Mei 30, 2018 07:41 UTC
  • Kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Hasan al Mujtaba AS

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji. Mwezi 15 Ramadhani ni siku inayosadifiana na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam Hasan al Mujtaba, mjukuu mpenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW.

Imam Hassan AS ni mtoto wa Bibi Fatimatuz Zahra SA na Imam Ali bin Abi Talib AS, na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Bwana Mtume SAW kuhamia katika mji mtakatifu wa Madina. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali AS. Leo tumekuandalieni makala maalumu ya kuangalia kwa muhtasari sira, mwenendo na mafundisho ya kimaneno na kimatendo ya mtukufu huyu, tukianza kwa kutoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa Waislamu wote ulimwengu kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa mjukuu huyo wa Bwana Mtume tukimuomba Allah azitakabalie funga na ibada zenu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

******

Tarehe 15 Ramadhani miaka 1436 iliyopita yaani mwaka wa tatu Hijria ilichomoza nuru katika nyumba ya Bibi Fatima na Imam Ali AS na kuiangazia nyumba hiyo tukufu baada ya kuzaliwa mtoto ambaye aliondokea kuwa dhihirisho la ukarimu na wema ulimwenguni. Katika siku hiyo Imam Ali na Bibi Fatma AS waliruzukiwa ua lao la kwanza lenye harufu nzuri yaani Imam Hasan al Mujtaba AS ambaye aliongeza joto la mapenzi baina ya watukufu hao. Imam Hassan alikuwa ishara na dhihirisho la moja ya ndoa tukufu kabisa na mjukuu wa kwanza wa Mtukufu Mtume Muhammad SAW. Baada ya Mtume SAW kuletewa habari ya kupata mjukuu wake wa kwanza alifurahi mno na uso wake ulionekana ukiwa na bashasha na furaha kubwa. Masahaba walimiminika kwa Bwana Mtume ili kumpongeza na kumpa mkono wa kheri na fanaka Bwana Mtume, pamoja na Imam Ali na Bibi Fatimatuz Zahra AS. Baada ya kuzaliwa mtoto huyo, Mtume SAW alimuadhinia katika sikio lake la kulia na kusoma iqama katika sikio lake la kushoto. Katika siku ya saba, Mtume SAW alimfanyia akika kwa kuchinja kondoo na kisha kuigawa nyama hiyo kwa masikini na wasiojiweza. Kuanzia siku hiyo ikawa ni sunna kwa Waislamu kumchinjia mtoto kondoo au mbuzi katika siku ya saba ya kuzaliwa kwake na sunna hiyo inajulikana kwa jina la akika. Mjukuu mkubwa wa Mtume Muhammad SAW alikuwa dhihirisho la wema, fadhila, hisani na ukamilifu na hakuwa na mithili katika sifa hizo wakati wa zama zake.

Alikuwa na sifa tukufu na za ukamilifu wa kibinadamu, sifa ambazo alizirithi kutoka kwa babu yake Bwana Mtume Muhammad SAW. Sifa nyingine aali alizojipamba nazo Imam Hassan AS ni uchaji Mungu, kushikamana na ibada, unyenyekevu, ushujaa, na kusamehe. Alikuwa akiwahimiza sana watu kujipinda kwa ibada ya kujiongezea elimu na kukuza akili zao. Katika sehemu moja ya maneno yake, mtukufu huyo amenukuliwa akisema: "Nawastaajabu wale watu wanaofikiria kushibisha matumbo yao, lakini hawajisumbui hata chembe kufikiria mambo ya ibada na kujifunza na kuzikuza akili zao" Kwa hakika Imam Hassan AS aliondokea kupendwa mno na Mtume SAW. Mapenzi makubwa ya Mtume SAW yalidhihirika zaidi pale aliposema:

"Ewe Mwenyezi Mungu! Mimi nampenda Hasan, Wewe pia mpende na kila mwenye kumpenda Hasan, basi Mwenyezi Mungu pia atampenda."

 

Moja ya sifa za wazi za Imam Hassan AS ambazo ni ruwaza njema kwa vipenzi vyake ni ukarimu wake wa hali ya juu. Imam Hassan alikuwa akimfanyia ukarimu mwenye kuhitaji mpaka anajiweza na kutokuwa mhitaji. Historia inaonyesha kuwa, mara mbili Imam Hassan alitoa kila alichokuwa nacho na mara tatu alitoa nusu ya mali yake katika njia ya Mwenyezi Mungu ili kuwafanyia ihsani watu wengine.

