Mwanzoni mwa mwezi wa Januari Michael Wolf, mwandishi wa Kimarekani alianza kusambaza kitabu ambacho kimeshika nafasi ya kwanza katika orodha ya vitabu vinavyouzwa kwa wingi zaidi katika mtandao wa Amazon.  

Nakala zote za kitabu hicho zilimalizika papo hapo katika maduka ya kuuza vitabu mjini New York nchini Marekani katika siku ya kwanza ya kuanza kuuzwa kitabu hicho. Kitabu hicho ambacho Rais Donald Trump wa Marekani na mawakili wake siku kadhaa kabla walifanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba hakitolewi na kuuzwa, kimepewa jina la Fire and Fury: Inside the Trump White House (Moto na Ghadhabu, Ndani ya Ikulu ya Trump). Kitabu hiki kinachunguza shakhsia ya Rais wa Marekani Donald Trump na kukosoa utendaji wake katika mwaka mmoja uliopita. Mwandishi wa kitabu hicho, Michael Wolf anasema: "Kitabu hiki kimetegemea zaidi ya mahojiano 200 na Rais wa Marekani na maafisa wake wa ngazi za juu katika kipindi cha miezi 18 iliyopita." Katika mahojiano yake na televisheni ya NBC Wolf amempiga vijembe Donald Trump na kusema kwamba: Ananisaidia sana kuuza kwa wingi kitabu changu na matamshi yake yanathibitisha yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki. Si jambo la kawaida kabisa kuona Rais wa Marekani akifanya jitihada za kuzuia kuchapishwa kitabu", mwisho wa kunukuu. 

Katika kitabu cha Fire and Fury, Michael Wolf anafichua picha ya ndani ya White House kwa kutegemea mahojiano aliyofanya na baadhi ya maafisa wa Ikulu ya Rais wa Marekani akiwemo Steve Bannon. Anasema mwenendo wa Trump ndani ya White House ni kama wa mtoto mdogo asiye na uwezo wa kuongoza nchi. Vilevile mshauri mkuu wa masuala ya uchumi wa Trump, Gary Cohen anafichua katika kitabu hicho kwamba: Trump hasomi chochote hata muhtasari wa ripoti zenye ukurasa mmoja anazoletewa kila siku. Huamka kutoka kwenye usingizi katika vikao muhimu na viongozi wa dunia, kwa sababu huonekana mchofu na asiye na hamu ya chochote. Wolf anaendelea kuandika kuwa: Kwa mtazamo wangu mimi ni kwamba Donald Trump hasomi wala kupitia lolote. Tatizo la pili ni kwamba, Trump si tu kwamba hapitii wala kusoma ripoti na muhtasari anaopewa na washauri wake lakini pia hasikilizi maneno yao. Kwa msingi huo kushindwa kumwambia lolote Trump umekuwa mgogoro wa washauri wake tangu siku ya kwanza kabisa."

Mshauri Mkuu wa zamani wa Donald Trump, Steve Bannon ambaye wachambuzi wengi wanasema ushindi wa Trump ulitegemea sana stratijia zake, anafichua katika kitabu hicho kwamba, Rais wa Marekani ni mtu asiye na mlingano wa kinafsi. Bannon anafichua katika kitabu cha Fire and Fury kwamba: Trump ni mchoyo na mbinafsi ambaye hakipi umuhimu kitu chochote isipokuwa nafsi yake. Bannon anaamini kuwa, Donald Trump anazidi kupata utajiri kutokana na kuuza jina lake na kwamba jina lake linaonekana kwa wingi katika mahoteli, makasino na vilabu vya anasa na viwanja vya mchezo wa golfu. Anasema: "Ndani ya White House, Trump anafanya kazi kama alivyokuwa katika mchezo wa filamu aliyoshiriki hapo kabla ya The Trainee ambako alikuwa akitumia istilahi ya: "Umetimuliwa kazi".  

Kuchapishwa na kuanza kuuzwa kitabu cha "Moto na Ghadhabu Ndani ya White House ya Trump" kumekabiliwa na hasira kali ya kiongozi huyo, na mawakili wake walifanya jitihada kubwa za kusimamisha uuzaji wake nchini Marekani. Katika mahojiano yake na kanali ya televisheni ya CNN, mwanahistoria wa Marekani Tim Naftali amesema kuhusu mienendo ya Trump na jinsi alivyokabiliana na suala la kuchapishwa na kuuzwa kitabu hicho kwamba: Hakukuwepo haja ya kutolewa kitabu hiki kwa ajili ya kudhihirisha wazi mienendo mibaya ya Donald Trump ambaye badala ya kupuuza kitabu hicho amekishambulia moja kwa moja na hawezi kujidhibiti."      

