• Utumwa Mamboleo, Jinai ya Kimyakimya

Mwaka 1949 Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe Pili Disemba ya kila mwaka kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kufuta Utumwa.

Licha ya kwamba imepita zaidi ya miaka 200 sasa tangu utumwa ufutwe rasmi na licha ya maazimio mengi yaliyotolewa kote duniani ya kufuta na kupiga vita utumwa, lakini inasikitisha kusema kuwa, hadi sasa utumwa ungalipo katika maeneo mbalimbali ya dunia ya sasa. Utumwa umekuwa jinai ya kimyakimya inayoendelea kufanyika katika nchi nyingi. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndipo jamii ya kimataifa ikatangaza Siku ya Kimataifa ya Kufuta Utumwa ili kuhimiza zaidi mapambano dhidi ya janga hilo. Mwaka huu kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, walimwengu waliadhimisha siku hiyo Jumamosi iliyopita yaani tarehe Pili Disemba. 

Ripoti ya tatu ya kigezo cha kimataifa cha Utumwa Mamboleo iliyotolewa mwaka jana wa 2016 ilikiri kwamba, watu milioni 45 wanaishi utumwani. Ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) pia inasema, biashara ya utumwa inawaingizia wahusika faida ya dola bilioni 150 kila mwaka na kwamba ndiyo yenye pato kubwa zaidi baada ya biashara ya dawa za kulevya na silaha. Inasema asilimia 70 ya watumwa hao wanafanyishwa kazi za kulazimishwa na kwamba asilimia 33 miongoni mwao ni watoto. Nusu ya watumwa mamboleo ni wanawake na wasichana. Vilevile ripoti ya ILO na Walk Free Foundation imesema kuwa, karibu watu milioni 5 kote duniani walikuwa watumwa wa ngono katika mwaka uliopita wa 2016.

Nukta ya kuashiria hapa ni kuwa, aina hii ya utumwa mamboleo haishuhudiwa katika nchi zinazoendelea tu bali hata katika nchi zilizoendelea. Kamishna wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya, Anna Cecilia Malmström siku chache zilizopita aliashiria tatizo la utumwa barani humo na kusema: Ni vigumu kuamini ukweli huo lakini ni kweli kwamba kuna makumi ya maelfu ya watumwa katika nchi za Ulaya ambao wanauzwa na kununuliwa kama bidhaa. Huu ni ukweli mchungu kuona biashara ya binadamu ikifanyika kandokando yetu na kuwa karibu yetu kiasi hiki" mwisho wa kunukuu.

Kufanya kazi za kulazimishwa ni miongoni mwa sura muhimu za utumwa mamboleo. Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) linasema kwa sasa wahanga milioni 21 wanafanyishwa kazi za kulazimishwa kote duniani. Maeneo yenye idadi kubwa zaidi ya watu wa aina hii ni Kusini mashariki mwa Asia na Afrika. Katika maeneo hayo watumwa hao hufungiwa katika vizimba na tundu kama za ndege na wanyama ili kuwazuia wasitoroke. Ripoti zimasema maelfu ya watumwa wanafanyishwa kazi za kulazimishwa katika majahazi na meli za uvuvi katika maeneo ya kusini mashariki mwa Asia hususan Myanmar na nchi nyingine kadhaa za eneo hilo na wanaporudi bara hufungiwa tena katika vizimba na tundu hizo. Hali hiyo pia inashuhudiwa katika nchi kama Indonesia ambapo watumwa hao mamboleo hutumika kuvua samaki wanaouzwa katika masoko ya kimataifa hususan huko Marekani. Watumwa hawa wanaishi katika vizimba na tundu ambazo huwa vigumu sana kwao kuweza kunyoosha migumu ndani yake. Chakuka chao huwa kiasi kidogo cha wali na nafaka, na baada ya kula na kupumzika kidogo hupandishwa tena melini na kwenye majahazi na kupelekwa baharini kwenda kufanya kazi za kulazimishwa.

Watumwa wanaofungwa katika vizimba na tundu kama za wanyama hupelekwa Marekani

Inasikitisha kwamba watoto wadogo wana nafasi makhsusi katika biashara hiyo yenye faifa kubwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, watoto ni wafanyakazi wa bei rahisi sana bali hata wanafanyishwa kazi bure na mara nyingi hufanywa watumwa wa ngono katika madanguro, na kwa sababu hiyo wanatafutwa sana. Ripoti ya Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) inasema: Kila mwaka watoto milioni moja na laki mbili hutekwa na magenge ya wafanya biashara ya binadamu kote duniani na kuingizwa katika utumwa. UNICEF inasema kuwa, watoto hao hufanyishwa kazi za kulazimishwa katika maeneo ya vita, au huuzwa mkabala wa chakula, dawa na bidhaa nyingine au kutumikishwa katika kazi haramu kama za madanguroni. Ripoti hiyo ya UNICEF inasema aghlabu ya watoto hao wanachukuliwa katika nchi za magharibi na katikati mwa Afrika kama Togo, Mali, Burkina Faso na Ghana. Inasisitiza kuwa idadi kubwa zaidi ya watoto wanaofanyishwa kazi za majumbani kama watumwa ni wasichana.   

