Mar 20, 2018 02:24 UTC
  • Nairuzi katika Haram ya Imam Ridha AS, kaskazini mashariki mwa Iran
    Nairuzi katika Haram ya Imam Ridha AS, kaskazini mashariki mwa Iran

Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Jumatano ya tarehe 21 Machi mwaka huu wa 2018 inasadifiana na kuanza mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia.

Ni sherehe za kale na za muda mrefu ambazo matawi yake yameenea katika kona mbalimbali za dunia hadi Afrika Mashariki.

Asili ya sherehe za Mwakakogwa huko Makunduchi visiwani Zanzibar, ni sherehe hizo za Nairuzi za nchini Iran. Mbali na Iran sherehe za Nairuzi hufanyika pia katika nchi za Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kirghizstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar huko Tanzania.

Leo tumeamua wiki hii tuzungumze kwa muhtasari kuhusu historia ya sherehe za mwaka huu mkongwe ambao hivi sasa unafuata Hijra ya Bwana Mtume Muhammad SAW ya kutoka Makka kwenda Madina lakini kwa kutegemea jua na si mwezi na ndio maana ukaitwa mwaka wa Hijria Shamsia. Karibuni.

Wananchi wa Iran katika maadhimisho ya Nairuzi

 

Nairuzi ni sherehe ambayo imedumu toka zama za kale na ingali inaadhimishwa. Kwa mujibu wa aghalabu ya ngano za kale na simulizi na mapokezi ya kihistoria kuhusu Nairuzi, sikukuu hii ilianzishwa na mfalme Jamshid katika silisila ya tawala za Pishdadi. Jamshid alikuwa mfalme wa nne katika silisila ya watawala wa Pishdadi na anatambuliwa kama muasisi wa sikukuu ya Nairuzi.

Jamshid alikuwa mfalme aliyependwa sana na wananchi. Inasimuliwa kuwa katika siku zake, nchi ilifika katika kilele cha utajiri wa mali. Ferdowsi, malenga maarufu wa Iran wa tungo za hamasa, katika simulizi yake kuhusu namna zilivyoanza sherehe za Nairuzi anasema, wakati neema zilipokuwa nyingi katika nchi, Mfalme Jamshid aliwakusanya maafisa wote wa serikali na kuwashukuru.

Jamshid aliwashukuru na kuwaenzi waliofanya kazi vizuri tarehe Mosi Farvardin ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa Hijria Shamsia. Aliitaja siku hiyo kuwa ni siku ya Nairuzi yaani siku mpya.

Pamoja na kwamba hakuna nyaraka kamili kuhusu historia ya Nairuzi, lakini ni jambo lisilo na shaka kuwa Nairuzi ni sherehe ya kale na ilikuwa ikisherehekewa katika ardhi ya Iran hata kabla ya kuwasili kaumu ya Arya. Kwa mujibu wa mtafiti Muirani, Mehrdad Bahar, Nairuzi ni mila na desturi ya kale ambayo ilikuwepo milenia ya tatu kabla ya Miladia (Kuzaliwa Nabii Issa AS). Anaandika hivi:

'Sherehe hizo zilikuwa zikiadhimishwa na makabila ya asili ya watu wanaohamahama nchini Iran.' Baadhi ya riwaya za kihistoria zinasema kuwa, Nairuzi iliingia Iran mwaka 538 kabla ya kuzaliwa Masih Isa AS baada ya Kourosh kuliteka eneo la Babel. Riwaya hizo zinasema kuwa katika kukaribisha Nairuzi, Kourosh wa Pili alikuwa na mpango maalumu wa kuboresha maisha ya askari wake, kusafisha na kudumisha usafi katika maeneo ya umma na nyumba binafsi sambamba na kuwaachilia huru wafungwa.

Sherehe za Nairuzi hufanyika katika msimu bora kabisa wa mazingira

 

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika maandishi yaliyopatikana kwenye majabali katika zama za Wakhamaneshi kwenye karne ya 6 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa AS, watu wa zama hizo walikuwa wakifahamu vyema mila na desturi za Nairuzi. Wafalme wa silisila ya Wakhamaneshi walikuwa wakifanya makaribisho maalumu ya kuipokea Nairuzi katika eneo maalumu la ibada lililojulikana kama Takht-e Jamshid yaani Persepolis huko Shiraz, Iran.

