• Kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Hassan al Askari AS

Assalaam Aleikum Wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni tusikilize kwa pamoja kipindi hiki maalumu ambacho tumekuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka uzawa wa mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume SAW al Imam Hassan Askari AS.

Katika mtazamo wa Uislamu, Uimamu ni mwendelezo wa ujumbe wa Mtume Muhammad SAW. Bila shaka kufuata mwenendo huu kunaudhaminia Umma wa Kiislamu amani na usalama na kuukinga na madhara na vitisho mbalimbali. Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu kutokana na hekima yake na kuwatakia mema wanadamu, aliwachagulia walimwengu Maimamu kama viongozi wao wa kuwaongoza kwenye njia nyoofu na ya saada. Qur'ani Tukufu, akili, Mitume na viongozi wengine wa kidini waliokuja baada yao wanachukuliwa kuwa hoja ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu. Kuhusiana na suala hilo Imam Ali AS anasema: 'Dunia haiwi bila ya Hoja (kiongozi) wa Mwenyezi Mungu. Ima huwa ni mtu aliye wazi na anayejulikana au hujificha na kutoonekana na watu. Siri za Mwenyezi Mungu zimewekwa kwao na kila anayewakimbilia huwa yuko kwenye njia ya haki. Wao ni hazina ya elimu ya Mwenyezi Mungu......na walinzi wa dini yake. Wamesimama imara mithili ya mlima na Uislamu utaimarika kutokana na uepo wao.....''

Hii leo tuko kwenye siku za kukumbuka na kuadhimisha uzawa wa Imam Hassan Askari AS ambaye ni Hoja na Imam wa 11 wa Mwenyezi Mungu baada ya Mtume Mtukufu (saw). Huku tukikupongezeni kwa mnasaba huu adhimu wa kuzaliwa Imam huyo Mtukufu AS tunakuombeni muwe nasi katika dakika hizi chache za kipindi hiki ili tupate kujifunza machache kuhusiana na maisha ya mtukufu huyu, karibuni.

Uzawa wa Imam Hassan Askari (as)

Tarehe 8 Rabiu Thani 232 Hijiria Imam Hassan Askari alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina. Akiwa katika umri wa utotoni, mtoto huyo alilazimishwa na makhalifa wa Bani Abbas akiwa na baba yake Imam Hadi AS,  kuondoka mji huo na kuhamia katika mji wa Samarra ambao wakati huo ulikuwa makao makuu ya utawala wao. Hata kama mtukufu huyo  hakuweza kuishi zaidi ya miaka 28 lakini aliacha nyuma maarifa muhimu na adhimu ya Kiislamu.  Imam Hassan Askari AS alikuwa na huruma na upendo mkubwa uliokuwa ukiwavutia watu wengi. Historia inatwambia kwamba kuna baadhi ya watu waliokuwa wakichukia na kujitenga na Imam AS kwa kutokuwa na habari za kutosha kuhusiana na shakhsia yake lakini walipokutana naye walivutiwa sana na tabia zake na hivyo kuamua kubadilika kabisa na kuwa miongoni mwa wafuasi wake wa karibu. Miongoni mwa watu hao ni maafisa wawili waovu waliokuwa wakimtesa Imam AS alipokuwa amezuiliwa kwenye jela. Alipokuwa kwenye jela ya Bani Abbas, Imam AS alikuwa akiwaathiri pakubwa kwa maneno yake yanye mvuto mkubwa, askari magereza waliokuwa wakimchunga. Imam Hassan Askari alihudumia Uimamu kwa muda wa miaka 6 pekee ambapo alipitisha sehemu kubwa ya miaka hiyo michache akiwa uhamishoni na kwenye jela za Bani Abbas. Katika kipindi hicho ambapo ukandamizaji na dhulma ya Bani Abbas ilikuwa imefikia kilele, Imam Hassan Askari AS alipata fursa chache mno za kuweza kuandaa vikao vya masomo na mijadala ya kidini na ilikuwa vigumu sana kwake kuweza kupata fursa ya kukutana moja kwa moja na umati wa watu au kuwasiliana na wale waliokuwa na kiu ya kutafuta elimu. Kwa msingi huo Imam alitumia mbinu tofauti kama vile za kuandika barua na maandishi mengine ili kuwafikishia watu mafundisho ya dini. Ali bin Muhammad Maliki, mashuhuri kwa jina la Ibn Swabbagh ambaye ni mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu anasema hivi kumuhusu Imam Hassan Askari AS: "Alikuwa mtu wa pekee katika zama zake. Alipanda kwenye kipandio cha elimu na kutatua kwa busara, matatizo ya watu, mmoja baada ya mwingine. Vilevile alikuwa akibainisha na kuweka wazi mambo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kifikra." Wanahistoria wote wanakubaliana kwamba Imam Hassan Askari AS alikuwa hazina kubwa ya elimu na maarifa na mjuzi mkubwa zaidi katika zama zake. Alihesabika kuwa aalim na mjuzi wa pekee katika zama zake ambaye alibobea katika elimu zote ziwe ni za kiakilia au kunakiliwa (kupokelewa).

