•  Kujiamini na ustawi wa kisayansi Iran

Hamjambo wapenzi wasikilizaji. Tuko katika siku hizi ambazo ni maarufu kama Alfajiri 10, ambazo ni siku za kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979. Tumewaandalia makala kadhaa kwa munasaba huo na leo tutaangazia maendeleo na mafanikio makubwa ya watu wa Iran katika uga wa sayansi kutokana na kujiamini taifa hili la Kiislamu. Karibuni.

Waledi wa mambo katika kufafanua kuhusu mizizi ya kuibuka Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran wanasema moja ya sababu za kushika kasi harakati za Mapinduzi nchini Iran ni ghadhabu ya wananchi ambao walikuwa wamedhalilishwa na watawala wa kiimla na waitifaki wao wa kigeni. Wananchi waliamini kuwa Ufalme wa Kipahlavi ulikuwa umelidhalilisha sana taifa la Iran na ni kwa sababu hii ndio, wakaitikia wito wa Imam Khomeini MA ambaye alikuwa akiwanadi kuelekea katika uhuru, kujitegemea na kujiamini. Kwa mtazamo huo tunaweza kusema kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ni natija ya kujiamini na kuwa na imani kuhusu uwezo wa kitaifa. Iwapo tutaangazia miongozo ya muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini MA, tunaona namna alivyosisitiza kuhusu udharura wa kuimarisha hisia ya kujiamini. Kwa mfano, katika kutathmini utendaji mbovu wa utawala wa kifalme wa Pahlavi alisema: "Nukta muhimu ni kuwa Wairani wafahamu kuwa wanaweza kutekeleza jambo wanalotaka. Kwa muda mrefu ilikuwa ikienezwa dhana kuwa Wairani hawawezi kufanya chochote na kwamba vitu wanavyohitajia vinapaswa kuagizwa kutoka nje ya nchi. Kutoka Ulaya au Marekani. Hili ni jambo ambalo lilipelekea Wairaini wasitumie uwezo wao wa kiakili na hivyo wazembee kifikra. Wairani wana ujuzi au uwezo sawa na watu wa nchi hizo bali hata wana uwezo mkubwa zaidi lakini hawakupewa fursa ya kuonyesha vipawa vyao. Tunapaswa kutumia vipawa vya wananchi, serikali inapaswa kuwawaunga mkono wavumbuzi ili, Inshallah, Iran iweze kujiundia kila kitu na ijitegemee."

Imam Khomeini MA

Leo tunapoingia mwaka wa 40 tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ile fikra ya 'Kujiamini Taifa' ambayo ilikuwa ikisisitizwa na viongozi pamoja na wanafikra wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya awali ya mapinduzi sasa imegeuka na kuwa sehemu ya sifa za utamaduni wa watu wa Iran. Hivi sasa miongoni mwa watu wa Iran, uhuru na kujitegemea si nara  tu bali ni jambo ambalo limeweza kufikiwa na nchi hii imeshuhudia mafanikio makubwa katika sekta zote za maisha ya wananchi kutokana na kujiamini.

Moja ya sekta muhimu zaidi ambayo tumeshuhudia uhuru, kujitegemea na kujiamini taifa ni sekta ya sayansi na elimu. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanalenga kujibu matakwa ya kihistoria ya taifa la Iran  ambayo ni kuhakikisha nchi hii inafikia kiwango cha juu cha ustawi na maendeleo na hayo hayawezekani isipokuwa kwa kutegemea elimu na uwezo wa ndani ya nchi ulio miongoni mwa vijana na wasomi wa nchi. Imam Khomeini MA,kama muasisi na kiongozi wa Mapinduzi daima alikuwa akisisitiza kuwa sayansi na elimu katika nchi ni kati ya malengo muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu. Imam alikuwa akiamini kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu yanaweza kufikia malengo yake mengine hasa uhuru wa kisiasa, kiuchumi na kifikra iwapo tu jamii itakuwa imejizatiti kwa silaha ya elimu ya juu na sayansi.

Moja ya nukta muhimu zinazoashiria kuimarika elimu nchini Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kupungua au hata kuangamizwa ujinga wa kutojua kusoma na kuandika katika jamii. Mafanikio katika sekta hiyo yamepatikana kufuatia hatua ya Imam Khomeini kuamuru kuanzishwa harakati ya kitaifa ya kukabiliana na kutojua kusoma na kuandika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Iran imeangamiza ujinga wa kutojua kusoma na kuandika

Mbali na sekta hiyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imeweza kupiga hatua kubwa katika kuwashirikisha wanawake katika nyuga mbali mbali za jamii hasa katika sekta za elimu, sayansi na teknolojia. Katika hali ambayo katika miaka ya kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kislamu ni asilimia 35 tu ya wanawake katika jamii ndio waliokuwa wamepata fursa ya kupata masomo ya kiwango cha juu, hivi sasa idadi hiyo ni zaidi ya asilimia 81. Leo wakati tunaadhimisha mwaka wa 39 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wanawake katika jamii sasa wanamiliki elimu na wameweza kukwea daraja za juu za masomo katika nyanja mbali mbali za kisayansi, kisiasa, kiuchumi na kijamii. Wanawake wa Iran hata wameweza kuwapita na kuwatangulia wanaume katika sekta mbali mbali za elimu. Mwaka 1978, kulikuwa na wanawake 50 eflu tu katika vyuo vikuu vya Iran lakini sasa idadi hiyo imefika milioni mbili. Azma ya wasichana na wanawake wa Iran katika kupata elimu ya juu ilishika kasi kiasi kwamba katika miaka ya hivi karibini,kumeshuhudiwa asilimia 56 ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya kiserikali nchini Iran wakiwa ni wasichana au wanawake.

