• Kulia Katika Maombolezo ya Imam Hussein (AS): Unyenyekevu wa Moyo na Mapenzi ya Nafsi

Assalamu alaykum wapenzi wasikilizaji, warahmatullahi wabarakatuh. Kwa kuwadia mwezi wa Muharram, kwa mara nyengine nyoyo za waliokomboka kifikra duniani zinajielekeza kwa Imam Hussein (as) huku macho yao yakibubujikwa na machozi kwa kulikumbuka tukio la Karbala. Ni miaka 1372 imepita tangu lilipojiri tukio hilo, lakini unapowadia mwezi wa Muharram kila mwaka, Waislamu huendelea kujumuika pamoja na kushiriki kwenye majlisi za kumuomboleza Hussein Ibn Ali (as) na wafuasi wake.

Maombolezo ni hafla inayofanyika kwa madhumuni ya kumliwaza mtu au watu waliofikwa na msiba. Lakini katika maombolezo ya Imam Hussein (as) ilivyo hasa ni kwamba washiriki wa hadhara ya maombolezo, wao wenyewe wanajihesabu kuwa ndio waliofikwa na msiba wa tukio kubwa la Ashura; kwa hivyo kimsingi huwa wanaliwazana kwa kushiriki kwenye maombolezo hayo. Bila shaka kuweka hadhara za maombolezo ya Imam Hussein (as), mbali na kuwa na lengo la kuwaliwaza waombolezaji huwa ni fursa pia ya kuhuisha na kudumisha hamasa adhimu ya Ashura. Na hasa kwa kuzingatia kwamba kumuomboleza Imam Hussein (as) kupitia hafla inayokutanisha Waislamu wa hali na matabaka yote, wake kwa waume, wazee kwa vijana wakiwemo hata chipukizi na watoto wadogo, huzijaza nyoyo za waombolezaji maarifa ya kina ya ujumbe na mafunzo yaliyomo kwenye hamasa ya mtukufu huyo.

Ijapokuwa katika maombolezo ya Imam Hussein (as) washiriki huwa wanalia na kuhuzunika lakini kufanya hivyo huwa na taathira nzuri kwao kiroho na kimaanawi. Kinachoonekana kidhahiri ni ghamu katika nyuso zao, lakini majonzi yaliyomo kwenye batini za waombolezaji hao ni tofauti kabisa na majonzi na huzuni wanazokuwa nazo katika maisha ya kila siku. Ghamu na huzuni hizo ni chemchemu na cheche ya harakati. Si huzuni za kusababisha msongo wa mawazo, ni huzuni zinazompa mtu utulivu na nishati maalumu ya ndani ya nafsi. Ndio maana watu waliowahi kushiriki kwenye hadhara za maombolezo ya Imam Hussein (as) huwa katu hawachoshwi wala hawapungukiwi na hamu ya kushiriki tena na tena katika hadhara hizo; na hilo ni dhihirisho la ukweli wa maneno ya Bwana Mtume SAW aliposema: " إن لِقتلِ الحسین حرارةٌ فی قلوب المؤمنین لاتَبرَد ابداً " “Hakika kuuliwa (shahidi) Hussein kunazitia joto nyoyo za waumini ambalo halipozeki wala halizimiki abadani".