Kipindi cha Uimamu wa Imam Hassan Askari AS ndicho kipindi ambacho kilishuhudia mvurugiko mkubwa zaidi katika utwala wa Bani Abbas. Kutofaa makhalifa na mvutano katika ukoo wa ufalme, malalamiko ya watu na mapambano ya mara kwa mara na kuenea fikra potovu katika jamii ni baadhi ya mambo yaliyoibua migogoro ya kisiasa na kijamii katika zama hizo. Watawala walikuwa wakikandamiza watu waliokuwa wakiwatawala na kutumia fedha zao kujengea makasri ya kifahari huku wakipuuza matatizo na masaibu yao. Licha ya vizingiti vingi alivyowekewa na watawala hao, matatizo ya kijamnii na muda mfupi wa Uimamu wake, lakini Imam Askari AS alifanikiwa kuwalea wanafunzi mashuhuri ambao kila mmoja alikuwa na mchango mkubwa katika kueneza maarifa na mafuindisho ya Uislamu. Inasemekana kuwa wanafunzi hao walikuwa zaidi ya 100 ambapo kuna nyuso mashuhuri miongoni mwao. Katika kipidi cha Uimamu wa Imam Hassan Askari AS miji na maeneo kama vile Kufa, Baghdad, Nishabur, Qum, Khorasan, Yemen, Rei, Azerbaijan na Samarra yalikuwa miongoni mwa vituo muhimu vya Mashia. Ili kueneza utamaduni wa Shia na kuimarisha maarifa na elimu ya kidini, Imam AS aliwaandikia barua wakazi wa miji na maeneo hayo zikiwemo barua alizowaandikia watu wa miji ya Qum na Nishabur, ambazo zimenukuliwa katika vyanzo mbalimbali vya kihistoria. Imam pia aliandika vitabu kadhaa kwa ajili ya kueneza elimu na kulinda misingi ya itikadi ya Uislamu. Moja ya vitabu hivyo ni tafsiri ya sehemu kadhaa za Qur'ani Tukufu. Vitabu vyake vingine vinahusiana na sheria za Kiislamu na masuala yanayohusiana na uhalali na uharamu wa baadhi ya mambo. Mtukufu Imam pia alikuwa akishukuru na kuwapongeza waandishi na watu waliokuwa wakijihusisha na mambo ambayo yalikuwa yakiinua kiwango cha elimu, mafundisho, mwamko na fikra za watu kwenye jamii.

Nukta muhimu katika maisha ya Imam Hassan Askari AS ilikuwa ni ya kuzaliwa mtoto wake. Habari ilikuwa imeenea miongoni mwa watu kwamba mtu ambaye angekuja kuuokoa ulimwengu kutokana na dhulma pamoja na uonevu alikuwa ni mwana wa Imam Hassan Askari AS, mtoto ambaye kupitia mapambano yake angeuokoa ulimwengu kutokana na dhulma hiyo kwa kueneza uadilifu na usawa katika kila pembe ya dunia. Kwa msingi huo makhalifa wa Bani Abbas walikuwa na wasiwasi mkubwa wa kuzaliwa mtoto huyo wa Imam Hassan Askari AS. Walikuwa wamesikia hadithi nyingi zinazohusiana na kuzaliwa Mtoto wa Imam Hassah Askari ambaye angedhihiri na kuukomboa ulimwengu pamoja na kuujaza uadilifu na usawa baada ya kujaa dhulma na uonevu. Hadithi hizo zinazosema kuwa warithi na watu watakaochukua uongozi kutoka kwa Mtume Muhammad AS ni kumi na wawili na kwamba wote wanatoka katika kabila la Qureish zimepokelewa kwa wingi katika vyanzo na vitabu vya Ahlu Sunna. Kuna hadithi nyingi pia katika vitabu hivyo mashuhuri vya Ahlu Sunna zinazosema kuwa Mahdi, ambaye ni mwokozi wa ulimwengu, ni katika kizazi cha Bibi Fatimah AS. Kwa hivyo watawala wa Bani Abbas walikuwa wakimdhibiti Imam Hassan kwa wasiwasi na uaingalifu mkubwa. Hii ni kwa sababu walikuwa wakitambua vyema kuwa Imam Hassan Askari alikuwa ni Imam wa 11 wa Maimamu waliomrithi Mtume SAW na kwamba utabiri wa kuzaliwa Imam Mahdi (AF) ulikuwa umewadia. Udhibiti huo ulikuwa mkali kiasi kwamba katika baadhi ya siku za wiki, Imam alilazimishwa kufika kwenye makao makuu ya utawala wa Bani Abbas au kufungwa kwenye jela zao. Licha ya juhudi hizo zote za ukandamizaji na udhibiti wa Bani Abbas dhidi ya Imam Askari AS lakini Mwenyezi Mungu alitaka Imam Mahdi (AF), mwana wa Imam Hassan Askari AS azaliwe tu.

