Sep 11, 2018 07:46 UTC
  • Nafasi ya Qur'ani Tukufu katika mapambano ya Imam Husain AS (1)

Mapambano ya Karbala na Hamasa ya Imam Husain AS alikuwa ni mapinduzi ya kipekee ambayo yaliweza kwa haraka mno kushinda mapinduzi mengine yote, kuwafedhehesha madhalimu, kufichua uovu wao na kusafisha vumbi la propaganda chafu lililokuwa limefunika uhakika wa dini tukufu ya Kiislamu.

Leo tumeamua tuanze kungalia japo kwa juu juu nafasi ya Qur'ani tukufu katika mapambano ya Imam Husain AS katika kukabiliana na watu na matukio yaliyojiri katika kipindi chote cha tangu kutoka Madina mtukufu huyo kuelekea Makka hadi kuwasili kwake Karbala na kuendesha mapambano ya kishujaa ambayo yatabakia katika umri wote wa mwanadamu. Imam Husain AS alitumia vyema kila fursa aliyoipata kusoma aya za Qur'ani Tukufu na kutoa ufafanuzi wa aya hizo kwa ajili ya kuzinyoosha nyoyo za watu waliopotea na vile vile kuwafafanulia sababu za kwa nini ameamua kuongoza mapambano dhidi ya madhalimu na kufufua dini ya Uislamu halisi.

******

Wapenzi wasikilizaji, Qur'ani na Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW ni madhihirisho mawili ya uhakika mmoja na kila moja ya vizito hivyo viwili ni dhihirisho la rehema, mahaba na uongofu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Vizito hivyo viwili havitengani kabisa na kwa wale wanaotaka kuelewa kwa undani kabisa mafundisho ya Qur'ani Tukufu, hawana njia nyingine isipokuwa kurejea kwa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW na kusoma kwa kina na uangalifu sira za kinadharia na kivitendo za watukufu hao.

Katika mfumo wa kimaumbile, haiwezekani dunia kuwepo bila ya uwepo wa Imam maasumu kama ambavyo ni muhali kuweza kutambua inavyotakiwa undani wa aya za Qur'ani Tukufu bila ya kupitia kwa Imam maasumu. Hadithi maarufu, mutawattir na iliyopokewa na watu wengi sana ya "thaqalayn" inabainisha kwa uwazi uhakika huo. Katika lahadha ya mwisho ya uhai wake hapa duniani, Bwana Mtume Muhammad SAW alisema: "Mimi ninaondoka, lakini nimekuachieni vitu viwili vizito na vyenye thamani; kimoja ni Kitabu cha Allah, Qur'ani Tukufu na kingine ni kizazi na Ahlulbayt wangu; vizito viwili hivi haviwezi kutengana kamwe hadi vitakapokutana nami katika hodhi ya Kauthar."

Maimamu watoharifu kutoka kizazi kitukufu cha Mtume Muhammad SAW ni Huja wa Mwenyezi Mungu ardhini, na Imam Husain bin Ali AS ni miongoni mwao. Maimamu hao ni ruwaza za heshima, uhuru, ukombozi na ni viongozi wa jihadi na kuwa tayari kufa shahidi katika njia ya Allah, huku Imam Husain AS akiwa na lakabu ya Bwana wa Mashahidi. Imam Husain AS aliishi na Bwana Mtume Muhammad SAW kwa karibu miaka sita na alikuwa pamoja naye katika kitovu cha wahyi na nuru ya Qur'ani Tukufu na hivyo aliweza kuwa na maarifa makubwa sana kuhusu Qur'ani Tukufu. Kama ilivyokuwa kwa babu yake, Bwana Mtume Muhammad SAW, tabia za Imam Husain pia kila kitu chake kinakwenda kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani Tukufu kutokana na malezo bora aliyoyapata kutoka kwa babu yake Mtume Muhammad SAW, baba yake Imam Ali AS, na mama yake, binti wa Mtume, Bibi Fatimatuz Zahra AS.

Kwa Imam Husain AS, Qur'ani ilikuwa ni mkondo wa kina kirefu cha bahari ya elimu na maarifa. Alikuwa akisisitiza mara zote kuwa Qur'ani Tukufu ndio msingi mkuu wa maisha ambao inabidi kuusoma muda wote na kuufanyia kazi. Amenukuliwa akisema: Kitabu cha Allah yaani Qur'ani Tukufu, kimesimama juu ya nguzo nne kuu. Ibara, ishara, mambo ya kupendeza na uhakika. Ibara katika Qur'ani ni kwa ajili ya watu wa kawaida. Ishara na mambo yasiyo wazi ni kwa ajili ya waja maalumu wa Allah. Mambo ya kuvutia na kupendeza ni kwa ajili ya mawalii na uhakika uliomo ndani ya Qur'ani ni kwa ajili ya Mitume na Manabii. Hivyo kila mtu anaweza kupiga mbizi kwa kadiri ya uwezo wake ndani ya Qur'ani tukufu na kustafidi na elimu na welewa kwa kiwango cha ufahamu wake.

