• Vazi la Hijabu na Uhuru wa Mwanamke

Vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu ni miongoni masuala yaliyozusha mjadala mkubwa na mbali na mvuto wake, lakini pia limekabiliwa na mitazamo tofauti katika jamii mbalimbali.

Kulinda vazi la mwanamke na kuchagua mavazi yanayofaa na ya staha ni miongoni mwa masuala muhimu ya kiutamaduni ambayo kila taifa hufanya jitihada za kuhakikisha yanalindwa na yanaakisi thamani za kijamii na kiutamaduni za jamii husika.

Wanawake wa Iran baada ya kuipokea dini ya Uislamu walilikubali vazi la hijabu na daima wamekuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea vazi hilo na kulitambua kuwa ni kinga na ngao inayolinda hadhi, heshima na shakhsia ya mwanamke Mwislamu. 

Uwajibu wa vazi la hijabu kwa mwanamke ni miongoni mwa mambo ya dharura na ya wazi kabisa katika dini ya Uislamu. Qur'ani tukufu, hadithi za Mtume (saw) na maimamu watoharifu katika kizazi chake na fatuwa za wanazuoni na maulamaa wa Kiislamu vyote vimesisitiza na kutilia mkazo uwajibu wa vazi hilo kwa mwanamke Mwislamu. Katika Qur'ani tukufu kuna aya kadhaa zinazowajibisha vazi hilo kwa mwanamke Mwislamu. Kitabu hicho pia kina zaidi ya aya 10 zinazosisitiza udharura na umuhimu wa kulindwa hadhi, utakasifu na heshima ya mwanamke. Kwa mfano aya ya 59 ya Suratul Ahzab inasema:  Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake wa Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu."

 

Hii leo imethibitika kuwa, aina maalumu ya vazi ambalo baadhi wanadai kuwa ni la kulazimishwa na kwamba ni kikwazo cha maendeleo na ustawi wa mwanamke, ni suala la kimaumbile na lina uhusiano wa moja kwa moja na siha na afya ya kinafsi ya mwanadamu. Vazi la hijabu la mwanamke ni kanuni ya maumbile safi na halisi na hapana shaka kuwa, kuasi kanuni ya maumbile kunamnyang'anya mwanamke utambulisho wake. Baadhi ya wataalamu wa elimu ya jamii wanaamini kuwa, vazi la hijabu la mwanamke ni jambo la kimaumbile kwa jamii ya mwanadamu. Mwanafalsafa wa Kifaransa, Charles de Montesquieu ameandika kuwa: Kanuni za maumbile zinahukumu kwamba, mwanamke anapaswa kujisitiri kwa sababu mwanaume ameumbwa akiwa na kiu, na mwanamke amepewa nguvu kubwa zaidi ya kujizuia. Hivyo basi, mgongano baina ya viwili hivyo unaweza kuondolewa kwa vazi la staha na hijabu, na kwa msingi huo mataifa yote duniani yanaamini kuwa, wanawake wanapaswa kuwa na haya na vazi la staha.

Uchunguzi wa wataalamu wa elimu nafsi umebaini kuwa, vazi la mwanamke ni suala la dharura sana katika kukua na kubalehe kwao kinafsi na kisaikilojia. Wale wanaodhani kuwa, tofauti iliyopo baina ya mavazi ya mwanamke na ya mwanaume ni alama za ukosefu wa usawa katika haki za mwanamke na mwanaume na kwamba ni ishara ya kutekwa wanawake wameghafilika na hakika kwamba, vielelezo vya kubalehe kiakili na kinafsi kwa wanaume na wanawake vinatengana na kuachana katika awamu fulani, na tofauti na propaganda zinazotolewa kuhadaa jamii, vazi linalofaa kwa wanawake linafungamana na tofauti za awamu na vipindi mbalimbali vya kukua na kubalehe kwao kiakili na kinafsi na jambo hili lina asili katika maumbile ya mwanadamu. 

Huenda ni kwa sababu hiyo ndiyo maana watu ambao hukumbwa na tatizo la kutojiamini hujielekeza katika tabia ya kujiremba na kujikwatua kupita kiasi na huamini kuwa, uzuri wao wa ndani ya nafsi na batini yao hautoshi. Kinyume chake, wanawake na wanaume wenye uelewa wa juu zaidi au wale wenye nafasi nzuri za kijamii huwa na dhahiri ya kawaida na yenye hadhi na heshima. Jambo la kutilia mkazo hapa ni kwamba, katika dini ya Uislamu kumesisitizwa kuwa, mwanamke ndani ya familia anapaswa kupewa mazingatio sana na mumewe na kutumia na vilevile kudhihirisha urembo, umaridadi na vivutio vyake vyote ambavyo ni vya dharura katika maisha ya ndoa, kwa ajili ya mumewe. Suala hili linaashiriwa katika aya ya 55 ya Suratul Ahzab inayowaruhusu wanawake kudhihiri wakiwa bila ya vazi la hijabu na watu wa familia kama baba, mume, watoto na kadhalika.

 

Hata hivyo mwanamke huyu huyu napoingia katika jamii huachana na ile sifa yake ya kijinsia na kudhihiri kama mwanadamu mwenye hadhi na heshima zote za kibinadamu katika nyanja mbalimbali. Hivyo vazi la hijabu lililofaradhishwa na Uislamu kwa ajili ya mwanamke linamuwezesha kuingia vyema katika medani na masuala ya jamii sambamba na kulinda utukufu na heshima yake. Inatupasa kuelewa kwamba, kama Uislamu usingeruhusu kushiriki mwanamke katika masuala ya kijamii basi kusingekuwepo haja ya kuainisha hijabu na mipaka baina ya jinsia mbili za kike na kiume. Hivyo basi, vazi la hijabu ni wenzo unaomuwezesha mwanamke kushiriki katika masuala ya kijamii kwa njia salama na sahihi. Muziki

أَکْرِمْ نَفْسَکَ عَنْ کُلِّ دَنِیة وَإِنْ سَاقَتْکَ إِلَی الرَّغَائِبِ، فَإِنَّکَ لَنْ تَعْتَاضَ بِمَا تَبْذُلُ مِنْ نَفْسِکَ عِوَضاً. وَلاَ تَکُنْ عَبْدَ غَیرِکَ وَقَدْ جَعَلَکَ اللهُ حُرّاً.

