• Kuzaliwa Mbora wa Wanawake, Bibi Fatima al Zahra (as)

Historia na vitabu vya hadithi vinasimulia kwamba, wakati Mtume Muhammad (saw) alipokuwa akisubiri wahyi na ufunuo kutoka kwa Mola wake, malaika Jibrail aliteremka kwake na kumwambia: Ewe Muhammad! Mwenyezi Mungu Mtukufu anakupa salamu na anakuamuru ujitenge na Khadija kwa muda wa siku arubaini.

Mtume (saw) alijitenga na mke wake, Bibi Khadija akitekeleza amri hiyo ya Mwenyezi Mungu. Alikuwa akifunga swaumu mchana na kufanya ibada nyakati za usiku katika kipindi hicho cha siku 40. Wakati huo alimtuma swahaba wake mwema, Ammar bin Yasir kwa Bibi Khadija ili amwambie kwamba, amejitenga naye kwa amri ya Mwenyezi Mungu na si kutokana na jambo lolote jingine. 

Baada ya kupita siku 40 Malaika Jibrilu aliteremka tena kwa Mtume Muhammad (saw) na mara hii alimpatia mtukufu huyo tunda la tufaha na kumwambia: Yaa Muhammad! Mola wako Mlezi anakupa salamu na amekutumia hadiya na zawadi hii kutoka peponi. Mtume (saw) alikula tunda hilo na kisha akarejea nyumbani kwa Bibi Khadija amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake. Bibi Khadija alipoamka alianza kuhisi nuru ya Fatima.

Siku moja Mtume (saw) alipoingia nyumbani kwa Bibi Khadija alimuona kana kwamba anazungumza na mtu mwingine. Alimuuliza: Unazungumza na nani? Bibi Khadija alisema: Janini aliyeko tumboni mwangu anazungumza na mimi na kuniliwaza. Baadaye Malaika Jibrilu aliteremka kwa Mtume (saw) na kumwambia kwamba: "Mwambie Khadija kwamba mtoto aliyeko tumboni mwake ni wa kike, na kizazi chako wewe kitatokana na yeye." 

 

 Tarehe 20 Jamadithani mwaka wa tano baada ya Mtume Kubaathiwa na kupewa utume, Bibi Khadija amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake alihisi uchungu mkali. Alimtuma hadimu wake akamwitie wanawake wa Kikuraishi ili wamsaidie katika machungu za uzazi; hata hivyo wanawake hao walikataa na kusema: Ulikataa matakwa yetu na ukakubali kuolewa na yatima wa Abu Twalib ambaye hakuwa na mali wala utajiri. Bibi Khadija alibakie peke yake akizongwa na machungu ya uzazi na ghafla wanawake wanne warefu waliingia nyumbani kwake. Awali aliogopa na kutaka kujua walikuwa kina nani? Sara mke wa Nabii Ibrahim Khalilullah, Asia, mke wa Firauni, Maryam binti Imran mama yake Nabii Issa, na Kulthum, dada yake Nabii Mussa, Kalimullah waliketi kandokando ya Bibi Khadija na kumsaidia katika machungu ya uzazi na kujifungua. 

Siku hiyo ya tarehe 20 Jamadithani Bibi Khadija alijifungua mtoto wa kike ambaye nuru yake ilitanda nyumba yote ya Mtume (saw). Mtoto huyo alioshwa kwa maji ya Kauthar na kisha akawekwa kwenye kitambaa cheupe kuliko maziwa na chenye harufu nzuri kuliko ya miski.

Ulipofika wakati wa kumpa jina mtoto huyo malaika wa Mwenyezi Mungu aliteremka kwa Nabii Muhammad (saw) na kumwambia: Mpe jina la Fatima. Alikuwa mtoto wa kwanza kupewa jina la Fatima baada ya kudhihiri Uislamu ambaye kuja kwake kulisahihisha ada na mtazamo wa kijahilia kuhusu mwanamke.