Baada ya kurejea kwa Mola wake Imam Khomeini MA, na katika kipindi cha uongozi wa Ayatullah Khamenei, kumeendelezwa hatu za kuimarisha moyo huo wa kujiamini katika taifa la Iran nukta ambayo imepelekea nchi hii kupata nguvu kielimu na kisayansi duniani.  Ayatullah Khamenei anaamini kuwa moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuimarihsa moyo wa kujiamini sambamba na kukuza vipawa vya vijana. Anasisistiza kuwa jambo hilo ni muhimu hasa katika kuiwezesha nchi isiwe tegemezi kielimu kwa madola ya Magharibi na badala yake nchi iwatemgee vijana wasomi na wenye vipawa kwani jambo hilo pia litachangia kuinua viwango vya elimu na ustawi wa kisayansi. Kuhusiana na kadhia hiyo, Kiongozi Muadhamu katika moja ya hotuba zake alisema: "Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, vijana na wasio kuwa vijana hawakuwa wakipewa fursa ya ubunifu katika nyuga za kisayansi. Lakini Mapinduzi ya Kiislamu yalipelekea kuibuka nguvu kazi huru na yenye kujiamini katika jamii. Mapinduzi ya Kiislamu yameiwezesha nchi hii kustawi kielimu. (Hotuba ya 14/07/82)

Katika kipindi cha uongozi wa Ayatullah Khamenei, Iran imeshuhudia ustawi na kasi kubwa katika nyuga mbali mbali za elimu. Kwa mujibu wa maelezo ya Orodha ya Kimataifa ya Sayansi, ISI, katika kipindi cha miaka 37 kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu (1940-1979), yaani katika zama za utawala wa Mfalme Pahlavi wa Pili,  ni makala 2026 tu za wasomi Wairani zilizochapishwa katika majarida au kuwasilishwa katika makongamano ya kimataifa. Hii ni katika hali ambayo katika kipindi hicho dunia ilishuhudia ustawi wa kasi katika uzalishaji elimu ambapo kiujumla katika kipindi hicho kulichapishwa makala milioni nane kote duniani. Lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kutokana na kasi ya uzalishaji elimu nchini Iran idadi ya makala hizo iliongezeka na kufika zaidi ya makala 245,000 na hivyo kuifanya nafasi ya Iran katika uzalishaji elimu kuongezeka kwa kiwango kikubwa.

Iran imeweza kupata mafanikio hayo ya kielimu katika hali ambayo nchi hii ilikuwa katika vita vya kulazimishwa kwa muda wa miaka minane (1980-1988) na hivyo kuyafanya mazingira ya elimu na utafiti kuwa magumu sana.

Ustawi wa kisaysni Iran

Mbali na kuimarika uzalishaji elimu Iran kwa mtazamo wa viwango na wingi, nchi hii pia imeshuhudia mabadiliko mengi mapya. Moja ya vigezo vya kupima kiwango cha uzalishaji elimu, ni kuangazia ni kiasi gani elimu hiyo inatumika kama marejeo. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, katika hali ambayo kati ya makala 2026 zilizochapishwa Iran kabla ya ushindi wa Mapinduzi ni makala 1178 tu zilizotumika kama marejeo, idadi hii baada ya ushindi wa Mapinduzi imepindukia 9,450.

Kwa maeneno mengine ni kuwa, kiwango cha wasomi wa dunia kutumia makala za kielimu kama marejeo kimeongezeka kwa kiasi kikubwa sana.

Ustawi wa kielimu wa Iran umepata mafanikio makubwa pamoja na kuwa, katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, nchi hii imekuwa chini ya vikwazo vikali zaidi vya kidhalimu vya kisiasa na kiuchumi ambapo madola ya kibeberu, yakiongozwa na Marekani yamekuwa yakiweka vizingiti vingi katika njia ya ustawi wa Iran.

Pamoja na kuwepo njama hizo zote za uvurugaji, tunaweza leo kusema kwa fahari kuwa, katika kipindi hiki cha kuingia mwaka wa 40 tokea yapate ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, nchi hii, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kujiamini kitaifa, imeweza kufika katika kilele cha elimu duniani na ina mustakabali uliojaa matumaini kwa jamii yake na watu wa dunia.

Tags

Feb 08, 2018 08:29 UTC
Maoni