Imepokewa katika hadithi kwamba Abdurrahman Salami, alimsomesha mtoto wa Imam Husain AS sura ya Alhamdu. Mtoto huyo akaenda kwa baba yake mtukufu na kumsomea sura hiyo. Imam alitoa dinari na zawadi nyingi kumpa Abdurrahman Salami. Baadhi ya watu walidadisi na kusema, zawadi zote hizo umetoa kwa sababu ya kusomeshwa mwanao sura ya Alhamdu tu?! Imam aliwajibu kwa kuwaambia, kitu nilichotoa mimi kinaweza wapi kulipa fadhila na kazi kubwa iliyofanywa na mwalimu huyu wa Qu'rani wa mwanangu?

 

Mapambano ya Imam Husain AS yalitokea kwenye kipindi muhimu na hatari mno katika historia ya Uislamu mapambano ambayo yaliishia kwenye tukio adhimu na lenye funzo kubwa la Karbala katika siku ya Ashura, ya mwezi 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Hadi hivi sasa watafiti, waandishi na wasanii wameliakisi tukio hilo adhimu kwa sura tofauti na kutoa uchambuzi na tafsiri mbalimbali ambapo moja ya tafsiri na utafiti huo ni nafasi ya Qur'ani Tukufu katika harakati adhimu ya Imam Husain AS.

Katika muda wote, iwe ni wakati alipokuwepo mjini Madina, au njiani baina ya Madina na Makka au alipokuwa njiani baina ya Makka na Karbala, katika sehemu zote hizo Imam Husain AS alitoa darsa na ufafanuzi tofauti kuhusu Qur'ani Tukufu, alionesha mapenzi yake makubwa kwa Kitabu hicho kitakatifu na alitumia aya zake kuwaelimisha watu kuhusu misdaki na madhihirisho ya wazi ya ufisadi na udhalimu.

Baada ya Muawiya, mwanawe Yazid alihodhi madaraka bila ya ustahiki wala kuwa na sifa za kuwa kiongozi. Bali Yazid alikuwa maarufu kwa ufisadi na kutofaa kwa lolote. Hivyo alihitajia uungaji mkono wa watu mashuhuri ili kuimarisha utawala wake wa kidhulma. Wakati Walid bin Utbah aliposhindwa kuwakinaisha kwa njia za kawaida wakazi wa mji mtakatifu wa Madina na baada ya wakazi hao wa Madina kukataa kutangaza utiifu wao kwa Yazid, Marwan ibn al-Hakam, aliamua kutumia njia za vitisho na ukandamizaji kwa tamaa ya kupata mkono wa utiifu kwa ajili ya utawala dhalimu wa Yazid. Bay'a na mkono wa utiifu wa Imam Husain AS ungelitosha kabisa kuupa uhalali utawala wa Yazid, hivyo Marwan alikwenda kwa Imam Husain AS kujaribu kumlazimisha atangaze utiifu wake kwa Yazid. Imam AS alimsomea Marwan aya za Qur'ani Tukufu na sambamba na kufichua wazi sura ya ukandamizaji na jinai za Bani Umayyah aliwatangazia walimwengu kuwa daraja ya kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume SAW ni ya juu mno na haiwezi kufananishwa na ya Bani Umayyah! Imam alimwambia Liwali wa Yazid, yaani Marwan ibn al Hakam kwamba: Ole wako! Wewe ni muovu na mchafu, wakati sisi ni kizazi ambacho Mwenyezi Mungu amesema juu yetu kwamba: Kwa hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu nyinyi Ahlul Bayt na kukusafisheni kwa usafi uliokamilika. (Surat al Ahzab, aya ya 33). Na baada ya hapo alimwambia Marwan, mithili yetu sisi, kamwe hatuwezi kutangaza utiifu kwa mtu muovu kama Yazid.

Kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, wale watu wanaofikia ukamilifu wao wa kibinadamu na waliopikika barabara kwa imani, huwa hawana hofu na wala hawahuzuniki. Ni kwa sababu hiyo na ni kwa kushikamana kwake na tawhidi hiyo ndio maana Imam Husain AS hakuogopeshwa na udikteta na ukatili wa kupindukia wa Yazid bin Muawiya, bali aliamua kutoka Madina na familia yake yote kwa ajili ya kwenda kuitetea na kuihami dini ya Uislamu.

Tags

Maoni