Jul 14, 2018 12:46 UTC
  • Siku ya Idadi ya Watu Duniani

Tarehe 11 Julai mwaka huu dunia iliadhimisha Siku ya Idadi ya Watu Duniani. Tarehe 11 Julai mwaka 1989 alizaliwa mtu wa bilioni tano katika sayari hii ya dunia.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Javier Pérez de Cuéllar alieleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko kubwa la idadi ya watu duniani na kumtaja mwanadamu huyo nambari bilioni tano kuwa ni tukio muhimu katika historia ya dunia. Alisisitiza kuwa kuna haja na udharura mkubwa zaidi wa kuwepo ustawi endelevu, kuboreshwa huduma za elimu, afya na masuala ya kijamii.

Tangu wakati huo Umoja wa Mataifa ulipendekeza tarehe 11 Julai kila mwaka ipewe jina la Siku ya Idadi ya Watu Duniani. Lengo ni kuwahamasisha wanadamu kuweka taratibu na mipango mizuri zaidi ya ustawi na ushirikiano katika masuala ya idadi ya watu.

Shirika la Idadi ya Watu Duniani la Umoja wa Mataifa (UNFPA) linakadiria kwamba, idadi ya wanadamu wote waliozaliwa katika historia ya kiumbe huyo hadi kufikia mwaka jana wa 2017 ni karibu bilioni 108. Kwa mujibu wa takwimu hiyo, idadi ya watu duniani mwaka 1804 ilikuwa karibu bilioni moja. Katika miaka ya 1927, 1960 na 1974 idadi ya watu duniani ilikuwa bilioni 2, 3 na 4 kwa utaratibu. Takwimu za karibuni kabisa zinasema kuwa, mwanzoni mwa mwaka 2017 idadi ya watu duniani ilikuwa karibu bilioni 7 na milioni 285. Takwimu hizi zinaonesha kuwa, moja ya 15 ya idadi ya watu wote katika historia ya mwanadamu wako hai kwa sasa.

Asilimia 60 katika idadi hiyo ya watu duniani wanaishi barani Asia. Asilimia 20 katika hiyo 60 wako China na asilimia 17 wanaishi India. Hii ina maana kwamba, zaidi ya mtu mmoja baina ya kila watu watatu wanaoishi katika sayari hii ya dunia ama ni Wachina au Waindia. Asilimia 12 ya idadi ya watu wa dunia wako Afrika na asilimia 11 wanaishi Ulaya. Karibu asilimia 13 ya watu wa dunia wanaishi America ya Kaskazini na Kusini. Mji wa Vatican ambao una serikali inayojitawala katikati ya jiji la Roma huko Italia na wenye jamii ya watu 800 na Jamhuri ya Nauru yenye jamii ya idadi ya watu 9378 ndizo nchi zenye idadi ndogo zaidi ya watu duniani. Nchi za China, India, Marekani, Indonesia Pakistan na Brazil zina nusu ya idadi ya watu wote duniani. 

Kwa kutilia maanani takwimu zilizotolewa, kwa wastani kila dadika moja watu 150 huongezeka kwenye idadi ya watu wa dunia. Kwa mwenendo huu wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanakadiria kuwa, hadi kufikia mwaka 2050 idadi ya watu duniani itafikia bilioni 9.8 na kwamba ongezeko hilo la watu litakuwa kubwa zaidi katika nchi zinazostawi. Takwimu zinaonesha kuwa, nusu ya ongezeko la idadi ya watu duniani itazihusu nchi za India, Nigeria, Pakistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Tanzania, Indonesia na Uganda. Hadi kufikia mwaka 2022 idadi ya watu wa India itakuwa kubwa zaidi ya ile ya China.

Ongezeko hilo la idadi ya watu duniani litaonekana zaidi barani Afrika na idadi ya watu wa bara hilo itakuwa mara dufu. Taasisi ya Utafiti wa Idadi ya Watu ya Ufaransa inasema: "Miongoni mwa mabadiliko makubwa yanayokuja ni ongezeko kubwa la idadi ya watu barani Afrika." Kwa sasa mtu mmoja kati ya kila watu sita duniani anaishi barani Afrika, na karne moja ijayo mtu mmoja kati ya kila watatu duniani atakuwa barani Afrika. Idadi ya watu bilioni 1.2 waliokuwa wakiishi Afrika mwaka 2017 inatazamiwa kufikia bilioni 2.5 mwaka 2050 licha ya maradhi mbalimbali yanayoliandama bara hilo, na huwenda hadi kufikia mwaka 2100 idadi ya Waafrika itafikia watu bilioni 4.4.  

Umoja wa Mataifa umetaja sababu ya ongezeko la idadi ya watu duniani kuwa ni kuongezeka kwa matarajio ya kuishi (life expectancy) duniani. Ripoti zinasema kuwa, matarajio ya kuishi yamepanda kutoka miaka 65 mwaka 1990 na kufikia umri wa miaka 70 mwaka 2010. Zinaongeza kuwa, hadi kufikia mwaka 2045 matarajio ya kuishi yatafikia umri wa miaka 77. Kupungua kwa vifo vya watoto wadogo pia ni miongoni mwa mambo yanayopelekea kuongezeka idadi ya watu duniani hususan katika nchi zinazostawi.     

