• Quds, Kituo cha Dini za Mwenyezi Mungu -1

Miaka mia moja baada ya kutolewa Azimio la Balfour (Balfour Declaration) la waziri wa wakati huo wa mambo ya nje wa Uingereza akiafiki kuundwa dola la Kiyahudi katika ardhi ya Palestina, Donald Trump, Rais wa sasa wa Marekani ameitangaza Quds tukufu (Jerusalem) na Baitul Muqaddas, Kibla cha Kwanza cha Waislamu wote, kuwa ni mji mkuu wa utawala huo bandia wa Israel.

Suala la kuufanya mji huo mtakatifu kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel lilikuwa ajenda kuu ya Wazayuni wavamizi tangu mwanzoni mwa kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina. Hata hivyo kwa kutilia maanani utukufu wa mji huo na kuwepo Msikiti mtakatifu wa al Aqsa katika eneo hilo na vilevile umuhimu wake kwa Waislamu wote duniani, Wazayuni wa Israel hawakuweza kupata uungaji mkono wa kimataifa hususan kutoka wa waitifaki wao wa Magharibi wa kuufanya mji wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu. Mwaka 1995 Kongresi ya Marekani ilipasisha muswaada katika uwanja huo kutokana na ushawishi mkubwa wa makundi ya mashinikizo ya Kizayuni. Hata hivyo marais wote waliotangulia wa Marekani sawa wawe wa chama cha Democratic au wale wa Republican walijizuia kutekeleza muswaada huo wa Kongresi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Hatima ya mji wa Quds ilizua changamoto na mvutano mkubwa katika mazungumzo yote ya amani kati ya Wapalestina na utawala ghasibu wa Israel kiasi kwamba, mjadala huo uliondolewa katika orodha ya masuala yaliyokuwa yakijadiliwa katika mchakato wa mapatano ya pande hizo mbili chini ya usimamizi na upatanishi wa Marekani! Hata hivyo mazungumzo hayo yaliyojiepusha kadhia ya Quds yaligonga mwamba na kubakia angani bila ya kufikia matunda yoyote. Kwa kutilia maanani hayo yote inaonekana kuwa, hatua ya Donald Trump ya kuutambua mji mtakatifu wa Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel imechukuliwa baada ya kushindwa njama na mipango yote ya Washington na waitifaki wake katika eneo la Mashariki ya Kati na kufeli njama zao huko Syria na Iraq kwa ajili ya kufuta harakati za mapambano. 

Uamuzi wa Trump wa kuitambua Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel umepingwa na walimwengu wote

Marekani na wenzake walianzisha na kufadhili makundi ya kitakfiri na kiwahabi kama Daesh kwa shabaha ya kuzigawa nchi za Iraq na Syria na kuimarisha zaidi utawala ghasibu wa Israel. Hata hivyo harakati za mapambano na kusimama kishujaa majeshi na makundi ya kujitolea ya Syria na Iraq yakisaidiwa na washirika wao kutoka Iran, Hizbullah na Russia kulivuruga mahesabu yao kwa maslahi ya kambi ya mapambano. Hivi sasa faili la Daesh limefungwa katika nchi za Syria na Iraq. Vilevile jitihada zote zilizofanywa na nchi zinazoyafadhili makundi ya kitakfiri na kigaidi zikiongozwa na Saudi Arabia kwa ajili ya kufungua medani mpya ya vita huko Lebaon dhidi ya harakati ya Hizbullah na harakati za mapambano, zimegonga mwamba na kuangukia pua.

Ni katika mazingira hayo ndipo Rais Donald Trump wa Marekani akatoa tangazo la kuitambua rasmi Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Kwa hatua hiyo, Trump amefanya jitihada za kutaka kutimiza matakwa ya Wazayuni baada ya kushindwa mtawalia katika miaka ya hivi karibuni mkabala wa harakati na kambi ya mapambano. Pamoja na hayo upinzani mkubwa wa jamii ya kimataifa dhidi ya uamuzi huo wa Trump umeonesha kuwa, Wazayuni na Marekani wametengwa. Kwa sababu, ghairi ya utawala unaoua watoto na wa kigaidi wa Israel hakuna nchi yoyote iliyotambua Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel. Vilevile waitifaki wakubwa wa Marekani na utawala ghasibu wa Israel barani Ulaya wote wameonesha msimamo hasi dhidi ya uamuzi wa Trump kuhusu Quds tukufu na kuutaja kuwa utapelekea kushindwa mchakato wa mapatano ya Mashariki ya Kati. Hapa inatupasa kusisitiza kuwa mchakato huo ulikufa muda mrefu uliopita na hatua ya Trump imepigilia msumari mwingine katika jeneza lake. Pamoja na hayo yote inabidi tusema kuwa, hatua hiyo ya Rais wa Marekani ya kuutambua mji wa Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel haitabadili ukweli wa historia na nafasi ya mji huo kati ya Wapalestina na Waislamu kote duniani. 

