• Ummul Banin, Mama wa Mashahidi wa Karbala

Siku ya tarehe 13 Jamadithani kwa mwaka wa Hijria Qamaria inakumbusha tukio la kuzama kwa jua la mke mwema na mwaminifu, mama mwenye huruma aliyekusanya sifa zote njema za kimaadili, imani, ukamilifu wa kiroho, subira na uvumilivu, elimu na maarifa na kadhalika na kuwa kigezo chema cha kuigwa cha mwanamke kamili wa Kiislamu.

Jina la mwanamke huyo ni Fatima aliyepewa kuniya ya Ummul Banin. Baba yake ni Hizam bin Khalid kutoka kabila la Bani Kilab na mama yake alikuwa Thumamah. Inakadiriwa kuwa alizaliwa mwaka wa tano baada ya hijra ya Mtume kutoka Makkah kwenda Madina. Familia na kabila lake lililikuwa la watu mashujaa, wakarimu, wenye maadili mema, wenye watu wenye hadhi ya kijamii na adhimu na walitambuliwa kuwa vinara wa Waarabu baada ya kabila la Quraish. Allamah Sayyid Muhsin Amiin, mwanafasihi mashuhuri na mwandishi wa wasifu wa karne ya 13 Hijria anasema: Ummul Banin (as) alikuwa malenga hodari na alizaliwa katika familia mashuhuri na ya watu mashujaa. Aqiil bin Abi Twalib aliyekuwa mtaalamu wa nasaba za Wanaarabu alimwambia Imam Ali (as) kwamba: "Kati ya Waarabu wote ni muhali kupata watu mashujaa zaidi kuliko ukoo wa Fatima binti Hizam." 

Baada ya kufa shahidi Bibi Fatima bint Muhammad (saw), Ali bin Abi Twalib alimuomba kaka yake, Aqiil ambaye alikuwa gwiji na mtaalamu na nasaba amtafutie mke mwema kutoka kizazi cha watu mashujaa atakayemzaliwa watoto mashujaa. Aqiil alimwelekeza kwa Faitma al Kilabiyya ambaye kabila lake la Banii Kilab halikuwa na mfano katika ushujaa. Imam Ali pia alikubali ushauri wa kaka yake kisha akamtuma kwa baba yake Ummul Banin. Hizam au Huzam ambaye alikuwa maarufu sana kwa kuwapenda na kuwakirimu wageni alimkaribisha na kumkirimu kwa kumchinjia mnyama. Ada ya Waarabu ilikuwa ni kumkaribisha mgeni kwa siku tatu ukimkirimu bila ya kumwambia lolote na kumuuliza haja yake baada ya kipindi hicho. Familia ya Fatima bint Huzam iliyokuwa ikiishi nje ya Madina ilitekeleza kikamilifu ada hiyo na katika siku ya nne ilitaka kujua sababu ya safari ya Aqiil kwa heshima na taadhima. Aqiil alisema: "Nimekuja kumchumbia binti yenu, Fatima kwa ajili ya Ali bin Abi Twalib." Hizam ambaye hakutarajia kabisa suala hilo alipigwa na butwaa na mshangao na kujibu kwa kusema: "Nasaba sharifu na tukufu iliyoje na familia adhimu yenye utukufu! Hata hivyo Aqiil! mwanamke wa kijijini kama mwanangu Fatima si laiki ya mtu adhimu kama Ali bin Abi Twalib.

Baada ya kusikia maneo hayo Aqiil alisema: Ali anayajua haya unayoyasema lakini pamoja na hayo anataka kumuoa Fatima. Baba yake Ummul Banin ambaye hakujua aseme nini, alimuomba Aqiil ampe muda ili apate kuzungumza na mama wa binti yake, Thumama binti Suhail na Fatima mwenyewe.         

Alimwambia: Wanawake wanajua vyema zaidi hali za kiroho na kinafsi za mabinti zao na vilevile maslahi yao."

Mke wake ambaye alikuwa mpenzi mkubwa wa kizazi cha Mtume Muhammad (saw) alijibu bila ya kusita kwamba: "Ewe Hizam! Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba nimemlea vizuri binti yangu huyu na ninamuomba Mwenyezi Mungu mtukufu ampe saada na ufanisi na amfanye mke mwema kwa Ali bin Abi Twalib. Muoze Fatima kwa Ali."     

Siku ya kwanza Fatima binti Huzam alipoingia nyumbani kwa Imam Ali (as), Hassan na Hussein walikuwa wagonjwa kitandani. Baada tu ya kuingia nyumbani mwanamke huyo mwema alikwenda moja kwa moja kwa wajukuu hao wawili wa Mtume (saw) na kuanza kuwajulia hali na kuwashughulikia kama mama mwenye huruma kwa watoto wake. Katika siku hizo za mwanzoni, mwanamke huyo mwema alimuomba Imam Ali (as) awe anamuita kwa kuniya yake ya Ummul Banin badala ya jina lake la Fatima ili watoto wa Fatimatu Zahra, binti wa Mtume, wasipate machungu ya kumkumbuka mama yao kwa kusikia jina hilo mara kwa mara. Ummul Banin alitaka kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Bibi Fatima (as) mbele ya watoto wake, mama ambaye aliaga dunia akiwa bado kijana na kuwaacha wanaye wachanga katika hali ya uyatima wa kutokuwa na mama. Watoto wa Bibi Fatima binti Muhammad (saw) walimuona mama yao katika mwanamke huyo mwema na kupungukiwa na majonzi ya kutokuwa na mama kutokana na upendo, huruma na mwenendo aali na mwanamke huyo mchamungu.