Kabla ya kuzungumzia uhusiano uliopo baina ya vazi la hijabu na uhuru inatupasa kwanza tusome kipande kidogo cha wasia wa Imam Ali bin Abi Twalib kwa mwanaye Hassan al Mujtabaa (as) pale alipomwambia: "Epusha nafsi yako na mambo machafu (mauvu na maasi) japokuwa yatakufikisha katika matakwa yako ya kinafsi, kwa sababu kamwe mambo hayo (maasi na mambo machafu) hayawezi kufidia unachokipoteza katika nafsi yako. Usiwe mtumwa wa mtu mwingine ilhali Mwenyezi Mungu amekuumba ukiwa huru." 

Kwa msingi huo ni vyema kwa mwanadamu kufuata irada na matakwa ya Mola wake Muumba na kuuona uhuru wake katika mipaka ya matakwa ya Mwenyezi Mungu.

Kwa kuwa katika dini ya Uislamu, sheria zote zimewekwa kwa msingi wa itikadi ya Tauhidi na maadili mema, uhuru wa mwanadamu umewekwa katika mipaka maalumu ya sheria na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Mwanadamu ni kiumbe huru na chenye hiari ya kutumia haki zote zilizoainishwa katika sharia. Kwa mfano tu miongoni mwa kanuni za sharia ni kwamba, mwanadamu anaweza kupiga hatua yoyote anayotaka katika medani ya elimu na maarifa na ana uhuru kamili katika suala hilo. Si hayo tu bali utawala wa Kiislamu unawajibika kumtayarishia mazingira bora zaidi ya kutumia haki hiyo. Hata hivyo kanuni hiyo hiyo imeweka mipaka ambayo kwa hakika si mipaka bali ni kinga na ngao inayoizuia jamii kutumbukia katika shangalabaghala, kukosa mwelekeo na kuchupa mipaka. Mfano wake ni aina ya vazi la mwanaume na mwanamke katika sheria ya Uislamu ambalo limeainishwa kwa ajili ya kudhamini maisha bora zaidi ya kijamii na kuikinga jamii na baadhi ya majanga na maafa ya kimaadili.

Suala hili halihusu dini ya Uislamu pekee. Hii leo katika baadhi ya nchi zilizostaarabika pia kuwemekwa sheria na kanuni zinazobana au kuweka mipaka ya aina ya mavazi, mienendo na kadhalika. Kwa mfano pale mwanaume anapotoka nje katika hadhara ya umma akiwa na vazi la kulalia (night dress) au pajama hukamatwa na polisi kwa sababu kitendo hicho kinapingana na adabu na taratibu za kijamii. Suala hili katika mtazamo wa elmu jamii, si dhidi ya uhuru, utukufu na hadhi ya mwanadamu na wala si dhulma na kinyume cha busara. Naam, vazi na kujisitiri kwa mwanamke katika mipaka iliyoainishwa na Uislamu humpa hadhi na heshima na kumlinda na chokochoko za watu wasio na maadili mema.

Image Caption

Kwa msingi huo uhuru wa mwanamke unatimia kwa kulea na kustawisha uwezo wake wa kifikra na kiakili, kupeleka juu kiwango cha elimu na maarifa yake, na kutekeleza majukumu yake na kushirikishwa katika masuala ya kijamii kwa njia sahihi na za kimantiki. Vazi la hijabu ya Kiislamu ambalo limefaradhishwa kwa ajili ya kulinda hadhi ya wanawake, kuimarisha takwa na uchamungu na kumsaidia mwanamke katika kulinda maadili mema yake na ya jamii, si tu kwamba halibani uhuru wa wanawake, bali pia linawawezesha kushiriki vyema zaidi katika shughuli mbalimbali za kimalezi na kijamii kama mwandamu mwenye hadhi sawa na mwenzake wa kiume na si kama jinsia ya kike.

Nukta hii inashuhudiwa vyema kwa mwanamke Mwislamu wa Iran ambaye amepata hadhi na heshima kubwa hususan baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kupiga hatua kubwa za maendeleo katika nyanja mbalimbali sambamba na kulinda vazi lake la hijabu ya Kiislamu. Maendeleo ya kielimu ya wanawake wa Iran hayawezi kufumbiwa macho. Kiwango cha wanachuo wa kike nchini Iran kimeongeza katika nyanja zote na kuzidi asilimia 60. Ongezeko la asimilia 30 ya madaktari wa kike, ustawi wa asilimia 40 ya madaktari bingwa na la asilimia 99 ya wataalamu wanawake ni miongoni mwa maendeleo yasiyo na kifani ya wanawake wa Iran katika sekta ya tiba pekee. Huu ni mfano mdogo tu wa maendeleo ya wanawake Waislamu wa Iran ambao wamekhitari kuvaa vazi la staha na stara la hijabu ya Kiislamu. Suala hili kwa hakika linaonesha kwamba, vazi la hijabu si kizuizi wala haliwawekei mipaka na vigingi wanawake, bali ni ngao na kinga inayolinda hadhi, heshima na utakasifu wa wao.      

Tags

Mar 03, 2018 10:19 UTC
Maoni