Kwenye sherehe hizo maalumu wafalme walikuwa wakiwakaribisha watu kutoka kaumu na mataifa mbali mbali. Kila mwaka wawakilishi wa mataifa mbalimbali duniani, wakiwa wamevaa nguo zao za kienyeji na kitaifa walikuwa wakifika huko Takht-e Jamshid na kusherehekea sikukuu ya Nairuzi. Katika maadhimisho hayo, walikuwa wakimletea mfalme wa Iran zawadi zenye thamani kubwa.

Nyaraka za historia zinaonyesha kuwa, mwaka wa 416 kabla ya kuzaliwa Masih Isa AS, Mfalme Dariush wa Kwanza alitengeneza sarafu za dhahabu kwa mnasaba wa Nairuzi. Sehemu moja ya sarafu hiyo ina taswira ya askari akirusha mshale. Katika zama za watawala wa Waashkani na Wassasani kuanzia karne ya 247 BC hadi karne ya 650 Miladia kuliendelea kufanyika sherehe za Nairuzi ambazo ziliadhimishwa kwa siku kadhaa mfululizo. Katika zama za Waashkani sikukuu hii ilikuwa na duru mbili yaani Nairuzi ndogo na Nairuzi Kubwa. Katika zama za Wasassani, Nairuzi ilisherehekewa kwa sura ya Nairuzi ya Umma na Nairuzi Maalumu.

Nairuzi ya umma ilidumu kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe Mosi Farvardin na Nairuzi Maalumu ilisherehekewa katika siku ya sita ya Farvardin ambapo kulifanyika sherehe kubwa. Kwenye siku tano za kwanza za Nairuzi kulikuwa na karamu kwa ajili ya umma ambapo pia wananchi walipata fursa ya kutoa maombi yao. Katika siku ya sita ambayo ilikuwa ndio Nairuzi kubwa kulifanyika sherehe maalumu ya mfalme na watu wa karibu naye. Tunaweza kusema kwamba sherehe hiyo ilikuwa maalumu katika kasri la utawala.

Sherehe za Nairuzi ni za kimataifa, hazihusiani na taifa la Iran tu

 

Baada ya kuingia Uislamu katika ardhi ya Iran, Wairani Waislamu waliendelea kuadhimisha sikukuu ya Nairuzi lakini kwa kuzingatia mafundisho, mila na desturi za Kiislamu. Katika zama za utawala wa Waseljuki walioanza kutawala Iran katika karne ya 10 Miladia kulifanyika mabadiliko katika kalenda kuhusu mwaka unaofuata jua yaani mwaka wa Shamsia.

Mwaka 467 Hijria Qamaria sawa na mwaka 1,074 Miladia, Jalaluddin Malik Shah Seljuki aliwataka wanahisabati na wataalamu wa falaki yaani elimu ya nyota akiwemo Omar Khayyam Nishaburi wafanye utafiti juu ya namna ya kuifanyia marekebisho kalenda iliyokuwepo wakati huo. Magwiji hao wa Kiirani waliamua siku ya kwanza ya Nairuzi isadifiane na siku ya kwanza ya msimu wa machipuo na ndio maana kalenda ya Iran ikapewa pia jina la 'Kalenda ya Jalali' au 'Maliki'.

Kimsingi ni kuwa, kalenda hii ilienda sambamba na kalenda ya kimaumbile kikamilifu. Kwa hivyo si tu kuwa Nairuzi iko katika siku ya awali ya msimu wa machipuo, bali pia kalenda ya Jalali au Hijria Shamsia inaenda sambamba na misimu yote ya kimaumbile katika eneo hili. Mwaka wa kalenda ya Jalali ni makini sana ikilinganishwa na Kalenda ya Miladia (Gregorian) ambayo baada ya kila miaka elfu 10 huwa na hitilafu ya takribani siku tatu.

Baada ya kudhihiri Uislamu nchini Iran hasa katika zama za utawala wa Wassafavi yaani karne za 10 na 11 Hijria Qamaria au karne ya 16 Miladia, sherehe za Nairuzi zilichanganywa na mila na desturi za Kiislamu na hivyo kupata uhai na ufahamu mpya. Aidha kuna riwaya za Kiislamu kuhusu umuhimu wa sikukuu ya Nairuzi jambo ambalo limefanya sherehe hizo zipate umuhimu zaidi hasa miongoni mwa Waislamu wa madhehebu ya Kishia.