Jambo linalompa thamani na hadhi mwanadamu na kuelekeza harakati na misimamo yake ni fikra na itikadi zake, na viwili hivi huongozwa na kupewa mwelekeo na elimu na maarifa. Vilevile elimu na maarifa huwa na faida pale inapoambata na imani. Fatima (as) binti wa Mtume wetu Muhammad (saw) alikusanya yote hayo kwa pamoja. Alikuwa mwanamke aliyekusanya thamani za kibinadamu na kimaadili, mwenye imani, ikhlasi na uchamungu. Aliashiki ibada na kujipinda katika kumtii Mola Muumba na daima alikuwa akisema: "Ladha ninayoipata katika kumwamudu Mwenyezi Mungu inanizuia kuomba kitu kingine chochote. Sina haja na takwa jingine ghairi ya kutazama jamala na utukufu wa Mola Muumba."

Miongoni mwa majina mashuhuri ya mtukufu huyo ni Zahra ambalo lina maana ya nuru inayong'aa. Imam Ja'faru Swadiq (as) aliulizwa: Kwa nini Fatima alipewa jina la Zahra? Alisema: Kwa sababu wakati wowote Fatima alipokuwa akisimama kwenye mihrabu na kujishughulisha na ibada, nuru yake ilikuwa ikiangazia wakazi wa mbinguni, mithili ya nyota zinavyowaangazia wakazi wa ardhini..".

Elimu na maarifa ya Bibi Fatima (as) ilikuwa na mfungamano wa moja kwa moja na elimu ya baba na mwalimu wake, yaani Mtume Muhammad (saw). Alikuwa akifafanua hadithi za Mtume na imenukuliwa kwamba, alikuwa akiwafundisha wanawake wa Kikuraishi maarifa ya Kiislamu. Miongoni mwa mifano hai ya elimu na maarifa ya Bibi Fatima ni hotuba ya kihistoria aliyoitoa katika Msikiti wa Mtume mjini Madina mbele ya khalifa wa wakati huo siku chache baada ya Mtume (saw) kuaga dunia. Imenukuliwa kwamba, hadimu na mwanafunzi wa Bibi Fatima (as) yaani Fidha Mwenyezi Mungu amrehemu, hakuzungumza kwa kipindi cha karibu miaka 20 isipokuwa kwa kutumia aya za Qur'ani tukufu.

Fatima (as) alikuwa mwalimu na kigezo bora cha kuigwa katika mwenendo na matendo. Alikuwa kipenzi na mahbuba wa Mtume (saw) na sehemu ya mwili wake kama ilivyopokewa katika hadithi na historia ya Kiislamu. Wakati wowote Mtume (saw) alipomtembelea, Fatima alinyanyuka na kusimama kuonesha heshima na taadhima kwa mtukufu huyo, na Mtume wa Mwenyezi Mungu alifanya hivyo hivyo na kumkalisha Fatima mahala pake wakati Bibi Fatima alipomtembelea. Imam Ruhullah Khomeini anasema: "Historia ya Uislamu ina vielelezo tosha vya jinsi Mtume wa Mwenyezi Mungu alivyokuwa akimpa heshima kubwa mtoto huyo sharifu na mwema, yaani Bibi Fatima ili kuonesha kwamba, mwanamke ana hadhi makhsusi katika jamii ambayo kama si juu ya ile ya mwanaume basi kwa uchache haiko chini yake".

Sura ya Bibi Fatimatu Zahra (as) katika Qur'ani tukufu pia inaonesha picha aali na isiyo na kifani. Suratul Kauthar ni kielelezo kikubwa zaidi cha adhama na utukufu wa Bibi Fatima katika kitabu hicho kitukufu cha Mwenyezi Mungu. Baada ya kuzaliwa kwa mtukufu huyo, Mwenyezi Mungu SW alimwambia Mtume wake kwamba: Hakika sisi tumekupa Kauthar kwa maana ya kheri nyingi na kwamba kizazi chake kamwe hakitakatika kama walivyokuwa wakitamani makafiri na washirikina. Maulama na wanazuoni wa Kiislamu wametaja aya nyingi za Qur'ani zilizoteremka kutaja mema na nafasi adhimu ya Fatima kama aya maarufu ya Mubahala, Aya ya Tat-hiir, aya kadhaa za Suratu Dahr na kadhalika. Katika tafsiri yake ya Qur'ani, mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Jalaluddin Suyuti amenukuu karibu hadithi 20 zilizopokewa kwa sanadi na wapokezi tofauti kuhusu aya ya 33 ya Suratul Ahzab inayosema: Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara", kwamba: "Ahlulbait na Watu wa Nyumba ya Mtume wanaokusudiwa katika aya hii ni Mtume mwenyewe, Ali bin Abi Twalib, Fatima, Hassan na Hussein peke yao."  

