaburi tukufu la Imam Hussein (as) huko Karbala nchini Iraq kuna maeneo mengine matukufu. Kwa idadi ya wafuasi wake waliouawa pamoja naye katika ardhi hiyo tukufu, Imam Hussein (as) mara 72 aliwatoa wafuasi hao mmoja baada ya mwingine, kwenye mahema na kuwapeleka katika medani ya vita kupigana na maadui wa Uislamu. Alifanya hivyo taratibu au mara nyingine kutembea kwa kasi kama wanavyofanya Mahujaji ''sa'i'' baina ya vijilima viwili vya Swafaa na Marwa mjini Makka. Baada ya kuwatoa wahanga wafausi na wapendwa wake wote kwenye medani ya vita na kubaki peke yake, Imam Hussein (as) aliingia kishujaa kwenye medani hiyo, huku akiwa ananong'ona maneno yafuatayo: Labbeik Allahuma Labbeik!....Ewe Mwenyezi Mungu! Ninaharakisha kuja kwako. Kwako ambapo Wewe ni mmoja tu bila ya kuwa na mwenza. Peke yangu peke yangu! Niko kwenye njia yako na ninakuja kwako. Nimeutenganisha moyo wangu na mahusiano na mafungamano yote na kuufungamanisha na mapenzi yako tu. Hivi sasa sisikitishwi kwa kuwa mpweke wala kutokuwa na wa kunisaidia na sisikitishwi pia na upweke wangu mbele ya maadui. Sio kufa shahidi kwa wana wangu kunanifanya niishiwe nguvu wala matatizo ya jamaa zangu. Sio kupotea nguvu za macho yangu kutokana na kiu wala wingi wa maadui."

Hatimaye Imam Hussein (as), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw) aliachwa pekee yake na kuuawa kinyama kwenye madani ya vita na watu waovu na maadui wa Uislamu ambao hawakuwa na chembe yoyote ya huruma wala utu.

Sep 24, 2017 12:29 UTC
Maoni