Imam Askari AS alificha na kukufanya kuwa siri kubwa kuzaliwa kwa mwanawe Imam Mahdi (AF). Ni wazi kuwa kama maadui wangepata habari ya kuzaliwa kwake wangefanya njama za kumuua. Pamoja na hayo yote lakini Imam aliwaonyesha baadhi ya wafuasi wake wa karibu na waaminifu mtoto huyo ili baada ya kuuawa shahidi kwake wasije wakachanganyikiwa na kutomjua Imam wao wa zama waliyepasa kumfuata. Ni kutokana na hatua hiyo ya busara ya Imam Askari ndipo mara tu baada ya kuuawa kwake shahidi, wafuasi wake wote walikubaliana kwa sauti moja kwamba Imam alikuwa amewaainishia mtoto wake kuwa Imam ambaye walipasa kumfuata baada yake. Hatua nyingine ya busara aliyoichukua Imam ni kutayarisha fikra za watu ili wapate kujiandaa kwa ajili ya Imam wao huyo wa baada yake, yaani Imam Mahdi (AF), kuondoka machoni pao na kughibu kwa muda. Hii ni kwa sababu watu walikuwa hawajawahi kupitia kipindi kama hicho cha kughibu Imam wao, na kwa hivyo kulikuwepo na haja ya kuwatayarisha kifikra. Hadi wakati huo, wafuasi na wapenzi wa Ahlul Beit walikuwa wamezoea kwenda na kukutana moja kwa moja na Maimamu wao na kuwaelezea matatizo yao ya mtu binafsi na ya kijamii. Kwa msingi huo watu walikuwa wamezoe kukutana ana kwa ana na Maimamu wao. Lakini baada ya hapo hali ingebadilika na kuwalazimu kutokutana tena moja kwa moja na Imam wao. Hivyo Imam alilazimika kuwaandaa kisaikolojia na kifikra kwa ajili ya hali hiyo mpya ya ghaiba ambayo kidhahiri ingewatenganisha na Imam wao wa Zama. Kutokana na udharura huo Imam Askari AS aliwalea baadhi ya wafuasi wake ambao wangechukua jukumu la kusimamia kipindi hicho cha ghaiba. Imam AS alitumia mbinu tofauti kuwashawishi watu kwamba katika kipindi cha ghaiba, wawafuate na kuwasikiliza wanazuoni, mafakihi na wapokezi wa hadithi ambao walilelewa na Maimamu wa Ahlul Beit AS, ili wapate kujifunza kutoka kwao mafundisho ya kidini.

Haram ya Imam Hassan Askari (as) mjini Samarra

 

Miongoni mwa sifa muhimu za Imam Hassan Askari AS ni kutosalimu amri kwake mbele ya watawala dhalimu na irada yake isiyoterereka katika kutetea fikra na mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu. Mu'tamid Abbasi, mtawala wa Bani Abbas alikuwa akifahamu vyema ushawishi mkubwa wa kimaanawi na kielimu aliokuwa nao Imam Askari AS katika jamii. Alikuwa akishuhudia vyema jinsi matabaka mbalimbali ya watu yalivyokuwa yakimpenda na kumfadhilisha mjukuu huyo wa Mtume SAW juu ya watu wengine wote. Hapo alihisi kwamba jambo hilo bila shaka lingedhoofisha misingi ya utawala wake wa kidhalimu. Hivyo aliamua kufuta na kumuondoa mtukufu huuyo AS miongoni mwa watu kwa njia yoyote ile. Wakati Imam AS anaaga dunia hakuwa amezidisha umri wa miaka 28. Imam huyo ameacha nyuma mwanawe mwenye umuhimu na thamani kubwa, Imam Mahdi (AF) ambaye ni Imam na Hoja ya Mwenyezi Mungu kwa walimwengu. Imam ambaye siku moja atadhihiri na kuujaza ulimwengu uadilifu na usawa baada ya kuwa umejaa dhulma na uonevu.

Kwa mara nyingine tena wapenzi wasikilizaji, tunatoa mkono wa pongezi na fanaka kwa Waislamu wote duniani na hasa wapenzi na wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) kwa mnasaba huu adhimu wa kusherehekea uzawa wa mmoja wa wajukuu wa Mtume, Imam Hassan Askari AS. Tunamuomba kwa baraka zake atuwezeshe kuwa miongoni mwa wafuasi halisi na wa kweli wa njia yake tukufu, Amin. Tunahitimisha kipindi hiki maalum kwa kunukuu Hadithi ya Imam huyo Mtukufu al-Imam Hassan Askari ambapo amesema: "Sisi ni kimbilio la watu ambao hutukimbilia, na nuru na mwangaza wa wale wanaotaka fikra na ufahamu kutoka kwetu. Mtu anayetupenda sisi (Watu wa Nyumba ya Mtume) atakuwa pamoja nasi katika daraja za juu Peponi.'

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Dec 25, 2017 08:11 UTC
Maoni