Jan 19, 2019 07:14 UTC
  • Mchango wa ibra katika maisha ya mwanadamu

Hamu ya kutaka kubakia hai na kuishi daima humlazimisha mwanadamu kuchagua njia na mbinu bora zaidi za kuishi. Mwanadamu huwa kama mchoraji ambaye hufanya jitihada za kuchora picha na mchoro mzuri zaidi wa maisha yake.

Hufanya jitihada za kugundua vipawa na vipaji vyake kuujua ulimwengu unaomzunguka na muumba wake na kutafuta njia nzuri zaidi za kuwasiliana na wenzake. Hata hivyo kuishi maisha bora na mazuri si jambo rahisi kama wengi wanavyodhania, kwa sababu maisha ya mwanadamu hapa duniani yana panda shuka nyingi, misukosuko na milima na mabonde mengi yanayomlazimisha kuwa na masurufu ya kumuwezesha kukabiliana na changamoto zake.

Miongoni mwa mambo yanayomuwezesha mwanadamu kushinda matatizo na misukosuko ya maisha na kuchagua njia bora zaidi maishani mwake ni kudurusu, kusoma na kutafakari katika maisha ya watu na kaumu zilizotangulia na kuchukua ibra na mafunzo ambavyo huwa masurufu ya njiani katika safari ya maisha yake kuelekea Akhera. Naam, kutaamali na kutadabari katika maisha ya watu waliotangulia na kutumia tajiriba na uzoefu wao humpa mwanadamu uhai na maisha mapya. Tunapaswa kutumia vyema kipindi cha thamani cha maisha yetu mafupi kwa kupata ibra, mafunzo na darsa kutokana na maisha ya waliotutangulia. 

Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema akimuusia mwanaye, Hassan (as) kuhusu umuhimu wa kujifunza na kupata ibra kutokana na maisha ya waliotangulia kwamba: "Japokuwa mimi sijaishi muda mrefu kama waliokuwepo kabla yangu, lakini nimedurusu matendo yao, nikatafakari katika mambo yao na kupita katika athari na waliyoyabakisha hadi nikawa kama mmoja wao. Si hayo tu, bali kutokana na niliyoyasoma katika habari zao, nimekuwa kana kwamba nimeishi na wa mwanzo wao hadi wa mwisho wao..." (Nahjul Balagha, barua ya 31). 

Neno "ibra" kwa lugha ya Kiarabu linatokana na neno "'abara"  lenye maana ya kupita na kuvuka, kwa maana ya kupita kwenye mambo ya dhahiri ya matukio mbalimbali na kufika kwenye kina na ujumbe wa matukio hayo. Kupata ibra, darsa na somo kuna maana pana na kubwa. Historia ya kaumu zilizopita, kudhihiri na kutoweka kwa madola na tawala mbalimbali na kadhalika vyote vina ibra na somo kwetu. Kuyoyoma kwa umri na ujana na kuingia uzeeni ni mawaidha na somo tosha kwa kila mwenye akili na macho. Matukio ya watu waliopatwa na mashaka na kunusurika, wale waliokumbwa na misukosuko na mabalaa kisha wakapata raha na faraja yanatoa ibra na mafunzo kwetu. Vifo vinavyotokea kila siku vya ndugu, jamaa, wapendwa wetu au watu baki ni mawaidha na ibra. Matukio mbalimbali ya kimaumbile kama mitetemeko ya ardhi na mafuriko, mabadiliko ya kijamii na mambo mengine mengi vinatoa ujumbe na darsa ambazo iwapo mwanadamu atazitumia vyema zinaweza kuwa taa inayomulika njia yake na kumuelekeza katika bara ya amani. 

Imam Ali bin Abi Twalib: Kila pumzi unayovuta ni hatua moja kuelekea kwenye mauati.  

Hii leo tunawaona vijana katika jamii zetu waliopatwa na uraibu wa dawa za kulevya na uasherati na hatimaye kupoteza nishati na nguvu zao za ujana. Wako wasichana na wavulana ambao kutokana na kutekwa na mapenzi ya kijuujuu hujikuta wametumbukia katika ndoa zisizofaa na kupitisha sehemu muhimu ya umri wao katika mazonge na matatizo mengi. Utawaona wanafunzi wa vyuo vikuu waliochagua kozi za masomo bila ya kushauriana na wazazi na watalaamu na hatimaye kupoteza bure umri wao katika masomo na mambo ambayo hawana vipaji vyake au hayaoani na matakwa yao. Hii leo tunawaona watu mashuhuri na wale wanaojiita au kuitwa "celebrity" ambao kutokana na kupenda jaha, ukubwa na umashuhuri, hufanya mambo ya kushangaza ambayo hatimaye kuwatumbukiza katika kashfa, fedheha na aibu kubwa. Haya yote na mfano wake yanaweza kuwa ibra na mafunzo kwa mwanadamu.   