Ufichuaji wa kitabu cha Fire and Fury haukuishia katika shakhsia na mienendo binafsi ya Doland Trump bali pia umegusia anga inayotawala sasa nchini Marekani. Hivi sasa uchunguzi unaofanywa na Inspekta Muller kuhusu kiwango cha uingiliaji kati wa Warussi na aina yake katika uchaguzi wa rais wa Marekani ni miongoni mwa mijadala mikubwa nchini humo. Japokuwa kitabu hicho hakikumuashiria moja kwa moja Trump katika kadhia hiyo lakini mwandishi wake anamnukuu mshauri wake mkuu wa zamani, Steve Bannon akisema: Donald Junior Trump, mtoto wa kiume wa Rais wa Marekani alikuwa na mawasiliano na Warussi na anayataja mazungumzo na mawasiliano hayo ambayo yalifanyika katika kipindi chote cha kampeni za uchaguzi wa rais uliomfikisha madarakani Trump kuwa ni ya "kisaliti" na "yasiyo ya kizalendo". Donald Trump amejibu matamshi hayo kwa kusema: Bannon amepagawa na kurukwa na akili.  

Trump na Steve Bannon

Miongoni mwa mambo yaliyofichuliwa katika kitabu cha Moto na Ghadhabu Ndani ya White House ni ushirikiano uliopo baina ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman na Donald Trump na familia yake. Mwandishi wa kitabu hicho anasema, ushirikiano huo umejengeka juu ya ufahamu finyu na mdogo. Mwandishi wa kitabu hicho aliyetegemea mahojiano yake na baadhi ya maafisa wa White House anafichua kuwa, baada ya kutangazwa Muhammad bin Salman kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Trump alisema kuwa yeye na mkwe wake, Jarde Kouchner wamepanga mapinduzi nchini Saudi Arabia na kumpachika kibaraka wao yaani Muhammad bin Salman, katika uongozi wa Saudia. Kitabu hicho pia kina ushahidi mpya kuhusu uungaji mkono wa Trump kwa ukandamizaji unaofanywa na Bin Salman dhidi ya wanamfalme wenzake huko Saudia.  

Michael Wolf

Michael Wolf anaandika kuwa: "Rais Donald Trump amepuuza maagizo ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni au kupingana nayo na kuafiki mpango wa dhulma na mabavu wa Wasaudia dhidi ya Qatar. Mtazamo wa Trump ni kuwa, Qatar inayasaidia kifedha makundi ya kigaidi, lakini mwenendo kama huo huo wa Saudi Arabia wa kuyafadhili makundi ya kigaidi unapaswa kufimbiwa jicho. Trump alihalalisha mtazamo wake huo kwa kudai kuwa, baadhi ya wanachama wa familia ya kifalme ya Saudi Arabia tu ndio wanaotoa misaada ya kifedha kwa makundi ya kigaidi," mwisho wa kunukuu.  

Katika sehemu nyingine ya kitabu cha Moto na Ghadhabu Ndani ya White House, mwandishi anaashiria mizizi na chanzo cha mitazamo mikali ya Trump dhidi ya Iran na kusema kuwa, kiongozi huyo wa Marekani amelifanya suala la vita na propaganda chafu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kuwa msingi wa siasa zake za nje. Michael Wolf anaandika kwamba: Trump amejifunza kutoka kwa mshauri wake wa zamani wa usalama wa taifa, Michael Flynn kwamba "kila mtu anayeipinga Iran ni mtu mzuri sana".

Ufichuaji wa kitabu cha Fire and Fury sasa unapewa mazingatio makubwa na walimwengu hususan nchini Marekani. Mwandishi wake, Michael Wolf ameiambia televisheni ya CNN kwamba: "Kipindi cha sasa ni kipindi kibaya na cha aina yake na mwelekeo mkubwa wa watu kwenye kitabu changu ni ithibati kwamba yaliyomo hayakutiwa chumvi. Kwa msingi huo inatupasa kusema kuwa, kitabu hiki ni aina ya utekelezaji wa kifungu nambari 25 cha Katiba."

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, kifungu hicho cha Katiba ya Marekani kinahusiana na suala la kutafuta rais mpya wa nchi hiyo wakati mienendo na hali ya kiakili na kinafsi ya rais aliyeko madarakani inapotiliwa shaka.

Licha ya White House na Donald Trump mwenyewe kukanusha yaliyozungumzwa ndani ya kitabu hicho wakisema kuwa hayana msingi, lakini uchunguzi wa kwanza wa maoni uliofanywa na taasisi ya Gallup wiki moja baada ya kuanza kuuzwa umeonesha kuwa kiwango cha umaarufu wa Trump kimeshuka kwa asilimia mbili na kufikia asilimia 37.

Kwa kutilia maanani uhakika uliofichuliwa na Michael Wolf kuhusu mienendo ya Doland Trump ndani ya Ikulu ya White House, tunaweza kusema kuwa, yaliyomo ndani ya kitabu hicho yatashughulisha sana akili na fikra za Trump katika miezi ijayo na kuathiri maamuzi na mitazamo yake isiyo ya busara.       

Tags

Feb 03, 2018 18:34 UTC
Maoni