Mei 01, 2018 08:35 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hujambo mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Jumatatu ya tarehe 30 Aprili ilisadifiana na siku ya mwisho ya kuondoka Wareno baada ya kutimuliwa kwenye eneo la maji ya kusini mwa Iran. Kwa mnasaba wa tukio hilo, siku hii inajulikana katika kalenda rasmi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama "Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi". Baada ya utangulizi huo mfupi nakuomba sasa ujiweke tayari kusikiliza yale niliyokuandalia kwa mnasaba wa siku hiyo.

Katika kalenda rasmi ya Iran kuna siku nyingi za matukio yenye kumbukumbu za kubakia milele. Lakini Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi ina sifa kadhaa maalumu na za kipekee. Sababu ni kwamba jina la Ghuba ya Uajemi limeambatana na kufungamana na historia ya eneo na utambulisho wa Iran wa miaka elfu kadhaa pamoja na eneo zima kwa ujumla. Ni kwa sababu ya yote hayo na kutokana na kuandamwa na maajinabi utambulisho wa kiutamaduni na wa kihistoria wa taifa la Iran, ndipo Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni likaamua kuitangaza tarehe 30 Aprili inayosadifiana na tarehe 10 Ordibehesht kuwa Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi.

 

Ghuba ya Uajemi ni moja ya bahari nne mashuhuri ambazo kwa mujibu wa itikadi ya Wagiriki wa kale chimbuko lao ni bahari moja kuu yenye upana unaolingana na wa maji yote ya dunia; na watu wote katika pembe tofauti za dunia walikuwa wakilijua eneo hilo kubwa la maji kwa jina la Pars au Uajemi. Ghuba ya Uajemi ambayo ni njia muhimu zaidi ya kusafirishia mafuta duniani ina mfungamano usiotenganika na ustaarabu na utamaduni wa Iran na ni moja ya majina ambayo tangu hapo kale na hadi hivi sasa limekuwa likitumiwa katika maandikiano na mikataba kati ya kaumu na mataifa mbalimbali yaliyo mbali na ya karibu.

Muhammad Ajam, mwandishi na mtafiti wa masuala ya Ghuba ya Uajemi na Asia Magharibi na mmoja wa waasisi na waendeshaji wa kituo cha mitaala ya Ghuba ya Uajemi anauzungumzia umuhimu wa eneo la Ghuba ya Uajemi na taathira za lango hilo bahari katika nyuga tofauti kwa kusema: Uhasasi na unyeti wa Ghuba ya Uajemi una umuhimu mkubwa sana kwa kuzingatia nafasi yake ya kiuchumi, kisiasa, kibiashara na kimawasiliano katika dunia hii pana. Katika nyaraka zilizopo zilizoandikwa kwa lugha ya Kiarabu eneo hili limetajwa kwa jina la "Khalijul-Farisy" na kuna nyaraka 11 pia zenye itibari za Umoja wa Mataifa ambazo nazo pia zimelitaja kwa uwazi kabisa jina la Ghuba ya Uajemi.

Hakuna shaka yoyote kuwa Ghuba ya Uajemi ina ukale kama ilivyo historia ya ardhi ya Iran; na jina la Uajemi katika eneo hili pana la maji ni sisitizo la utambulisho halisi wa historia ya eneo na pia ni hoja inayobatilisha utumiaji wa jina jengine lolote lile ghairi ya neno Ghuba ya Uajemi. 

 

Ghuba ya Uajemi ambayo ni njia kuu na muhimu ya bahari, tangu hapo kale na tokea karne na dahari, daima imekuwa na nafasi ya kipekee kisiasa; na leo hii pia ingali inatambulika kimataifa kuwa ndio njia muhimu zaidi ya bahari duniani. Lakini wakati huohuo, kwa sababu ya thamani na umuhimu wake wa kijiografia na kiustaarabu, Ghuba ya Uajemi imekuwa uwanja wa mashindano na mivutano pia baina ya madola ya kieneo na ya kimataifa. Miongoni mwa zama ambazo Ghuba ya Uajemi ilishuhudia uwepo wa maajinabi, ni kipindi cha miaka 150 ambapo njia hiyo ya majini na lango bahari la Hormuz vilikuwa vikidhibitiwa na Wareno. Lakini uwepo wao huo ulifikia tamati mnamo tarehe 30 Aprili mwaka 1621.