Quds tukufu

Tunapotazama historia ya Baitul Muqaddas tunaona kuwa, mji huo na maeneo yake matakatifu ipo siku yatakombolewa kutoka kwenye makucha ya Wazayuni na waungaji mkono wao licha ya majeraha yote yaliyousibu. Quds na Baitul Muqaddas ni kituo kikuu na kitovu cha dini tatu za Mwenyezi Mungu yaani Uislamu, Ukristo na Uyahudi na ina nafasi makhsusi baina ya wafuasi wa dini hizo. Mji huo wa kihistoria una historia ya maelfu kadhaa ya miaka na umeendelea kusimama kidete mithili na miamba inayouzunguka. Jina la mji wa Baitul Muqaddas siku zote linaandamana na Quds, utukufu na utakatifu na tangu zamani mji huo wa kale ulikuwa ukijulikana kama mji wa amani na usalama. Mji huo ulikuwa eneo la Mitume na Manabii wa Mwenyezi Mungu na majengo ya kale yaliyobakia hadi hii leo ya mji huo ni kielelezo cha historia na utambulisho wake. Makanisa ya kihistoria yaliyobakia hadi hii leo ya mji huo kama Kanisa la Ufufuo (Church of the Resurrection), misikiti ya kale hususan Msikiti wa al Aqsa ni nyaraka za historia na utambulisho wa mji wa Quds. Mji huo wa Quds pia ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu. Waislamu walikuwa wakiswali kuelekea Baitul Muqaddas hadi mwaka mmoja baada ya Hijra na kuhama kwa Mtume Muhammad (saw) kutoka Makka na kwenda Madina kwa amri yake Mwenyezi Mungu.

Quds ina umuhimu mwingine mkubwa kwa Waislamu nao ni kuwa, ulikuwa ngazi na Miiraji ya Bwana Mtume (saw) kuelekea mbinguni. Safari hiyo ilianzia kandokando ya Ukuta wa Buraq ulioko karibu na Msikiti wa kihistoria wa al Aqsa ambao Wayahudi wanauita "Ukuta wa Kulia" (Wailing Wall, au Western Wall). Miiraji ni miongoni mwa miujiza ya Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw). Miiraji ndiyo safari takatifu kuliko zote katika historia ya mwanadamu na msafiri wake alikuwa Muhammad (saw), uwanja uliotumiwa kupaa katika safari hiyo ulikuwa Msikiti mtukufu wa Makkah, mapitio yake yalikuwa Msikiti wa al Aqsa na mwenyeji wa msafiri huyo mtukufu alikuwa Mwenyezi Mungu Jalla Jalaluh. Lengo la safari hiyo lilikuwa kuonyeshwa adhama, ishara na alama za utukufu wa Mola Muumba, na zawadi alizopewa msafiri huyo ni habari za mbinguni na ulimwengu wa malakuti na kuinua juu kiwango cha ufahamu wa mwanadamu kuhusu dunia hii ya kimaada.

Jina la Msikiti wa al Aqsa na Miiraji ya Mtume (saw) vimetajwa katika aya ya kwanza ya Suratul Israa ya Qur'ani tukufu. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya hiyo kwamba: Ametakasika aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.

Msikiti wa al Aqsa

Kwa mujibu wa hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu, mwaka mmoja kabla ya Hijra na kuhama kwa Mtume kutoka Madina, Mtume Muhammad (saw) alisafirishwa kwa Buraqi baada ya kuswali Swala ya Magharibi katika Msikiti wa Makka na kupelekwa mbinguni kupitia Baitul Muqaddas. Aliporudi aliswali Swalatu Subh katika Msikiti wa Makka. Safari hiyo ya Miiraji ilifanyika akiwa macho na kwa mwili wake Mtume Mtukufu na si usingizini au safari ya roho tu kama wanavyodai baadhi ya watu. Asili ya kufanyika safari hii ni miongoni mwa masuala yasiyo na shaka ndani yake katika Uislamu na madhehebu zote zimeafikiana kuhusu asili ya tukio hilo. Nukta ya kutiliwa maanani hapa ni kuwa, Mwenyezi Mungu SW alimshusha Nabii Adamu duniani kutoka mbinguni, kinyume chake, alimpeleka Nabii Muhammad kutoka ardhini na dunia hii kuelekea mbinguni. Katika usiku huo, Mtume Muhammad (saw) aliona ulimwengu wa juu na aali, malakuti za ulimwengu usio wa maada na maajabu ya maumbile ya Allah SW. Vilevile alikutana na Manabii na Mitume waliomtangulia. Katika safari hiyo pia Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu alioneshwa pepo na moto wa Jahannam, hali ya watu wa peponi na neema zake, na hali ya watu wa Jahannm na adhabu na mashaka yao.

Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa, Msikiti wa al Aqsa unashika nafasi ya tatu kwa utukufu zaidi baina ya Waislamu baada ya Masjidul Haram huko Makka na Msikiti wa Mtume mjini Madina. Msikiti huo ulijengwa na Nabii Daud (as) na kukamilishwa na mwanaye, Nabii Sulaiman. Tangu wakati huo msikiti huo ulijengwa upya mara kadhaa katika vipindi mbalimbali vya historia ikiwa ni pamoja na kujengwa upya katika kipindi cha utawala wa Abdul Malik bin Marwan, mtawala wa kizazi cha banii Umayyah. Msikiti huo uliharibiwa na zilzala kubwa iliyotokea mwaka 585 Miladia na ukakarabatiwa na Swalahuddin Ayyubi mwaka 583 Hijria. Sehemu nyingine ya msikiti huo mtukufu ilijengwa katika karne ya 9 Hijria. Wakati wa Vita vya Msalaba, Wakristo walisimama katika msikiti huo na hadi sasa una ukumbi uliotumiwa na wapiganaji wa Vita vya Msalaba kama ghala la kuhifadhi silaha zao. Katika Msikiti wa al Aqsa pia kuna eneo maarufu la ibada ambalo wanahistoria wanasema lilikuwa likitumiwa na Nabii Zakaria (as). Waislamu waliudhibiti kikamilifu mji wa Quds (Jerusalem) katika zama za utawala wa Khalifa Umar bin Khattab mwaka wa 15 Hijria.

Tags

Dec 19, 2017 11:25 UTC
Maoni