• Marekani na makabiliano ya daima dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu

Kipindi hiki kimejaribu kutupia jicho kwa ufupi uadui ambao umekuwa ukiendeshwa na Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa karibu miaka 40 iliyopita.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanakaribia kuingia katika mwaka wake wa 40. Kwa kawaida miaka 40 huwa ni umri wa kukomaa mwanadamu na mfano au umri huu pia unaweza kutumika kuhusiana na mapinduzi haya ya Kiislamu. Katika kipindi hiki cha miaka 40 Mapinduzi ya Kiislamu yamevuka milima na mabonde mengi. Ikiwa tunataka kuashiria moja ya masuala ambayo daima yamekuwa yakiyaandama mapinduzi haya ya Kiislamu hatuwezi kukosa kuashiria uadui wa watawala wa Marekani dhidi ya mapinduzi haya. Ili tupate kujua vyema chanzo cha uadui huo tunapasa kurejea nyuma hadi kipindi cha kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kufahamu nafasi iliyokuwa nayo Iran katika siasa za Mashariki ya Kati na kimataifa za Marekani. Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilikuwa na nafasi maalumu katika siasa za nje na za usalama za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu mzima kwa ujumla. Katika kipindi hicho na kwa mtazamo wa Jumuiya ya Kijeshi ya Nchi za Magharibi Nato, Iran ndiyo ilikuwa katika nukta ya mwisho kijografia kabla ya kukutana na hasimu mkuu wa nchi hizo yaani Russia, kambi kuu ya kijeshi ya Mashariki. Kwa msingi huo Marekani haikuwa tayari kufumbia macho nafasi ya kistartijia ya Iran katika kukabiliana na Russia, hivyo baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia ilifanya juhudi kubwa za kuimarisha nafasi yake ya kijeshi na kisiasa nchini Iran. Ili kufikia lengo hilo la kibeberu nchini Iran, Marekani haikuwa ikizingatia misingi wala thamani zozote za maadhili wala demokrasia. Kuhusu suala hilo, mwaka 1953 Marekani ilifanya mapinduzi dhidi ya serikali halali ya Dakta Muhammad Muswadiq na hivyo kuvuruga juhudi zote za kuimarisha demokrasia nchini hapa. Baada ya kutekelezwa mapinduzi hayo yaliyofanyika kwa ushirikiano na nchi nyingine ya kikoloni yaani, Uingereza, Marekani ilimrejesha nchini hapa Mfalme Muhammad Ridha na hivyo kubuni msingi wa kurejeshwa nchi mfumo wa udikteta na ukandamizaji. Katika uwanja huo, Marekani na utawala ghasibu wa Israel zilianzisha Savak nchini hapa ambalo lilikuwa ni shirika la ujasusi la kuogofya zaidi duniani na ambalo lilitumiwa na Wamarekani na Wazayuni kwa ushirikiano wa vibaraka wao nchini kuzima sauti za wapigania uhuru. Marekani ilitumia washauri na vibaraka wake kudhibiti mifumo yote ya kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kiutamaduni nchini na wakati huo huo kuulazimisha utawala wa wakati huo wa Iran kupitisha sheria ya Capitulation ambayo iliwapa Wamarekani kinga ya kushtakiwa humu nchini. Katika kipindi cha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kulikuwa na washauri wa Marekani wapatao 30,000 nchini Iran.