Daima Ummul Banin aliwatanguliza wana wa Fatima na kuwafadhilisha kuliko watoto wake mwenyewe na aliwapenda sana kuliko wanaye wa kuzaa. Aliliona suala hilo la kuwapenda watoto wa Sayyida Fatima kuwa ni wajibu wake wa kiimani na kidini uloamrishwa na Mwenyezi Mungu katika aya ya 23 ya Suratu Shura pale aliposema: Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi kwa ndugu zangu wa karibu. Na anayefanya wema tutamzidishia wema. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye shukrani. 

Mwanahistoria wa karne ya 10 Hijria, Zainuddin A'mili ameandika kwamba: Ummul Banin alikuwa mwanamke mwenye maarifa na utukufu mkubwa. Aliwaashiki Ahlubaiti wa Mtume (saw) na alisabilia maisha yake kwa ajili ya kuwatumikia. Vilevile Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) walimpa nafasi ya juu na heshima maalumu", mwisho wa kunukuu.

Matunda ya masiha ya ndoa ya Ummul Banin na Imam Ali bin Abi Twalib (as) yalikuwa watoto wanne wa kiume waliokuwa na majina ya Abbas, maarufu kwa lakabu ya Qamaru Banii Hashim, Abdullah, Ja'far na Uthman na wote waliuawa katika mapigano ya Karbala wakiwa pamoja na kaka yao, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). Kizazi cha Ummul Banin (as) kilibakia kupitia mtoto wa Hadhrat Abul Fadhl Abbas (as) yaani Ubaidullah. Kutokana na kuuawa shahidi watoto wake wote wanne katika siku moja ya Ashuraa huko Karbala, Ummul Banin amepewa fahari ya lakabu ya "Mama wa Mashahidi" na hivyo kupata fahari ya kuwa mke wa shahidi na mama wa mashahidi waliouawa katika kutetea dini ya Allah (SW).

السلام علیک یا ام البنین

Wanahistoria wanasema: Wakati Ummul Banin alipomuona mjumbe wa Imam Ali bin Hussein Zainul Abidin (as) aliyekuwa amefika Madina kutoa habari ya kuuawa shahidi Imam Hussein na wafuasi wake katika ardhi ya Karbala alimwambia: "Nipe habari za Hussein." Mjumbe huyo alijibu kwa kusema: Mwenyezi Mungu akupe subira na uvumilivu. Mwanao Abbas ameuawa. Ummul Banin alisema: Nipe habari za Hussein. Mjumbe wa Imam Sajjad alimwambia kuwa watoto wake wote wanne wameuawa. Ummul Banin alikariri tena takwa lake akitaka kujua habari za Hussein kwanza kabla ya watoto wake wa kuzaa. Alisema: Watoto wangu na kila kilichoko dunia kiwe fidia na mhanga wa Abu Abdillah Hussein. Niambie kwanza habari za Hussein. Wakati mjumbe huyo alipotoa habari ya kuuliwa shahidi Imam Hussein (as) Bibi Ummul Banin alipiga mayowe na kusema: Umekata mshipa wa moyo wangu ewe Bashir! Bibi huyo mwema na mchamungu alilia sana kwa uchungu na maumivu.   

یا ام البنین

Miongoni mwa sifa aali za Ummul Banin, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, ni kipaji chake kikubwa katika taaluma ya fasihi kilichodhihiri vyema zaidi katika utungaji wa mashairi. Kabila la Bani Kilab ni mashuhuri sana kwa kuwa na malenga wakubwa na watajika, na Waarabu walikuwa wakiwategemea sana katika taaluma hiyo. Watu wa kabila la Bani Kilab walikuwa vinara na magwiji wa fasihi na malenga wa Kiarabu. Bibi Fatima Ummul Banin alikulia katika kabila hilo na kupata elimu na maarifa ya lugha na utunzi wa mashairi. Miongoni mwa mashairi ya mtukufu huyo ni lile alilotunga na kulisoma baada ya kuuliwa watoto wake katika medani ya Karbala. Wanahistoria wanasema Ummul Banin (as) aliumizwa sana na mauaji ya Karbala kiasi kwamba kila siku alikuwa akishika mkono wa mjukuu wake mchanga, Ubaidullah mwana wa Abul Fadhl Abbas na kwenda naye katika makaburi ya Baqii mjini Madina alikokuwa akiketi na kufanya kilio cha kuwakumbuka mashujaa hao. Alihuisha jina la mashahidi wa Karbala na kufichua uovu na dhulma za Bani Umayyah kwa mashairi yake.  

Kaburi la Ummul Banin, Madina

Hatimaye bibi huyo mwema aliyekuwa ashiki na hadimu wa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) aliaga dunia katika siku ya tarehe 13 Jamadithani mwaka 64 Hijria. Mwili wake mtukufu ulizikwa katika makaburi ya Baqii yanayopakana na Msikiti wa Mtume Muhammad (saw) mjini Madina. Mwenyezi Mungu SW aiweke roho yake peponi na Mtume na Ahlibaiti zake watukufu na aturuzuku shifaa na maombezi yao. Inna lillah wainna ilayhi rajiuun. 

Mar 03, 2018 10:30 UTC
Maoni