• Wafuasi wa Imam Hussein AS

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachozungumzia fadhila na ubora wa masahaba wa Imam Hussein (as) na imani yao thabiti, kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika jangwa la Karbala, wafuasi wa Imam Hussein (as) walikuwa wa kila aina, kila umri na kila rangi. Mzee, kijana, mwanamke na mtoto, mweusi kwa mweupe, wote walikuwa katika jangwa hilo kwa ajili ya kumnusuru Imam Hussein Bin Ali bin Abi Twalib (as). Baadhi ya masahaba kama vile Habib Bin Madhahir na Muslim bin Ausajah ni miongoni mwa Mashia waliokuwa na ikhlasi na masahaba wa zamani, huku baadhi yao wakiwa ni kama vile Zuhair bin Qain Bajala na Othmani Maslak. Aidha wengine walikuwa ni kama vile Wahab bin Abdullah Kalbi, Mkristo ambaye ndio kwanza alikuwa amesilimu na kuingia katika Uislamu ambapo aliendelea kushikamana na mjukuu huyo wa Mtume (as) na kuuawa shahidi.

******

Ndugu wasikilizaji mnafaa kufahamu kwamba, mwanzoni mwa kudhihiri dini ya Uislamu kulijiri vita na mapigano mengi dhidi ya ukafiri na udhalimu, hata hivyo hakuna mapigano yaliyokuwa na sifa ya usafi na ikhlasi kama yale ya Karbala. Hii ni kusema kuwa, katika vita hivyo kwa uchache kulidhihiri aina fulani ya kutokuwepo ikhlasi kwa baadhi ya  watu na wakati mwingine kulishuhudiwa nukta za giza lililotokana na unafiki na kupenda dunia. Baadhi ya askari ambao walikuwa wakipigana vita ima hawakuwa na ari, au walikuwa na woga na walikuwa na tamaa ya kupata ngawira na mali na wakati mwingine walimuacha hata Mtume Muhammad (saw) peke yake akiwa na masahaba wachache tu waaminifu. Kama ilivyotokea katika vita ya Uhud ambapo wapenda dunia miongoni mwa askari walimuacha Mtume akiwa peke yake huku akinusurika kuuawa. Aidha katika vita vya Khandaq (Vita vya Ahzab) pia masahaba wa Mtume (saw) walikumbwa na woga wa kukabiliana na wapiganaji shujaa wa Kikuraishi ambapo walishindwa hata kuinuka katika maeneo yao kwa ajili ya kupambana na mushrikina. Hali ikiwa hivyo katika vita hivyo, katika tukio la Karbala, Imam Hussein (as) kwanza aliondoa baia (kiapo) kutoka kwa masahaba wake wote, ambapo alimtaka kila mmoja wao kuondoka uwanja wa Karbala kwa sababu yoyote ile. Katika njia yao kuelekea Karbala na kwa mara kadhaa, wafuasi wa Imam Hussein walikuwa wakisafisha nia na kuamua kumfuata mjukuu huyo wa Mtume (saw). Hii ni kwa kuwa walimfahamu Imam kuwa mtu bora wa zama zao ambaye mapinduzi yake yalipasa kuwa mema ili yawe fundisho kwa zama na vizazi vijavyo. Kila mtu aliyesalia pamoja na Imam Hussein alijitenga mbali na aina yoyote ya wasi wasi na udhaifu. Na suala hilo ndilo liliifanya siku ya Ashura kuwa kiigizo chema na kamilifu. Wakati habari ya kuuawa shahidi Muslim Bin Aqil ilipowafikia watukufu hao, Imam aliwakusanya masahaba wake na kusema: "…Mashia wetu wametuacha, anayetaka kati yenu kuondoka, basi na aondoke bila ya tatizo na mimi nimeondoa kutoka kwake baia na hatokuwa na dhima yoyote kwetu sisi." Mwisho wa kunukuu. Hata hivyo masahaba hao wa mjukuu wa Mtume ambao walifadhilisha kifo cha shahada kuliko maisha ya udhalili, waliendelea kusalia pamoja na Imam Hussein hadi mwisho wa uhai wao.

 

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni kipindi maalumu kinachozungumzia fadhila na ubora wa masahaba wa Imam Hussein na imani yao thabiti, kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wakati Imam Hussein (as) alipowasili jangwa la Karbala tarehe pili mwezi wa Muharram mwaka 61 Hijiria na akiwa na masahaba wake aliomba dua akisema: "Ewe Mola wangu! Ninajikinga kwako kutokana na shida na balaa…Mola wangu! Ninajikinga kwako kutokana na huzuni na tabu. Hii ni sehemu ya mafikio yetu. Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba eneo hili ndipo tutafufuliwa siku ya Kiama. Nilisikia kauli hii kutoka kwa babu yangu, Mtume wa Mwenyezi Mungu na hakuna shaka yoyote katika kauli yake." Mwisho wa kunukuu. Licha ya wafuasi wa Imam kusikia maneno ya mtukufu huyo, hawakuondoka mahala hapo na kumuacha peke yake. Katika kitabu cha Injili imepokewa kuwa Nabii Isa (as) alikuwa na masahaba 12 waaminifu na waliotambulika kwa jina la 'Hawariyyuna.' Hata hivyo katika usiku ambao nabii huyo wa Mungu alitabiri kuwa atapatwa na shida, masahaba hao si tu kwamba walipatwa na wasi wasi mkubwa kwa kuwaogopa askari wa adui, bali mbali na Yuda, wengine pia walikaribia kumkana Nabii Isa (as).