Uzoefu mchungu wa vita wa Marekani huko Korea na Vietnam ambao ulipelekea askari wengi wa nchi hiyo ya Magharibi kupoteza maisha yao katika vita hivyo uliwapalekea watawala wa White House kufikia natija hii kwamba ilikuwa ni kwa maslahi yao kukabidhi utekelezaji wa siasa zao za ubeberu Mashariki ya Kati kwa vibaraka wao katika eneo. Kwa msingi huo juhumu hilo la polisi wa Marekani katika Mashariki ya Kati na hasa eneo la Ghuba ya Uajemi lilikabidhiwa Iran iliyokuwa ikitiwaliwa na Shah. Iran katika kipindi hicho ilikuwa na nafasi bora zaidi ikilinganishwa na nchi nyingine za eneo, kwa kuzingatia utajiri wake, idadi kubwa ya watu wake, nafasi yake ya kistratijia, uthabiti wa kisasa na nguvu yake kubwa ya kijeshi. Hapo ndipo sera za Nguzo Mbili za Rais Richard Nixon wa Marekani zilipoanza kutekelezwa kuhusiana na Mashariki ya Kati. Kwa mujibu wa sera hizo, serikali za Iran na Saudi Arabia zilichukuliwa kuwa nguzo mbili muhimu za Marekani katika eneo na hivyo kutwikwa jukumu la kusimamia utekelezaji wa siasa za Marekani katika Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo nchi mbili hizi zilipewa misaada chungu nzima ya kiuchumi na kijeshi na kuchukuliwa kuwa chombo cha kutekelezwa siasa za Marekani bila ya Marekani yenyewe kuwa katika eneo hili. Katika hili pia Iran ilithaminiwa zaidi kuliko Saudia na hivyo kupata misaada zaidi ya kifedha na kijeshi kutoka kwa Marekani na nchi nyingine za Magharibi. Kwa kuzingatia ongezeko kubwa la bei ya mafuta mwaka 1973 ambalo lilipelekea pato la Iran kuongezeka maradufu, Nixon aliamua kumwaga silaha za Marekani nchini Iran kwa gharama ya serikali ya Tehran na hivyo kuifanya Iran kuwa mnunuzi mkubwa zaidi wa silaha za nchi hiyo katika eneo. Marekani iliiuzia Iran ndege za kivita aina ya F14 katika hali ambayo hakuna hata mshirika mmoja wa Marekani katika eneo na hasa utawala ghasibu wa Israel, waliopewa ndege hizo. Wamarekani walikuwa wakiichukulia Iran kuwa kisiwa cha amani na usalama katika Mashariki ya Kati. Hivyo Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yalikuwa mfano wa zilzala ambayo ilisambaratisha siasa zote za kieneo na kimataifa za Marekani nchini Iran. Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuondoka Iran katika mackucha ya ubeberu wa White House ni dalili kuu ya kuanza uadui wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ni kwa sababu baada ya ushindi huo, ushawishi na satwa ya Marekani Mashariki ya Kati ilipungua kwa kiwango kikubwa na siasa zake kupata pigo kubwa kutoka kwa Mapinduzi ya Kiislamu.

Muhammad Ridha Shah, polisi wa Marekani katika eneo

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani ilianza kutumia misamiati kama 'Uislamu wenye misimamo mikali' katika duru za kiasa na kihabari ili kuhalalisha siasa na juhudi zake za kutaka kuupindua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. Hata hivyo ni wazi kuwa kushikamana Iran na misingi pamoja na thamani za Kiislamu ni moja ya sababu za kuchukiwa kwake na watawala wa Marekani wanaofanya njama usiku na mchana ili kuusambaratisha mfumo wa Kiislamu nchini. Kuhusiana na suala hilo, Brzezinski, mwananadharia mashuhuri na ambaye alikuwa mshauri wa usalama wa taifa wa Rais Jimmy Carter wa Marekani katika kipindi cha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, alisema kwamba kuhuishwa Uislamu halisi Mashariki ya Kati kufuatia kuangushwa Shah na matokeo yake nchini Iran ya Khomeini, lilikuwa tishio kubwa na la kudumu dhidi ya maslahi ya Marekani katika eneo ambalo maisha ya nchi za Magharibi yalikuwa yanafungamana nalo moja kwa moja. Alisema: 'Uislamu unaofuata mafundisho ya kimsingi ni suala ambalo hii leo linatishia mfumo na uthabiti uliopo.' Ayatullah Khamenei Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema kuhusiana na suala hili kwamba: 'Hii leo uadui wa kambi ya uistikbari dhidi ya Iran ya Kiislamu unatokana na Uislamu. Wana uadui na Uislamu ndio maana wanatoa mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wallahi hakuna sababu nyingine yoyote inayoifanya Marekani ilichukie taifa la Iran isipokuwa kutokana na kuwa wao ni Waislamu wanaoshikamana vyema na mafundisho ya Uislamu halisi na hivyo wanataka nyinyi muachane na mshikamano huu.'