Wanadamu wenye akili, busara na maarifa huwa hawapiti haraka na bila ya kutafakari kandokando ya matendo, athari na historia ya kaumu zilizopita. Bali hutumia mambo hayo kwa ajili ya kupata ibra, darsa na mafunzo. "Huvuka" dhahiri ya mambo hayo na kuingia na kuzama ndani yake na kupata ujumbe na masomo yake. Kwa utaratibu huu watu hawa hufanya makosa machache mno ikilinganishwa na mafanikio yao maishani.

Majengo ya kale ya Takhte Jamshiid nchini Iran

Qur'ani tukufu pia imewahimiza wanadamu kutumia ibra kwa ajili ya kuwa na maisha bora na mazuri. Kitabu hicho kinasisitiza katika zaidi ya aya kwamba: Chukueni ibra enyi watu wenye kuona mbali, kama inavyosema aya ya 2 ya Suratul Hashr. Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu kimesimulia visa vingi vya Mitume na kaumu zilizopita na kuwataka wanadamu kutafakari na kuzama katika matukio yaliyojiri maisha mwao na kupata ibra na mafunzo. Mfano wa visa hivyo ni kile cha Nabii Sulaiman aliyepewa utajiri wa dunia nzima, akawa na uwezo wa kutumikisha watu na majini, akapewa uwezo wa kuzungumza na ndege na wanyama lakini kamwe hakughafilishwa au kutekwa na vyote hivyo, na daima alikuwa alijidhalilisha mbele ya Mola Muumba na Muweza na kufanya jitihada kubwa za kuwatumikia raia wake.

Kisa cha kaumu ya Nabii Lut iliyojihusisha na uchafu wa liwatwi na ushoga na kumsahau Mola Muumba na hatimaye ikaangamizwa kwa adhabu kali, kisa cha Nabii Mussa na Firauni, visa vya Qaruna, Nabii Ibrahim, Bibi Maryam na kadhalika vilivyotajwa katika sura za Qur'ani tukufu vyote vina ibra na mafunzo kwa wanadamu wenye macho na wenye kutafakari.

Lengo la Qur'ani tukufu kusimulia visa hivyo si kwa ajili ya kufurahisha barza na vikao, bali kwa ajili ya kutoa miongozo, masomo na ibra. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana katika visa hivyo Qur'ani tukufu imejiepusha kutaja mambo yasiyo na faida au yenye faida chache na kutosheka na yale yenye nafasi muhimu katika kutoa miongozo na mafunzo. Kwa mfano tu hutapata katika visa hivyo vya Qur'ani kukitajwa tarehe ya kuzaliwa au kufariki dunia au idadi ya watoto na wake wa Mitume wa Mwenyezi Mungu.

Miongoni mwa visa vya kuvutia mno ambavyo vimesimuliwa katika Qur'ani tukufu kwa ajili ya ibra na mafunzo ni kisa cha Nabii Yusuf (as). Baada ya kusimulia kisa hicho kwa mapana na marefu na kuashiria nukta muhimu na zinazotoa ibra, darsa na mafunzo tele kwa wanadamu, Qur'ani tukufu inafunga sura hiyo kwa kusema: Kwa hakika katika hadithi zao limo zingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyozuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyokuja kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.

Kisa cha Nabii Yusuf (as) kina makumi ya ibra, hekima na mafunzo yanayoweza kutoa mwanga na mwongozo katika maisha yetu ya kila siku. Miongoni mwa masomo hayo ni husda ya ndugu zake Yusuf na athari zake mbaya, jinsi ya kuzima njama na hila za maadui, kuthibitishwa utakasifu na usafi wa mienendo ya mtukufu huyo, kujiepusha na matamanio ya nafsi na vishawishi vya ngono, kashfa na fedheha ya Zuleikha, jinsi ya kuwakirimu na kuwatukuza wazazi wawili japo utakuwa na cheo na nafasi ya juu na mengine mengi yanayozungumziwa au kuashiriwa katika aya za sura hiyo. Aya hiyo iliyosomwa punde inawataka wanadamu wasisome na kusimulia visa vya kaumu zilizotangulia kwa ajili ya kufurahisha baraza, burudani na kadhalika bali kutafakati, kuchukua ibra na kupata mafunzo kuhusu maisha yao kwa ajili ya maisha yetu ya sasa.

Maoni