Hii ni katika hali ambayo Imam Hussein (as) katika usiku wa Ashura na baada ya kuwaomba adui muhula wa usiku mmoja, alitoa hotuba nyingine kwa masahaba wake akisema: "Mwenyezi Mungu nakushukuru sana pia nakushukuru kwa mema na mazito, tabu na raha. Mola wangu nakushukuru kwa kuwa wewe ni Mwenyezi Mungu ambaye ulimtuma kwetu Mtume ambaye alitufundisha elimuu ya Qur'ani na elimu ya dini. Mungu ambaye umetupa sisi masikio, macho na mioyo. Mwenyezi Mungu tujaalie tuwe kati ya watu wanaokushukuru. Ama baad! Mimi sijui wafuasi wengine ambao ni bora na wa kujitolea kama masahaba zangu wala familia ambayo ni tiifu na kweli kama familia yangu. Mwenyezi Mungu akupeni malipo mema kwa kunisaidia." Akiendelea na hotuba yake mjukuu huyo wa Mtume aliendelea kuwataka masahaba wake waondoke na kumuacha peke yake kwa kusema: "Ninafahamu kwamba kesho tutakuwa na vita na wao. Hivyo ninaondoa baia (kiapo) chenu kwangu. Tumieni giza hili kwa ajili ya kuondoka na kuepukana na eneo hili la hatari. Hao watu wananitaka mimi tu, na watakaponipata mimi, hawatokuwa na shida na nyinyi." Mwisho wa kunukuuu. Baada ya Imam Hussein kutoa hotuba hiyo kila sahaba alitoa maelezo yenye kusisimua na yenye kuonyesha upendo wake wa hali ya juu kwa mjukuu huyo wa kizazi cha Nabii wa Allah, huku akiahidi kuendelea kuwa pamoja na Imam hadi mwisho wa uhai wake. Awali alianza Abbas Ibn Ali, (ndugu ya Imam Hussein) kwa kusema; "Kwa nini tukuache? Ili tuweze kuishi baada yako? Kamwe Mwenyezi Mungu asitujaalie kuiona siku kama hiyo." Baada ya Abbas vijana wengine katika familia ya Bani Hashim mmoja baada ya mwingine walitoa maneno kama hayo na kuahidi kuendelea kuwa pamoja na Imam Hussein (as).

Makaburi ya mashahidi wa Karbala

 

Baada ya watu wa familia ya Mtume kutoa baia (kiapo) kwa Imam, Muslim Bin Ausajah Asadi, alikuwa mtu wa kwanza kusimama na kutoa maneno yenye msisimko na upendo kwa kusema: "Ewe Abu Abdillah! Hivi kweli tunaweza kukuacha? Wakati huo (tukikuacha) tutatoa udhuru gani mbele ya Mwenyezi Mungu? Hapana, naapa kwa Mwenyezi Mungu! Kamwe hatutokuacha, sitaondoa mkono wangu kwako hadi nitakapotoa pigo kwa maadui na upanga wangu hautoanguka hadi pale utakapoangushwa na adui. Na baada ya hapo ikiwa sitokuwa na silaha, basi nitawapiga maadui kwa mawe. Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu kamwe sitotengana na wewe ili Mwenyezi Mungu ajue kwamba tumelinda hadhi na heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu! Nikujua kuwa nitauawa, kisha kufufuliwa, kisha nikachomwa moto na kuwa majivu na kwa mara nyingine nikafufuliwa na nikafanyiwa hivyo mara 70, kamwe sitotengana na wewe hadi pale nitakapoungana na msafara wako wa shahada. Na ni kwa nini nisifanye hivyo; ilhali nitauawa mara moja tu na kisha kupata utukufu na saada ya milele?" Mwisho wa kunukuu.

 

Ndugu wasikilizaji  ni vyema mfahamu kwamba, Muslim Bin Ausajah Asadi, alikuwa mmoja wa masahaba wakubwa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na pia sahaba wa Imam Ali bin Abi Twalib (as), huku akiwa mtukufu, mchaji-Mungu na mwenye zuhdi kubwa. Aidha Muslim alikuwa mpiganaji na mpanda farasi shujaa ambaye alikuwa akizungumziwa sana katika vita mbalimbali vya Kiislamu. Sahaba huyo alitoka kabila la Bani Asadi ambalo lilikuwa linaishi mjini Kufa, Iraq. Na ndiye ambaye alimuandikia barua Imam Hussein kutoka Kufa na baada ya Muslim Bin Aqil kuwasili mji huo, aliendelea kuchukua baia (kiapo) kutoka kwa wakazi wa Kufa. Aidha baada ya kushikwa Muslim Bin Aqil na Hani Bin Urwa na kuuawa shahidi alielekea kwa Imam Hussein pamoja na familia yake na kujiunga na mtukufu huyo.

Ndugu wasikilizaji, na kufikia hapa kipindi hiki kilichozungumzia fadhila na ubora wa masahaba wa Imam Hussein na imani yao thabiti, kilichokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio kinafikia tamati. Mimi ni Sudi Jafar Shaban kwaherini.

 

Sep 11, 2018 07:49 UTC
Maoni