Jambo moja lililo wazi kabisa ni kwamba katika kipindi chote cha historia yake, na kwa mujibu wa nyaraka za kuaminika na zenye itibari, Ghuba ya Uajemi imekuwa daima ikijulikana kama sehemu ya ardhi ya Iran, na mamlaka ya utawala wake siku zote yamekuwa mikononi mwa Wairani. Katika enzi za utawala wa Wahakhamanesh, Wairani walikuwa wakiita bahari hiyo "Parsa Daraya" au "Bahari ya Pars". Wanahistoria wa Kigiriki wa zama za kabla ya kuzaliwa Nabii Isa AS yaani BC, kama Herodotus na Xenophon nao pia walikuwa wakiita njia hiyo muhimu ya baharini "Bahari ya Parsi".

Watafiti wa Kiislamu na Waarabu nao pia wameyataja katika athari na maandiko yao maji ya kusini mwa Iran kwa majina ya "Al-Bahrul-Farisiy" na "Khalijul-Farisiy". Pamoja na kuwepo nyaraka na ushahidi wote huo wa kihistoria, katika miongo ya karibuni na hasa kuanzia kipindi cha muongo wa 1960, baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo hili na harakati zenye mfungamano na maajinabi zimekuwa zikijaribu kutumia njia mbalimbali za kupotosha waziwazi historia ya eneo ili kwa dhana yao kuweza kulifuta jina la Ghuba ya Uajemi katika historia ya eneo hili. Katika uporaji huo wa ustaarabu na historia wamekuwa wakijaribu kuanzisha utambulisho bandia, ambapo hatua hiyo tab'an ni sehemu ya njama maalumu ya kisiasa. Kutunga historia bandia kwa ajili ya utambulisho wa kikaumu na kitaifa wa Ghuba ya Uajemi, ni moja ya malengo ya maajinabi, nia hasa ikiwa ni kuzusha hitilafu na tofauti katika eneo hili kwa kutegemea dhana hewa za kihistoria. Lakini kwa masikitiko inapasa tuseme kwamba, baadhi ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, ambazo hazina utambuzi kamili wa utambulisho na asili yao ya kikaumu na kikabila zimetumiwa kama wenzo wa mchezo huo wa kisiasa huku zikidhani kwamba zitaweza kujijengea utambulisho kwa kupotosha ukweli halisi wa kijiografia na kihistoria wa taifa na ardhi za watu wengine.

 

Ramani na maandiko ya kale kuhusiana na Ghuba ya Uajemi, eneo ambalo lina nafasi na hadhi ya aina yake ya kiutamaduni yanaonyesha kuwa ghuba hiyo pana ya ustaarabu ambayo inajulikana kama chemchemi ya suluhu, uweledi na uenezaji utamaduni kwenye maeneo mengine haijawahi kuwa na jina jengine lolote lile ghairi ya Ghuba ya Uajemi na wala hakuna anuani nyengine inayofaa na inayopendeza kubainisha hadhi na adhama yake ya kihistoria zaidi ya hiyo.

Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa hadi sasa imeeleza bayana kupitia taarifa mbili tofauti kwamba kwa mujibu wa nyaraka, maatlasi na ramani za kijiografia, jina la eneo hilo la majini ni Ghuba ya Uajemi. Miongoni mwa nyaraka na ushahidi huo ni taarifa maalumu iliyosajiliwa mwezi Agosti mwaka 1984 na kusainiwa na nchi 22 za Kiarabu za eneo hili kama hati ya Umoja wa Mataifa. Mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa pia, unaohusiana na uratibu wa majina ya kijiografia umekuwa ukisisitiza na kulitaja kila mwaka eneo hili kwa jina la Ghuba ya Uajemi.