Kwa mujibu wa riwaya za Maulamaa wa Kishia, Nairuzi ni siku tukufu. Imam Ja'afar Sadiq AS amenukuliwa akisema kuwa Nairuzi ni siku ya furaha na iliyobarikiwa na kwamba Nabii Adam AS aliumbwa katika siku kama hii. Aidha kwa mujibu wa riwaya nyingine, tunasoma kuwa katika siku inayosadifiana na hii yaani mwaka wa 10 Hijria, Mtume Muhammad SAW, akiwa katika eneo lijulikanalo kama Ghadir Khum, alimtangaza Imam Ali AS kuwa mtu atakayechukua uongozi baada yake kama Khalifa wa Waislamu. Kwa msingi huo Waislamu wa Iran wanaitambua Nairuzi kama siku yenye furaha na baraka na wameiambatanisha na utamaduni wa Kiislamu.

Mwaka 2009 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni UNESCO liliitangaza na kuisajili Nairuzi kama turathi ya kimaanawi duniani. Aidha Mwaka 2010 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin yaani Machi 21 kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nairuzi.

Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nairuzi kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena maumbile. Kwa mujibu wa tovuti ya Umoja wa Mataifa, sikukuu ya Nairuzi hueneza thamani za amani na mshikamano wa vizazi katika familia sambamba na kuleta maelewano na ujirani mwema na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kudumisha urafiki baina ya watu wa jamii mbali mbali. Katika matini ya kuidhinishwa Nairuzi kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imeandikwa hivi: "Sherehe za Nairuzi zina mizizi ya Kiirani ya zaidi ya miaka 3,000 iliyopita na leo zaidi ya watu milioni 300 huadhimisha siku hii."

Mazingira ya kupendeza yanayokuwepo wakati wa sherehe za Nairuzi

 

Mpenzi msikilizaji, baada ya kukuleteeni historia hiyo fupi ya sherehe za Nairuzi ambapo hata sherehe za Mwakakogwa huko visiwani Zanzibar zinatokana na sherehe hizo hizo za Nairuzi na mwaka mpya za Iran, hapa sasa ni vema tukasema machache kuhusu ada na desturi za Nairuzi nchini Iran. Muda wa makala hii umekaribia kufikia mwisho, hivyo tutagusia kwa muhtasari sana tu ada na desturi hizo.

Wakati wa kuingia mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia ambapo hivi sasa tumo katika mwaka wa 1397, huenda sambamba na kuwadia msimu wa machipuo na mabadiliko katika miti, mimea maua na majani. Bustani hunawiri kwa mandhari ya kijani kibichi na maua kuchanua. Kwa hakika mabadiliko hayo huashiria kumalizika msimu wa baridi na kuwadia kipindi cha upepo mwanana wenye kuleta utulivu wa moyo.

Katika msimu huu ambao ndio kwanza umeingia hapa nchini Iran hivi sasa, mimea huonekana ikiwa imechangamka na kunawiri ikiwa ni ishara ya kuwa na nishati na uchangamfu wa hali ya juu ikilinganishwa na vipindi vingine vya misimu ya mwaka. Kwa ufupi mandhari huwa ni ya kijani kibichi hali inayoashiria kufufuka maumbile na kuingia katika uhai mpya baada miti na mimea kukauka katika kipindi cha kipupwe na cha baridi kali. Katika msimu huu, bustani hunawiri kwa maua yaliyochanua kwa rangi tofauti yenye harufu nzuri.

Kwa hakika historia ya Wairani imejaa mafundisho ya kimaanawi ambayo mengi yake yametokana na mfungamano wa kidini wa jamii ya Iran ambao umejaa misingi ya maarifa na kutambua vyema maumbile ya mwanadamu. Maadhimisho haya huandamana na ada, mila na desturi mbalimbali na kutoa ujumbe wa amani, matumaini na bahati njema kwa mamilioni ya watu katika kona mbalimbali duniani.