Imenukuliwa kwamba, Imam Hassan al Mujtaba hakuwa akimrejesha mikono mitupu mtu yeyote aliyemuomba na katu hakuwa akimnyima aliyeomba bali daima alikuwa akitoa na kufanya ukarimu. Siku moja aliulizwa, inakuwaje, wakati wote humrejeshi mikono mitupu yeyote anayekuja kwako akitaradhia hali yake, mtukufu huyo alijibu kwa kusema: Mimi mwenyewe ni mwenye kumuomba Allah na mwenye matarajio kutoka Kwake Muumba. Ninaona vibaya sana kumrejesha mikono mitupu mwenye kuniomba, ilhali mimi mwenyewe ninataradhia hali yangu kwa Allah wakati wote. Mwenyezi Mungu amenizoesha kunipatia ujazi na neema Zake na mimi nimezoea mkabala wake kuwazingatia waja Wake na kugawana nao neema ninazopewa na Allah. Kisha Imam akaendelea kusema, pindi mwombaji na mhitaji anapokuja kwangu humwambia, ahlan wasahlan ewe ambaye umenipa fursa ya kutenda hisani na wema. Ninamuheshimu sana mtu huyo kwani hunipa fursa ya kutenda wema. Siku bora kabisa ya muungwana ni siku ambayo huja mtu kumuomba kitu na yeye akamkidhia haja yake.

Katika kipindi chote cha maisha yake yaliyojaa baraka, Imam Hassan AS daima alikuwa akijishughulisha na kuwaongoza watu kuelekea katika njia ya haki. Muamala wake na watu wa kawaida hata maadui ulikuwa mzuri mno kiasi kwamba aliweza kumvutia kila mtu. Katika mafundisho ya Uislamu, matajiri wana majukumu mazito mbele ya wanaohitaji na wasiojiweza na wanapaswa kujitahidi kukidhi mahitaji ya wasiojiweza katika jamii.

 

Wapenzi wasikilizaji, haya ni matangazo ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kilichoko hewani ni kipindi maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Hasan al Mujtaba, mmoja wa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW.

Kwa hakika Mitume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu katika mawaidha na vitendo vyao, walikuwa mfano wa kuigwa kuhusu masuala ya kuwapenda na kuwahudumia wanaadamu wenzao. Miongoni mwa hawa, Imam Hassan Mujtaba AS alikuwa na nafasi ya juu kwa mtazamo wa elimu, taqwa, fadhila na ibada. Katika suala la kuwasaidia na kuwahudumia mafukara na wasiojiweza, Imam Hassan alikuwa mashuhuri sana hadi kufika kiasi cha kupewa lakabu ya "Karim Ahlul Bayt" kutokana na ukarimu wake mkubwa.

Uwepo uliojaa baraka wa mtukufu huyo ni jambo ambalo lilileta utulivu kwa watu maskini, mafukara na wasiojiweza. Imam Hassan AS alikuwa kimbilio la waliokumbwa na masaibu ya kila namna na nui, alikuwa tumaini la wanyonge na wasiojiweza na mtulizaji nyoyo za wenye hangaiko. Kama tulivyosema, haikuwahi kushuhudiwa hata mara moja, mwenye haja kwenda kwa mtukufu huyo na kurejea akiwa mikono mitupu.

Zamakhshari ameandika katika kitabu chake cha Rabiul Abrar akinukuu hadithi kutoka kwa Anas bin Malik ya kwamba, siku moja mimi nilikuwa kwa Imam Hassan bin Ali AS, mara akaja kijakazi na kumpa zawadi ya maua Imam Hassan. Baada ya Imam Hassan kupokea maua yale akasema, uko huru katika njia ya Mwenyezi Mungu. Baada ya Anas bin Malik kushuhudia hayo akamwambia Imam kwa mshangao: Kijakazi huyu amekupa maua tu ambayo hayana thamani yoyote na wewe umemuachia huru? Imam alisema kumjibu Anas bin Malik kwamba: Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu alivyotufundisha. Allah anasema katika aya ya 86 ya Suratun Nisaa kwamba:

"Na mnapoamkiwa kwa maamkio yoyote, basi nanyi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo..." Hivyo basi, jibu bora la wema wa kijakazi huyo ni kumuachia huru." Aidha imekuliwa katika vitabu vya historia kisa kifuatacho. Pamoja na kwamba Imam Hasan al Mujtaba AS alikuwa mkarimu sana, lakini pia alikuwa akihimiza watu wajitegemee na waongeze juhudi katika maisha yao ili wasihitajie misaada isipokuwa wakati wa dharura sana. Siku moja Bwana mmoja alikwenda kwa Imam Hassan AS na kumuomba amsaidie fedha. Alimkuta Imam Hasan akiwa pamoja na ndugu yake Imam Husain AS. Imam Hassan al Mujtaba akamwambia yule bwana: Haijuzu kuwaomba watu isipokuwa katika mambo matatu. Kuwa na wajibu wa kulipa dia, lakini mtu akawa hawezi kulipa, au deni ambalo mtu hana uwezo wa kulilipa au masikini ambaye hana uwezo wa kukidhi mahitaji yake. Je wewe unataka tukusaidie lipi katika ya haya matatu? Bwana yule akasema, shida yangu ni moja kati ya mambo haya matatu. Imam Hassan akatoa dinar 50 na kumpa yule bwana kwa heshima na taadhima. Imam Hussein kwa upande wake kwa heshima ya kaka yake akampatia bwana yule dinari 49 ambazo zilimkidhia haja yote aliyokuwa nayo. Kisa hiki kinatufunza pamoja na mambo mengine kwamba, tunapomsaidia mwenye haja na ikawa hali inaturuhusu, basi tumsaidie kiwango cha kukidhi haja yake, ili mtu huyo asilazimike kwenda kuomba kwa wengine.