Shauku, huba na hisia za moyoni ni mambo muhimu zaidi yanayotoa msukumo wa kufanya hadhara za maombolezo ya Imam Hussein (as), lakini maombolezo hayo hayaishii kwenye nukta hizo tu bali yana chimbuko la mantiki na maarifa ya dini pia. Na ndiyo maana hadhara hizo za maombolezo huwa ni fursa pia ya kuwaelimisha watu kuhusu shakhsia na harakati ya Imam Hussein (as) pamoja na mafundisho ya dini aliyoyatolea mhanga roho yake. Katika hadhara hizo, makhatibu weledi na watoaji mawaidha waelewa hubainisha hukumu za masuala ya kisheria, ya kiakhlaqi na kiitikadi na kuwaelimisha waombolezaji kuhusu mafundisho mbalimbali ya dini. Kwa sababu hiyo hafla za maombolezo ya Imam Hussein (as) katika kipindi chote cha historia zimekuwa fursa ya kuhuisha dini na kueneza mafundisho ya Uislamu, kama ambavyo katika mwaka 61 hijria, Imam Hussein mwenyewe alipambana kwa lengo la kuhuisha dini hiyo tukufu. Katika hafla ya maombolezo ya Imam Hussein (as) na wafuasi wake waaminifu waombolezaji hupata fursa pia ya kuelewa shakhsia na adhama yao ya kiroho. Hao walikuwa waja waliokamilika kwa kupambika kwa sifa bora za subira, uaminifu, istiqama, ushujaa na kujitolea mhanga; na kila mmoja wao alikuwa kigezo na ruwaza ya mambo mema. Lakini mbali na hayo waombolezaji huweza pia kuwatambua maadui wa Imam Hussein (as), yaani Yazid na washirika wa Yazid na kujengeka ndani ya nafsi zao chuki na ghadhabu dhidi yao na kwa matendo yao maovu. Kwa msingi huo, katika maombolezo ya Imam Hussein (as) zinapatikana tija mbili za "Tawalli" na "Tabarri". Tawalli maana yake ni kupenda; na maana ya Tabarri ni kujibari na kuchukia, ambayo yote mawili ni miongoni mwa misingi midogo ya dini ya Uislamu. Kila Muislamu ana wajibu wa kuwapenda watu wa haki na kuwachukia watu wa batili. Na ndiyo maana washiriki wa hadhara ya maombolezo ya Imam Hussein (as) humtamkia Imam huyo na viongozi wao wengine kwamba:

" انّی سِلمٌ لِمن سالَمَکُم و حربٌ لِمن حارَبکم و وَلیٌ لِمن والاکم و عدوٌّ لِمن عاداکم ". Yaani mimi ni mpaji amani kwa wanaokupeni amani nyinyi, na mpiga vita wa wanaokupigeni vita nyinyi, na mpenzi wa wanaokupendeni nyinyi, na adui wa wanaokufanyieni uadui nyinyi". 

Hadhara ya mawaidha na maombolezo katika Hussainiyyah ya Imam Khomeini (MA)

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema katika aya ya 16 ya Suratul-Hadid ya kwamba: "" اَلَمْ یَأْنِ لِلَّذِینَ آمَنُوا أَنْ تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِکْرِ اللّهِ وَ ما نَزَلَ مِنَ الْحَقِّ ... yaani Je! Wakati haujafika bado kwa walio amini zikanyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na haki iliyo teremka? Wapenzi wa Imam Hussein (as) pia unapowadia mwezi wa Muharram nyoyo zao hunyenyekea kwa kumkumbuka na kumlilia kiongozi huyo mkubwa wa Tauhidi. Sababu ni kwamba machozi hayo na maombolezo hayo kwa ajili ya Hussein ni alama ya imani juu ya Allah na unyenyekevu wa nyoyo kwake Yeye Mola. Ni kama alivyosema Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba: "Kumpenda Hussein ni kumpenda Mwenyezi Mungu na kumfanyia uadui yeye ni kumfanyia uadui Mwenyezi Mungu". Machozi yanayomwagwa kwa ajili ya Hussein (as) ni machozi yanayotokana na imani juu ya ukamilifu wa kiutu na jitihada za kuufikia ukamilifu huo.

Kimsingi, siku zote msiba wa kuondokewa na waja wateule na watukufu huwa mkubwa na mzito, kiasi cha kuwafanya watu wengi wawe na masikitiko na kuwaomboleza waja hao. Lakini uchungu wa msiba huo huwa mkubwa zaidi pale waja hao wanapouliwa kidhulma. Kwa sababu hiyo kilio kilichoendelea kwa muda mrefu cha manusura mkuu wa Ashura, yaani Imam Sajjad (as) ambaye alishuhudia kwa karibu msiba na masaibu ya Karbala na kuuliwa shahidi kidhulma baba yake, ndugu zake, ami zake na wapendwa wake wengine, hakikuwa cha kuhuzunika kwa uchungu wa kuondokewa na wapendwa wake tu, bali pia cha kusikitikia dhulma waliyotendewa na kuondoka duniani waja waliokuwa wamefikia kilele cha utukufu, ukamilifu na utakasifu.