Dakta Pirouz Mojtahedzadeh, mtafiti wa jiopolitiki na jiografia ya kisiasa ameashiria historia bandia iliyotungwa kuhusiana na jina la Ghuba ya Uajemi na kueleza kwamba katika kipindi chote cha miaka iliyopita, kila aliposhuhudia utumiwaji wa jina bandia la Ghuba ya Arabuni amekuwa akiviandikia barua ya malalamiko vyombo vya habari au viongozi wa Magharibi wanaofanya hivyo na kupokea majibu ya kuomba radhi. Profesa Mojtahedzadeh anafafanua zaidi kwa kusema:

Leo hii, katika ulimwengu wa masuala ya kielimu jina bandia kuhusiana na Ghuba ya Uajemi halitumiki abadani; na hizi chokochoko zinazofanywa na baadhi ya nchi za kandokando ya Ghuba ya Uajemi hazifanywi kwa msingi wa kujiamini, lakini zinatokana na ukaidi na ubishani wa kisiasa.

Mohamamad Reza Sahab, mkurugenzi wa taasisi ya Kijiografia na Kikatografia ya Sahab anasema:

"Kuna nyaraka zisizo na chembe ya shaka zinazothibitisha kuwa Wagiriki walikuwa wakiita (Ghuba ya Uajemi) Sinus Persicus, na Waarabu pia kwa muda wa karne kadhaa walikuwa wakiita Ghuba ya Farsi au Bahari ya Farsi. Lakini katika miaka ya karibuni jina hili limevamiwa na kupotoshwa mara kadhaa na nchi changa za kandokando ya Ghuba ya Uajemi."

Pamoja na kuwepo nyaraka za kuaminika na ushahidi wa historia usio na shaka kuhusu eneo hili, huenda watu wengi wakapitikiwa akilini mwao na suali kwamba, kuna ulazima gani basi wa kutenga siku maalumu na kuipa jina la Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi?

Sababu muhimu zaidi ya kutangazwa siku hii, ni kukumbusha adhama na asili ya historia ya eneo hili jinsi ilivyokuwa tokea tangu na tangu. Lakini kusadifiana siku hii na kumbukumbu ya kutimuliwa wavamizi wa Kireno katika Ghuba ya Uajemi nako pia kunafikisha ujumbe maalumu kwa madola ya kikoloni duniani ambayo tangu zamani yamekuwa yakitafuta njia ya kuidhibiti Ghuba ya Uajemi na maliasili zake muhimu. Madola hayo yamekuwa siku zote yakikiri kwamba dola lolote litakalolihodhi eneo hili hasasi na la kistratejia, bila shaka yoyote litakuwa na uwezo unaohitajika kwa ajili ya kufanikisha malengo yake kimataifa na kuzifanya nchi na mataifa mengine yawe chini ya utegemezi wake. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana kuihodhi Ghuba ya Uajemi limekuwa moja ya malengo makubwa ya madola ya kibeberu. Hata hivyo historia ya eneo hili na kusimama kidete taifa shujaa na lenye ghera la Iran kumethibitisha mara kadhaa kuwa maajinabi hawatoweza kamwe kuwa na nafasi yoyote ya kuihodhi na kuidhibiti Ghuba ya Uajemi.

 

Ali Akbar Veleyati, mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa siku ya Jumapili ya tarehe 29 Aprili alihudhuria sherehe ya uzinduzi wa kitabu kiitwacho Ghuba ya Uajemi. Akihutubia hafla hiyo, Dakta Velayati alitanabahisha kwamba, kulibadilisha jina la Ghuba ya Uajemi ni utangulizi wa kuimiliki na hatimaye kuzusha madai ya uongo kuhusiana na umoja wa ardhi yote ya Iran. Na akaongezea kwa kusema: Baadhi wanataka kulibadilisha jina la Ghuba ya Uajemi na utambulisho wake ili waweze kuihodhi Bahari ya Hindi; lakini wananchi na serikali ya Iran wamesimama imara kukabiliana na hilo, na jambo la uhakika na la kudumu ni jina la milele la Ghuba ya Uajemi; na madola ya kikoloni yatabaki na ndoto yao tu ya kulihodhi au kulibadilisha jina lake.

Mpenzi msikilizaji, maelezo hayo ya mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa ndiyo yanayotuhitimishia kipindi hiki maalumu kilichokujieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi. Nakushukuru kwa kunisikiliza na nakutakia usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.../

Tags

Maoni