 

Kwa hakika suala la kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuwasaidia wasiojiweza ni jambo ambalo limetiliwa mkazo mno katika dini tukufu ya Kiislamu na katika Qur'ani Tukufu. Aya nyingi za Qur'ani Tukufu zinabainisha namna wanaowasaidia wengine wanavyopata ujira mkubwa ambao ni ujira wa kudumu na kubakia milele. Kwa mtazmo wa Qur'ani ni kuwa, moja ya majukumu muhimu ya watu katika jamii ya Kiislamu ni kuwasaidia wahitaji na wenye shida. Kila mtu anapaswa kusaidia kulingana na uwezo wake. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 274 ya Surat al-Baqara kwamba:

"Wale wanaotoa mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhaahiri, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika."

Imam Hassan al-Mujtaba AS akiwa kiongozi mkubwa wa Waislamu alikuwa mstari wa mbele katika kutoa na kuwatatulia shida zao wahitaji na watu wasiojiweza. Alikuwa akiwasaidia na kuwapa utulivu na matumaini katika nyoyo zao. Si hayo tu, lakini pia alikuwa akikaa pamoja na maskini, akila nao, akiamiliana nao kwa wema n.k.

Kiujumla ni kwamba Imam Hassan al-Mujitaba AS alikuwa na sifa nyingi bora za ukamilifu wa kibinadamu na sifa zake za maadili bora zilienea katika kila kona na zilikuwa zikizungumziwa na wengi katika zama zake. Moja ya sifa zake nyingine bora ilikuwa ni subira na uvumilivu mkubwa. Vitabu vingi vya historia vimeizungumzia kwa upana sifa yake hiyo bora. Hata maadui wakubwa wa Ahlul Bait wa Bwana Mtume Muhammad SAW kama vile Marwan walishindwa kuficha sifa hiyo na walikiri waziwazi kwamba uvumilivu na subira ya Imam Hassan AS ilikuwa imara kama mlima.

Uvumilivu na subira ya aina yake aliyokuwa nayo Imam AS ilipelekea kulindwa Uislamu na kuzidi kupata nguvu dini hiyo tukufu hadi hadi leo licha ya kupita karne nyingi za zama alizoishi duniani mtukufu huyo. Uvumilivu wa mtukufu huyo ulifikia kilele cha kunawiri baada ya kuwekeana makubaliano ya suluhu na Muawiya. Kama si subira na uvumilivu mkubwa, Imam asingeliweza kukabiliana na kipindi hicho kigumu mno katika maisha yake matukufu. Imam Hassan AS alilazimika kukubali suluhu hiyo ya kulazimishwa, ili kuilinda dini aliyokuja nayo babu yake, yaani Bwana Mtume Muhammad SAW. Ni jambo lililo wazi kuwa, nguzo na msingi mkuu wa Uislamu ungelikuwa hatarini kama asingelikubali suluhu hiyo. Mbali na kuvumilia vitimbi vya Muawiya, Imam alilazimika pia kuvumilia lawama kutoka kwa watu waliokosa kuwa na muono wa mbali. Aliwajibu watu waliokuwa wakimkosoa na kulalamika suluhu yake na Muawiya kwa kuwaambia: "Mimi nimefanya suluhu kwa ajili ya kulinda damu ya Waislamu. Kama nisingelifanya hivyo basi hakuna hata mmoja kati ya wafuasi wetu ambaye angebaki hai duniani... Ole wenu! Hamjui nimefanya hivyo kwa lengo gani? Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, kukubali suluhu kwa ajili ya wafuasi wangu ni bora zaidi kuliko kile kinachoangaziwa na jua wakati wa kuchomoza na kutua kwake..."

 

Naam wapenzi wasikilizaji, hiyo ni sehemu ndogo tu ya sifa bora kabisa za Watu wa Nyumba wa Mtume wa Rehma, Muhammad al Mustafa, SAW. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa Waislamu wote ulimwenguni kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa mjukuu huyo wa Bwana Mtume, Imam Hassan bin Ali al Mujtaba AS, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Tags

Maoni