Ayatullah Khamenei

Moja ya baraka kubwa za Mapinduzi ya Kiislamu ni kujitawala pamoja na mapambano yake dhidi ya ubeberu wa madola makubwa kama Marekani. Noam Chomsky mwandishi mashuhuri wa Marekani anasema: 'Uadui wa Marekani dhidi ya Iran utaendelea madamu nchi hiyo inaendelea kuwa huru na kutosalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani. Kwa mtazamo wa Marekani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikubaliki kabisa kwa sababu haifumbii macho kujitawala kwake.' Martin Indyk, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Marekani aliyekuwa akishughulikia masuala ya Mashariki ya Kati katika wizara hiyo na mmoja wa viongozi wa Marekani walio na chuki kubwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anasema hivi kuhusiana na Iran ya Kiislamu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu: 'Kuadhibiwa Mapinduzi ya Kiislamu litakuwa somo kwa nchi nyingine zilizochagua njia ya kujitawala na kutoitegemea Marekani.'

Mapinduzi ya Kiislamu yamepiga hatua kubwa katika nyanja za elimu na maendeleo na sasa yanachukuliwa kuwa mfano bora wa kuigwa na nchi nyingine. Kuhusu hili Ayatullah Khamenei anasema: 'Uadui wa mfumo wa uistikbari wa Maerekani na waistikbari wengine duniani kwa mfumo wa Kiislamu ni kutokana na upeperushaji wake wa bendera ya uadilifu. Ni kwa sababu wanaona nchi ikiwa katika harakati za kufikia ustawi na maendeleo ya kielimu na kivitendo kwa jina la Uislamu na mafundisho yake aali, na wanafahamu vyema kwamba jambo hilo litazuia ushawishi wao. Wao wanapinga kila nchi ambayo inajitahidi kufikia ustawi na maendeleo ya kielimu nje ya udhibiti na ushawishi wao.'

Taathira na ushawishi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika harakati zinazopigania uhuru na kujitawala katika pembe tofauti za dunia na kuchukuliwa mapinduzi hayo kuwa mfano bora wa kuigwa katika mapambano na madola makubwa pamoja na kuimarishwa moyo wa mapambano dhidi ya uistikbari wa kimataifa kwenye harakati hizo, ni dalili nyingine ya Marekani kudumisha uadui wake dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu. Alexander Haig, Waziri wa Ulinzi wa Marekani katika kipindi cha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema: 'Kwa mtazamo wangu tatizo hatari na muhimu zaidi kati ya matatizo haya ya kimataifa, ni matokeo ya kuenea Uislamu unaozingatia mafundisho halisi na ya msingi ambao chimbuko lake ni Iran na sasa unaenea na kutishia nchi za Iraq na uthabiti wa tawala za Kiarabu zilizo na misimamo ya wastani katika eneo. Ikiwa Iran haitadhibitiwa bila shaka maslahi ya madola makubwa yatahatarishwa kwa njia ya kutisha.' Wasiwasi wote waliokuwa nao watawala wa Marekani pamoja na wananadharia wao kuhusiana na matokeo ya Mapinduzi ya Kiislamu na udharura wa kukabiliano nayo sasa umethibiti. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata mafanikio na maendeleo makubwa kitaifa na kieneo. Hakuna mtu yoyote anayeweza kupuuza na kufumbia macho nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu katika kudhamini usalama na utulivu wa Mashariki ya Kati. Kadiri Iran ilivyobadilika na kuwa nchi yenye nguvu na taathira kubwa katika eneo na ngazi za kimataifa, ndivyo chuki na uadui wa Marekani dhidi yake pia umeongezeka. Kwa kadiri kwamba Mike Pence Makamu wa Rais Donald Trump wa Marekani alisema wazi wazi hivi karibuni alipokuwa akizitembelea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel kwamba ikiwa taifa la Iran linataka kuwa rafiki wa Marekani njia pekee ya kufanya hivyo ni kuiangusha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ama kama alivyosema Imam Khomeini (MA) Mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika kilele cha vita vya kulazimishwa, kipindi cha Vita Baridi na pia katika kilele cha nguvu ya Marekani katika kuitishia Iran kwamba hakuna chochote Marekani inachoweza kufanya, hivi sasa pia hakuna chochote kinachoweza kufanywa na nchi hiyo ya kibeberu mbele ya Mapinduzi imara ya Kiislamu ya Iran. Kama tunavyoshuhudia sasa Marekani imetengwa katika ngazi za kimataifa kutokana na siasa mbovu za Donald Trump na hivyo haina uwezo wowote wa kuidhuru Iran ya Kiislamu ambayo ina uzoefu mkubwa wa miaka 40 katika mapambano yake dhidi ya mfumo wa ubeberu duniani.

Tags

Feb 05, 2018 11:07 UTC
Maoni