Feb 01, 2018 08:12 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu katika mstari wa mbele wa kupinga uistikbari na kuunga mkono mapambano ya Kiislamu

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii maalumu niliyowaandalieni kwa munasaba wa siku hizi za maadhimisho ya kuingia katika mwaka wa 40 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya 1979. Katika makala hii ya leo tutaangazia kadhia ya 'Mapinduzi ya Kiislamu katika mstari wa mbele wa kupinga uiskitabiri wa kimataifa na kuunga mkono muqawama au mapambano ya Kiislamu.

Mwenyezi Mungu SWT anawapa ahadi ifuatayo watu ambao kwa kumtegemea yeye, wanasimama kidete mbele ya madhalimu na kupambana na waistikbari:"Hakika waliosema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa." Suuratul Fuss'ilat Aya ya 30.

Harakati ya Waislamu wa taifa la Iran, ambayo ilipata ushindi mwaka 1979 ilifanikwa kwa sababu ilijengeka katika msingi wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Wananchi wa Iran, chini ya uongozi wa Imam Khomeini MA, muasisi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  waliamini kuwa, kufuata mafundisho ya Kiislamu ndio njia bora na muafaka zaidi ya kufikia saada na ufanisi duniani na Akhera.

Moja ya malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu ni kusimama kidete mbele ya uistikbari au kwa maneneo mengine kupinga na kupambana na uistikbari. Kwa hakika kupambana na uistikbari kunafanyika kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu ambayo yanapinga kila aina ya dhulma. Kimsingi Uislamu unapinga kuwadhulumu wengine na pia unamtaka muumini asikubali kudhulumiwa na asimame kidete kukabiliana na dhulma na madhalimu. Kuhusiana na hili, Imam Khomeini MA alisema: "Sisi hatudhulumu, na wala hatukubali kudhulumiwa na wengine."

Wakati Uislamu unapopinga dhulma, ni wazi kuwa pia unalaani uistikbari kwani uistikbari maana yake ni dhulma na kukataa kukubali haki sambamba na hisia ya kujiona bora.

Uistikbari ni msamiati wa Qur'ani Tukufu na umekaririwa mara kadhaa katika kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu na  kwa msingi huo msamiati huo ni sehemu isiyotenganika na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Muistikbari wa kwanza alikuwa ni shetani ambaye alijiona kuwa mbora na kutokana na kiburi chake aliasi amri ya Mwenyezi mungu SWT ya kumsujudia Adam. Qur'ani Tukufu pia imewataja watu kama Qarun, Firauni na Haman (Waziri wa Firaun) na pia baadhi ya kaumu zilizopita ambazo ziliasi kuwa za kiistikbari.

Mwenyezi Mungu SWT katika Qurani Tukufu amewataja wenye kiburi na mustakbirina kwa kusema: Nitawatenga na Ishara zangu wale wanaofanya kiburi katika nchi bila ya haki. Na wao wakiona kila Ishara hawaiamini. Wakiiona njia ya uwongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu, na wameghafilika nazo. Suurat Al-A'raaf 146.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamejengeka katika msingi wa nadharia hiyo ya Qur'ani Tukufu ya kupambana na madhalimu na mustakbirina na ni kwa msingi huo ndio madhalimu na mustakbirina katika zama hizi wakachukizwa sana na Mapinduzi ya Kiislamu na hadi sasa wanaendeleza chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kipengee cha 154 cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimeashiria saada, uhuru, kujitegemea, serikali ya haki na uadilifu na haki kwa watu wote duniani na kuongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sambamba na kujiepusha na uingiliaji wowote wa mambo ya ndani ya mataifa mengine, inaunga mkono mapambano ya kutetea haki ya mustadhaafina mbele ya mustakbirina katika kila eneo la dunia."

Leo  misdaki ya wazi zaidi ya uistikbari duniani ni utawala wenye sera za kujitanua na za kikoloni wa Marekani.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amezungumza kwa mapana kuhusu suala  hili na hapa tunaweza kuashiria sehemu ya mtazamo wake aliposema: "Uistikbari ulikuwepo na ungali unaendelea katika zama hizi. Muundo wa kimsingi wa uistikbari ni sawa katika zama zote. Kile kinachotafautiana ni mbinu na sifa kwa kutegemea zama. Leo pia kuna mfumo wa uistikbari duniani ambao unaongozwa na Marekani."

Malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu katika kupambana na uistikbari yamejengeka katika msingi wa mafundisho ya Kiislamu na pamoja na kuwepo wimbi la propaganda za vyombo vya habari vya Kimagharibi, malengo hayo ya Mapinduzi ya Kiislamu yanaungwa mkono na mataifa ya Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu.