Wasomi wa Taasisi ya Utafiti wa Idadi ya Watu ya Ufaransa wanasema: "Japokuwa kiujumla kiwango cha uzazi (fertility) kimepungua kiasi duniani lakini ufa umeongezeka zaidi katika maeneo mbalimbali ya dunia. Mwaka 1950 kwa wastani kila mwanamke alikuwa akizaa watoto watano lakini kiwango hicho hii leo kimepungua na kufikia watoto 2.5. Kiwango cha chini kabisa cha uzazi na kuzaa kwa sasa kinashuhudiwa Taiwan na Korea Kusini ambako wastani wa kuzaa kila mwanamke ni mtoto 1.2, na kiwango cha juu zaidi cha uzazi kinashuhudiwa Nigeria kwa kila mwanamke kuzaa watoto 7.3. Nchi ambazo kila mwanamke huzaa zaidi ya watoto 3 kwa wastani zinajumuisha nchi zote za Afrika, baadhi ya nchi za bara Arabu na baadhi ya nchi za Asia kama Pakistan, Afghanistan hadi kaskazini mwa India. Ni katika nchi hizo ndiko kutakakokuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu duniani katika miaka ijayo."   

Kinyume na hali inavyoshuhudiwa katika nchi zinazostawi, kuna nchi zinazosumbuliwa na kutokuwa na ongezeko la idadi ya watu au ongezeko la mwendo wa kinyonga na dogo kupita kiasi. Wataalamu wanasema, kupungua ongezeko la idadi ya watu katika nchi hizi kutatia kasi katika mwenendo wa kuzeeka kwa jamii za nchi husika. Kutokana na ukweli kwamba, idadi ya vijana ni miongoni mwa vigezo muhimu vya ustawi na rasilimali muhimu ya kila nchi, baadhi ya nchi zinakutambua kupungua idadi ya watu katika jamii kuwa ni tatizo na pigo kubwa. Kwa msingi huo tangu mwaka 2010 hadi 2015 kiwango cha uzazi katika nchi 83 zenye asilimia 46 ya idadi ya watu duniani, kilikuwa chini ya makadirio. Kwa sababu hiyo nchi hizo ziliweka mikakati na kuanza kutekeleza sera za kuhamasisha ongezeko la uzazi ili kuepuka kuzeeka kwa jamii. Ni kwa kutilia maanani hali kama hii ndiyo maana mipango ya kuratibu masuala ya idadi ya watu ikatofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine.

Nchi zinazostawi zinazokabiliana na matatizo chungu nzima ya ongezeko kubwa la idadi ya watu zinalipa kipaumbele suala la kupunguza au kudhibiti ongezeko hilo. Ripoti ya mtandao wa "water.org" inasema, watu milioni 662 katika nchi hizo hawapati maji safi ya kunywa. Vilevile shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linasema kuwa mwaka 2015 watu milioni 795 hawakuwa na uwezo wa kupata chakula cha kutosha. Ripoti ya WFP imeongeza kuwa, 1 ya 9 ya jamii ya watu duniani inalala njaa, na kwamba kila siku watu elfu 25 wanafariki dunia kutokana na utapiamlo au maradhi yanayosababishwa na uhaba wa chakula. Vilevile ongezeko holela la idadi ya watu duniani limepunguza sana uzalishaji na ugavi wa chakula, na ugawaji wa maeneo au mashamba finyu baina ya idadi kubwa ya watu umesababisha matatizo ya kiafya, ghasia na machafuko katika familia, ukosefu wa kazi, msongamano mkubwa wa watu eneo moja, uchafuzi wa mazingira na matatizo mengine mengi ya kijamii. Vilevile vita na mapigano ya muda mrefu yaliyoshuhudiwa katika miongo ya hivi karibuni imesababishwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu na kugombania mashamba na rasilimali.

Kuwepo kwa hali hiyo kunazidisha udharura wa kupangwa ratiba za kudhibiti idadi ya watu katika familia. Suala la kupanga uzazi ni jukumu la pamoja la mke na mume na kutiliwa maanani suala hilo kunaweza kuzidisha hali bora, afya na utulivu ndani na nje ya familia. Uzazi wa mpango hupunguza mimba zisizotarajiwa, na kuwafanya wanafamilia yaani mke na mume kuwa na idadi ya watoto wanayoitaka wao na kupanga muda unaotenganisha baina ya mimba moja na inayofuata. Kwa msingi huo baadhi ya nchi kama China na India zimekhitari kaulimbiu ya "Udhibiti wa Uzazi na Idadi Ndogo wa Watoto" kama njia ya kufikia kwenye hali bora. Hata hivyo jambo litakalofanikisha mpango huo ni kutilia maanani haki za binadamu ndani ya familia katika kudhibiti idadi ya watu na uzazi wa mpango.

Maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani

Mkutano wa kwanza kabisa wa haki za binadamu uliofanyika mwaka 1968 ulipasisha kuwa ni haki ya binadamu kupanga utaratibu wa uzazi ndani ya familia. Hati ya mwisho ya mkutano huo iliyopewa jina la Azimio la Tehran iliweka bayana kwamba: "Wazazi wawili wana haki ya kimsingi katika kuainisha idadi ya watoto na tofauti ya umri baina yao na wana haki ya kuchukua uamuzi kwa uhuru katika masuala hayo." Ili kutilia mkazo suala hilo, Umoja wa Mataifa umeitangaza kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani kuwa ni "Kupanga Uzazi ni Haki ya Binadamu (Family Planning is a Human Right).

Pamoja na hayo hii leo familia nyingi duniani zimefikia natija kwamba, ongezeko la idadi ya watu linaweza kuwa ama fursa nzuri au tishio. Jamii yenye idadi kubwa ya watu wenye viwapa, elimu, maendeleo na hali bora ni fursa na neema kwa nchi yoyote ile, lakini katika jamii isiyokuwa na viwango vya maisha bora na mazuri, ongezeko la idadi ya watu linaweza kuwa na madhara kwa familia na nchi husika. Suala hili lina umuhimu mkubwa sana katika maamuzi ya familia kwa ajili ya kupanga uzazi.      

Maoni