Kila mwaka unapokaribia msimu wa machipuo na utangulizi wa kutokea mabadiliko ya kimsingi ya mimea na maumbile, Wairani hujiandaa kuupokea mwaka mpya kwa ada na desturi zao nzuri na za kuvutia. Kuna ada na mila mbalimbali za Wairani zinazohusiana na sikukuu hii kubwa ya kijadi. Baadhi ya ada na mila hizo zinahusiana na siku za mwisho wa mwaka, nyingine ni za wakati wa kuingia mwaka na baadhi yake zinahusiana na lahadha za kuingia mwaka mpya na siku za mwanzo za mwaka mpya.

Kila mwaka katika siku za kabla ya mwaka mpya yaani katika mwezi wa mwisho wa mwaka ambao unajulikana kwa jina la Esfand kwa kalenda ya Hijria Shamsia, masoko ya miji hufurika watu ambao huenda kufanya manunuzi ya mahitaji yao ya lazima kwa ajili ya siku za sikukuu ya Nairuzi kama nguo, vifaa vya nyumbani, vyakula na vitu kama hivyo. Hii ni kwa sababu wanataka kuhakikisha kuwa, watu wote wawe na nguo mpya za kuvaa na wawe na vyakula bora kabisa kwa ajili ya kuwakirimu wageni wakati wa sherehe za mwaka mpya.

Ada nyingine iliyozoeleka baina ya Wairani ambayo hufanywa katika siku za mwishoni mwa mwaka ni usafi wa jumla ambao unajulikana kama Khane Tekoni. Katika siku za mwisho wa msimu wa baridi, Iran hutawaliwa na harakati na hali maalumu ambapo watu wote hufanya hima zaidi ya usafi jumla wa nyumba, maeneo ya ibada kama misikini, vifaa vya nyumbani na hata maeneo ya umma katika bustani, barabara na mitaa ya miji. Usafi huu huwa wa aina yake na hutofautiana na ule usafi wa kawaida na wa kila siku. Bali usafi huu huambatana hata na kubadilisha upangaji wa vitu nyumbani, au hata kuweka mabusati mapya na kubadilisha vitu vya ndani ya nyumba kama makochi na mapazia na kadhalika na kununua vitu vipya.

Kimsingi Khane Tekoni, au usafi wa jumla wa nyumba ni kuondoa na kupangusa vumbi la nyumba na mji mwishoni mwa mwaka na ni nembo na ishara ya kujiandaa kuupokea mwaka mpya. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, dini tukufu ya Kiislamu inatilia mkazo juu ya suala la usafi ambapo Mtume SAW anautaja usafi kama ni ishara na dalili za imani. Mbora huyo wa viumbe anasema katika hadithi mashuhuri kwamba: Usafi ni katika imani. Kimsingi Khane Tekoni au usafi jumla wa nyumba hufanyika kwa ushirikiano wa wanafamilia wote na kila mtu hufanya kazi hiyo kulingana na uwezo wake kuanzia wakubwa hadi wadogo.

Sherehe za Nairuzi katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa

 

Amma katika ile lahadha na sekunde ya kuingia mwaka mpya watu wa familia hukusanyika pamoja na kuomba dua maalumu kwa Mwenyezi Mungu ya kuukaribisha mwaka mpya inayosema: "Ewe Mgeuzaji wa nyoyo na basari! Ewe Mpangiliaji wa Usiku na Mchana! Ewe Mbadilishaji wa mwaka na hali! Badilisha hali zetu kuwa bora ya hali."

Baada ya hapo husoma aya za Qur'ani na halafu mtu mzima zaidi wa familia huanza kutoa zawadi kwa wanafamilia na kikawaida fedha zinazotolewa kama zawadi huwa noti mpya kabisa.

Jengine kwa muhtasari ambalo ni vyema kulifahamu ni kwamba, maziara na maeneo matukufu hufurika watu wa kila rika katika ile lahadha na sekunde ya kuingia mwaka mpya wa Kiirani kwa ajili ya kumuomba Mwenyezi Mungu alete mabadiliko katika nafsi zao na vile vile kumuomba Mwenyezi Mungu abadilishe hali zao na kuwa bora ya hali wakiwa katika maeneo ya kimaanawi kama misikiti Husseinyiam haram na maeneo mengine matakatifu.

Yamebakia mengi bado ya kuashiria, lakini muda wa kipindi chetu umeisha kabisa kwa leo. Ishini Salama.

tamati

 

Tags

Maoni