Aya hii ni mashuhuri kwa jina la Ayatu Tat-hiir na iliteremshwa kwa Mtume (saw) akiwa nyumbani kwa mkewe mwema na mchamungu, Ummu Salama radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Imam Ahmad bin Hanbal, kiongozi wa madhehebu ya Hanbali amenukuu kutoka kwa mke wa Mtume (saw), Ummu Salama kwamba: "Wakati aya hiyo ilipoteremshwa, Mtume wa Mwenyezi Mungu alimwambia Fatima: Niitie mume wako na watoto wako wawili, yaani Hassan na Hussein. Tulipokwenda kwa Mtume (saw) alichukua kitambaa na kuwafunika nacho kisha akaweka mkono wake mtukufu juu yao na kusema: Mola wangu Mlezi! Hawa ndio Aali Muhammad. Teremsha salamu na baraka zako kwa Muhammad na Aali zake." Ummu Salama anasema: Niliinua upande mmoja wa kitambaa hicho nikitaka kuingia ndani yake na kujiunga nao lakini Mtume (saw) hakuniruhusu na aliniambia kwa heshima kwamba: Wewe utakuwa katika kheri lakini si miongoni mwa Aali Muhammad.

Ibn Hajar al Haithami pia anakiri kwamba, wafasiri wengi wa Qur'ani tukufu wanaamini kuwa, Ayatu Tat-hiir iliteremka kwa ajili ya Ali, Fatima, Hassan na Hussein.  

Maisha ya kawaida na ya watu wa chini, zuhudi na uchamungu zilikuwa miongoni mwa sifa kuu za maisha ya Bibi Fatima Zahra. Aliishi hivyo alipokuwa nyumbani kwa baba yake na hata baada ya kuolewa na Ali bin Abi Twalib. Roho aali na iliyojiepusha na anasa za dunia ilimfanya Mwanafatima awe mbali na dunia na vishawishi vyake. Daima alikuwa akisema: "Katika dunia yenu hii ninapnda zaidi vitu vitatu: Kusoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu yaani Qur'ani, kutazama uso wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na kutoa mali na nilichonacho katika njia ya Mwenyezi Mungu."

Bibi Aisha mke wa Mtume Muhammad (saw) anasimulia kwamba: "Sijawahi kuona mtu anayeshabiana zaidi na Mtume wa Mwewnyezi Mungu katika maneno na mwenendo wake kuliko Fatima. Mapenzi ya baba kwa mwanaye yalikuwa makubwa kiasi kwamba mara zote alipokuwa akimuona alikuwa akisema: Ninanusa harufu ya peponi kutoka kwa Fatima", mwisho wa kunukuu.

Bibi Fatima Zahra (as) alikuwa mfano aali wa mwanamke kamili aliyetumia uwezo wake kwa ajili ya kukwea daraja za juu za ukamilifu. Suala hilo lilimfikisha katika kilele cha taqwa na uchamungu na kutambulishwa na baba yake yaani Nabii Muhammad (saw) kuwa ni mbora wa wanawake wote duniani.

Sala na salamu za Allah zimshukie Bibi Fatima, binti wa Mbora wa Viumbe, mama wa Mabwana wa Vijana wa Peponi Hassan na Hussein na mke wa Simba wa Mwenyezi Mungu na Wasii wa Nabii Muhammad, Ali bin Abi Twalib (as).    

Mar 07, 2018 11:07 UTC
Maoni