Dhulma aliyofanyiwa Imam Hussein (as), mjukuu kipenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW na mmoja wa mabwana wawili wa vijana wa peponi katika siku ya Ashura pamoja na mashahidi wengine wa Karbala, ilikuwa kubwa kwa kadiri ya kuwafanya hata watu wengine wengi wasio Waislamu washiriki kwenye maombolezo ya mtukufu huyo. Ashiki na mapenzi makubwa waliyonayo baadhi ya waombolezaji kwa Imam Hussein (as) na wafuasi wake yameziathiri nyoyo zao kiasi kwamba baadhi ya wakati yanapotajwa majina yao tu hububujikwa na machozi.

Machozi yanayowatoka waombolezaji wa Hussein (as) ni dhihirisho la huruma na mahaba waliyonayo juu yake ndani ya nafsi zao. Ni mahaba na mapenzi ambayo Mwenyezi Mungu ameyajaza katika nyoyo zao.

Mwanamke asiye Muislamu raia wa Sweden akilia katika kampeni ya "Hussein ni nani?"

Bila ya shaka machozi hayo yana athari na taathira nyengine kadhaa. Kwa upande wa watu binafsi, kwa upande mmoja, kulia kunawapa waombolezaji wenyewe utulivu wa kimaanawi na kwa upande mwengine kuhudhuria kwao kwenye hadhara za maombolezo ya Imam Hussein kunazidisha mahaba na utambuzi wao juu ya mtukufu huyo na vilevile kunawafanya wawe na idili na hima zaidi ya kuhakikisha tabia na mienendo yao inafanana na ya mashahidi watukufu wa Karbala wanaowalilia.

Kumlilia Imam Hussein (as) kuna athari muhimu sana pia za kisiasa na kijamii. Kwa sababu mbali na kuwa na msisimko na hisia za upendo zinazojengeka ndani ya nafsi ya mtu, kulia huko kunafanyika pia kwa hali kamili ya uelewa ili kumkumbuka shakhsia mkubwa aliyejitolea mhanga kila alichokuwa nacho kwa ajili ya kuhuisha dini na kutekeleza uadilifu. Katika harakati yake hiyo kubwa isiyo na kifani, Imam Hussein (as) alimtoa mhanga hata mwanawe mchanga aliyekuwa angali ananyonya. Kwa hivyo kwa kumlilia Imam Husssein (as) nafsi ya muombolezaji huwa inajifungamanisha na shakhsia mkubwa na mtukufu na kuyafanya malengo matukufu aliyopigania yakite ndani ya moyo wake.

Maombolezo ya Imam Hussein (as) 

Kwa msingi huo, kulia katika utamaduni na mafundisho ya Ashura ni chachu ya kuhuisha na kudumisha kumbukumbu ya mapambano ya Imam Hussein (as) na kuufikisha ujumbe wa Bwana huyo wa mashahidi kwa jamii nyengine zote za wanadamu. Kulia ni silaha isiyoisha makali yake, ya kupaza sauti ya upinzani dhidi ya madhalimu na kulinda damu ya mashahidi. Imam Khomeini (MA) ameitolea ufafanuzi mzuri nukta hiyo aliposema: “Kulia katika maombolezo ya Imam Hussein (Alayhi-Salam) ni kuhuisha harakati; na maana ya uhuishaji huo ni kwamba kundi la watu wachache lilisimama kukabiliana na utawala mkubwa… wao (mabeberu) wanavihofu vilio hivi, kwa sababu vilio hivi ni mayowe ya mdhulumiwa, ni mayowe yanayotolewa dhidi ya dhalimu.” Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

 

 

Oct 02, 2017 02:30 UTC
Maoni