Aina nyingine ya sura za utumwa mamboleo ni utumwa wa ngono. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania huko Marekani, Kathleen Barry ameandika katika kitabu chake maarufu alichokipa jina la The Prostitution of Sexuality kwamba: Katika nchi maskini zenye uchumi unaoyumbayumba, wanawake wengi hutumbukizwa katika utumwa wa ngono kwa kadiri kwamba, kuanzia muongo wa 70 hadi sasa mamilioni ya wanawake kote duniani wameuzwa na kununuliwa kwa ajili ya kazi ya ukahaba. Anasema: "Aghlabu ya wanawake hao ni raia wa nchi za kisini mashariki mwa Asia, Ulaya mashariki, America ya Kusini na Afrika zenye uchumi duni na unaostawi."

Huenda usiamini, mpenzi msikilizaji, kusikia kwamba, katika karne hii ya 21 madalali wanawanadi wanawake makahaba hadharani katika baadhi ya nchi na hata kuwauza katika mnada wa kila mwezi! Baadhi ya nyakati wanawake na wasichana walionunuliwa kwa njia za magendo ya binadamu huuzwa kwa madalali kadhaa. Baadhi ya wanawake na wasichana hao huaga dunia kutokana na kupigwa au huchwa hivi hivi katika nchi walikopelekwa, na pale wanapokataa kuuza miili yao na kuasi amri za wamiliki wao, madalali hutoa vitisho vya kuua watu wa familia zao na kwa njia hiyo hulazimika kusalimu amri na kuanza kujiuza kwa faida ya wamiliki na mabwana zao au huuzwa katika mabaa, vilabu vya usiku na majumba ya anasa. Afisa mmoja wa Wizara ya Sheria ya Sweden ameeleza masikitiko yake kuhusu mwenendo huo na kusema: Inasikitisha kwamba tunawafunza watoto mashuleni mwetu kuhusu aina mbalimbali za utumwa katika karne zilizopita lakini nakala mpya ya utumwa huo ingalipo hadi hivi sasa."  

Utumwa mamboleo, matokeo ya ustaarabu wa dunia ya sasa

Uchunguzi uliofanyika umebaini kuwa, mara nyingi watumwa hao mamboleo wanapelekwa katika nchi za Magharibi na Marekani na kwamba mgogoro mkubwa zaidi wa haki za binadamu katika dunia ya sasa unashuhudiwa zaidi katika nchi hizo. Uchunguzi wa taasisi rasmi nchini Marekani unaonesha kuwa, kila mwaka zaidi ya wasichana laki moja wenye umri wa chini ya sheria wanafanyishwa biashara ya utumwa wa ngono nchini humo. Takwimu za Umoja wa Mataifa pia zimethibitisha kwamba, nusu ya wahanga milioni 3 wa biashara ya binadamu inayofanyika kila mwaka hupelekwa nchini Marekani na kwamba karibu asilimia 50 ya pato la mabilioni yanayotokana na biashara hiyo chafu huingia kwenye mifuko ya Wamarekani.

Nchi za Ulaya pia ni soko kubwa la biashara ya utumwa mamboleo hususan utumwa wa ngono. Nchi muhimu zaidi wanakotolewa watumwa hao ni zile za Ulaya mashariki kama Moldova, Albania, Romania, Ukraine na Bulgaria, Afrika kama Morocco, Algeria, Nigeria, Sudan na Sierra Leone, nchi za Asia kama China, Sri Lanka, Pakistan and Afghanistan na nchi za America ya Kusini kama Brazil, Jamhuri ya Dominican na Ecuador.

Uchunguzi unaonesha kuwa nchini Ujerumani pekee wanawake na wasichana elfu kumi kutoka nchi za Czech, Poland na Bulgaria wanatumikishwa kwa lazima katika vilabu vya anasa. Wataalamu wanasema faida kubwa ya biashara hiyo chafu inashajiisha zaidi biashara na utuwma wa aina hiyo.

Nukta ya kutiliwa maanani ni kuwa, kutokana na upuuzaji wa viongozi wa nchi za Ulaya, bei ya mtumwa mmoja katika eneo hilo la dunia ni sawa na bei ya gari kuukuu au bei ya simu ya mkononi (rukono) na wasichana wanauzwa kwa bei ya baina ya Euro 800 na 3000. Mbali na hayo kila mwaka watoto wapatao milioni moja, wasichana na wavulana, hutoweka katika umoja wa Ulaya ama kwa kutoroka, kutekwa nyara au kupotea. Wengi kati ya wahanga hao ni wasichana wanaofanywa watumwa wa ngono, ombaomba barabarani na baadhi yao hufanyishwa kazi katika mashamba na majumbani au kulazimishwa kuuza baadhi ya viungo vya miili yao.

Watoto wanatumiwa kama watumwa wa ngono

Kupanuka zaidi tatizo hilo la kimataifa kumeulazimisha Umoja wa Mataifa kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana nalo. Hata hivyo inasikitiasha kuwa, bado kuna watu wanaoendelea kuwadhulumu wanadamu wenzao kwa ajili ya maslahi yao binafsi. Hivyo basi ili kuweza kung'oa kabisa mzizi wa maafa hayo makubwa kuna ulazima wa kulindwa haki za kiraia na uhuru wa mtu binafsi, na madola makubwa yanapaswa kuchukua hatua za maana na kivitendo na kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Kutengwa siku makhsusi kwa jina na Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Utumwa mamboleo kwa hakika ni fursa nzuri zaidi ya kukumbusha majukumu hayo muhimuu.        

Dec 05, 2017 11:21 UTC
Maoni