Miongozo ya Imam Khomeini MA na baada yake, Ayatullah Khamenei ni jambo ambalo limepelekea walimwengu hasa katika eneo la Asia Magharibi kupata moyo na motisha wa kukabiliana na uistikbari wa Marekani. Kwa msingi huo, mapambanao ya wananchi yemeanzishwa na yanaendelea  Palestina, Lebanon, Iraq, Yemen, Bahrain na nchi zingine. Watu wa mataifa hayo wameamka na wanakabiliana kwa nguvu zao zote na madola ya kibeberu yakiongozwa na waitifaki wake ukiwemo utawala wa Kizayuni wa Israel.

Huko Palestina, makundi ya mapambano  kama vile Hamas na Jihad Islami yameibuka na yanaamini kuwa, mapambano ya silaha katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel ndio njia pekee ya kukomboa ardhi za Palestina.

Uzoefu uliofeli wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina, PLO, katika kujaribu kuelewana na kufanya mazungumzo na utawala ghasibu wa Israel ni ishara ya wazi kuwa Wazayuni hawafungamani na ahadi wanazozitoa katika meza ya mazungumzo bali wanatafakari kuhusu kukalia kikamilifu Quds Tukufu, ardhi zote za Palestina na hata baadhi ya nchi jirani. Idadi kubwa ya Wapalestina wameuawa shahidi katika mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni na hadi sasa kumekuwa na Intifadha (mwamko) kadhaa dhidi ya utawala huo ghasibu. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa ni wadhifa wake kusaidia harakati za mapamabano ya ukombozi wa Palestina na imekuwa ikitekeleza kivitendo sera hiyo. Ni kwa msingi huo ndio kiongozi wa Hamas, Ismail Haniya, hivi karibuni akamuandikia barua Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kumshukuru kwa uungaji mkono wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa harakati za ukombozi wa Palestina.

Wapiganaji wa Hezbullah katika oparesheni

Leo harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imegeuka na kuwa jinamizi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na imekuwa kizingiti katika kuenezwa sera za kibeberu na kutaka kujitanua Marekani katika eneo. Hizbullah iliasisiwia mwaka 1981 kufuatia ilhamu kutoka kwa fikra za kupambana na dhulma za Mapinduzi ya Kiislamu. Kufuatia mapambano ya muda mrefu, hatimaye mwaka 2000, Harakati ya Hizbullah ilifanikiwa kulishinda na kulidhalilisha jeshi la kisasa la utawala haramu wa Israel. Pia katika vita vya siku 33 vya 2006, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walishindwa vibaya katika makabiliano na wapiganaji shupavu wa Hizbullah.

Leo harakati ya Hizbullah ambayo inapata uungaji mkono wa  Iran, imebadilika na kuwa kigezo kwa mataifa mengine yanayopambana na madhalimu. Kushiriki wapiganaji wa Hizbullah katika vita dhidi ya magaidi wa kitakfiri wanaopata himaya ya Marekani na Saudia huko Syria ni nukta nyingine yenye kuashiria ushawishi mkubwa wa harakati hii ya Kiislamu. Nchini Iraq hali kadhalika harakati kadhaa zimeibuka nchini humo ambazo zimeathiriwa pakubwa na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na hapa tunaweza kuashiria harakati iliyaonzishwa na Imam Mohammad Baqir Sadri na dada yake, Bintul Hudaa ambao walikuwa wapinzani wakubwa wa udikteta wa Saddam na hatimaye waliuawa shahidi kutokana na harakati zao. Baraza la Kiislamu la Iraq limeendeleza harakati hiyo ya Sadr. Hapa pia tunaweza kutaja harakati ya wananchi wa Iraq ya Hashdu Shaabi ambayo imekuwa na nafasi kubwa katika kuangamiza magaidi wa ISIS wanaopata uungaji mkono wa uistikabari nchini humo. Nchini Bahrain pia kuna harakati inayopambana dhidi ya utawala wa kiimla nchini humo ambao unapata himaya ya Marekani na Saudi Arabia.

Wapiganaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen wanaopambana na wavamizi Wasaudi

Watu wa Yemen pia wako katika harakati ya kupambana na kukabiliana na hujuma ya utawala wa Saudia ambao unapata himaya ya Marekani na wameweza kutoa pigo kubwa kwa wavamizi. Kilicho wazi katika makundi hayo yote ni kuwa yamepata ilhamu kutoka kwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Harakati hizo, sawa na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran zinategemea nguvu za wananchi na mafundisho ya Uislamu halisi. Nukta nyingine muhimu ya harakati hizo za Kiislamu ni kutochoka na kutopoteza matumaini katika mapambano dhidi ya madola ya kibeberu na kiistikbari hasa Marekani, Uingereza, Saudia na utawala wa Kizayuni.

Qurani Tukufu inatoa bishara njema ifuatayo kwa wale wanaopambana dhidi ya mustakbirina: Hakika waliosema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa. Suuratul Fuss'ilat Aya ya 30.

 

Tags

Maoni