Sep 11, 2019 07:16 UTC

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika dakika hizi ambazo ndani yake tutazungumzia kuuawa shahidi Imam Ali bnil Husain Zaynul Abidin AS. Karibuni. ******

Mwezi 12 Mfunguo Nne Muharram, inasadifiana na siku alipouawa shahidi Imam Ali bnil Husain Zaynul Abidin AS ambaye moja ya lakabu zake ni Sajjad. Kila tunapomuangalia Imam Sajjad huwa anatukumbusha mapambano ya kishujaa ya baba yake mtukufu, Imam Husain AS katika jangwa la Karbala. Imam Sajjad AS alichukua jukumu la kuongoza umma wa Kiislamu mwaka 61 Hijria baada ya mapambano hayo ya Karbala na kuuawa shahidi kidhulma baba yake mtoharifu, Imam Husain AS. Imam Sajjad aliuawa shahidi kwa kupewa sumu mwaka 95 Hijria kwa amri ya Hisham bin Malik, khalifa wa wakati huo wa Bani Umayya. Kitu kikubwa zaidi kilichonukuliwa katika vitabu vya historia kuhusu Imam Sajjad AS ni ibada zake kubwa na sijda zake za muda mrefu mno hadi akapewa lakabu ya Sajjad, yaani mtu anayesujudu sana na kwa muda mrefu. Uchaji wake mkubwa wa Mwenyezi Mungu na wa sura ya kupendeza mno ulipelekea apewe lakabu nyingine pia ya Zaynul Abidin, yaani pambo la wachaji Mungu. Hata kuna baadhi ya watu wanadai kuwa Imam Sajjad AS alijitenga na masuala ya siasa na jamii na kujitenga pembeni kwa ajili ya ibada tu. Hata hivyo madai hayo si sahihi, kwani msimamo wa Imam Sajjad AS ulikuwa ni ule ule wa Maimamu wengine watoharifu; nao ni kupigania kusimama hukumu za Allah ardhini na kuimarika dini sahihi ya Uislamu. Imam huyo mtoharifu ambaye ni mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa na sifa zile zile za watu watukufu wa Mwenyezi Mungu, ushujaa, kupigania haki, kujishughulisha na masuala ya jamii ya Waislamu yakiwemo masuala ya siasa na uongozi na aliendelea na mapambano hayo ya kishujaa kwa muda wa miaka 35 hadi alipouawa shahidi akarejea kwa Mola wake kwa ufakhari mkubwa. Tunatoa mkono wa pole kwa mnasaba wa siku ya kukumbuka kuuawa shahidi mtukufu huyo.

 

Mwaka 61 Hijria, Imam Sajjad AS alikuwemo kwenye msafara wa baba yake Imam Husain AS kuelekea Kufa kwa ajili ya kuiokoa dini ya Uislamu. Muda mchache kabla ya kuwasili kwenye ardhi ya Karbala, Imam Sajjad AS alikumbwa na ugonjwa mkali sana alioendelea nao hadi siku kadhaa baada ya tukio la Ashura. Tab'an ugonjwa huo ndio uliopelekea awe mwanamme pekee aliyebakia hai katika msafara huo baada ya jinai kubwa zilizofanywa na wafuasi ya Yazid katika jangwa la Karbala, ikiwa hiyo ni hekima ya Mwenyezi Mungu SWT ya kumbakisha hai ili aweze kuendeleza njia tukufu ya Imam Husain AS katika kuhuisha dini tukufu ya Kiislamu na kuongoza umma wa Kiislamu. Jamii ya wakati huo ambayo kidhahiri ilionekana ya Kiislamu, ilikuwa inapita kwenye kipindi kigumu na nyeti mno. Tab'an hata baada ya kipindi hicho pia, kulishuhudiwa tawala za kidikteta na kiukandamizaji zikiwaongoza Waislamu, lakini wakati huo wa maisha ya Imam Sajjad AS na baada ya tukio la Karbla, hali ilikuwa ngumu na nyeti zaidi. Wakati huo matukufu ya Kiislamu yalishambuliwa bila kificho. Watu walikuwa wamezama katika upotofu kiasi kwamba hata hawakumuheshimu Bwana Mtume Muhammad SAW na walifikia kumchinja mjukuu wake Imam Husain AS. Ulimwengu wa Kiislamu wakati huo ulikuwa umeporomoka vibaya sana kifikra. Baada ya tukio la Ashura na kuuawa shahidi na kikatili mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW, watawala wa zama hizo akiwemo Yazid, waliona wazi kuwa tawala zao ziko hatarini, hivyo waliamua kutumia kila njia kulinda tawala zao. Moja ya mbinu walizotumia ilikuwa ni kujaribu kuwasahaulisha watu jinai walizofanya watawala hao madhalimu huko Karbala na vile vile kupotosha mapambano ya Karbla pamoja na kuyapunguzia umuhimu wake. Walizidisha ukandamizaji dhidi ya kila mfuasi wa watu wa nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW na kujaribu kuwafanya watu wabakie na majina tu ya Kiislamu lakini wasiwe na uthibitisho wowote wa kivitendo kuwa wao ni Waislamu. Wakati huo alihitajika mtu kama Imam Sajjad AS kuuokoa Uislamu na kuendeleza njia sahihi ya Bwana Mtume Muhammad SAW ambayo baba yake Imam Husain AS alimwaga damu yake kuilinda na kuifufua. Imam Sajjad AS aliamua kuwaongoza watu kupitia mafundisho yake matukufu katika dua na kunyenyekea kwa Mola wake. Alitumia fursa hiyo kuwa kigezo bora kwa watu wengine ili Waislamu waimarishe imani zao kivitendo na kupitia ibada.

 

Wasikilizaji wapenzi, kama tulivyotangulia kusema, sehemu kubwa iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Sajjad AS ni ucha Mungu wake mkubwa na ibada zake nyingi mno. Kitabu cha dua cha Sahifatu Sajjadia ni miongoni mwa urithi bora kabisa tulioachiwa Waislamu na mtukufu huyo. Imam Sajjad AS alitumia muda wake mwingi kuwalingania watu kujiepusha na madhambi. Hadithi nyingi zimepokewa kutoka kwa mtukufu huyo kuhusu suala hilo, hadithi ambazo zinaweza pia kuwa dawa ya kumzuia mtu na kufanya madhambi mazito kama ya kusengenya. Katika moja ya hadithi zake, Imam Sajjad (AS) amesema: "Mtu anayeuzuia ulimi wake usiwafedheheshe na kuwaharibia watu heshima zao, Mwenyezi Mungu atayafumbia macho madhambi yake Siku ya Kiyama".

Vile vile alikuwa akisisitiza mno suala la kutumia hekima katika kulingania watu dini. Pia wajibu wa kujua mbinu za kulingania dini ya Allah SWT. Katika hadithi moja iliyopokewa na Sheikh Kulaini katika kitabu cha al Kafi na kupokewa pia na maulamaa wengine wa Hadithi inasema: Mabwana kadhaa wa Kiquraish walimuuliza Imam Ali bin Hussain Sajjad AS kwamba: Tuwalinganie vipi watu dini hii? Imam Zainul Abidin AS aliwabainishia misingi ya dini na kuashiria kwamba misingi hiyo ni kuamini Utume wa Nabii Muhammad SAW. Aidha alisema: Mhimili wa nguzo zote hizo ni mambo mawili ambayo ni maarifa na kumjua Mwenyezi Mungu Mtukufu na kutafuta radhi Zake. Pia amenukuliwa akisema: Kumjua Mwenyezi Mungu ni kupwekesha Yeye na kutambua kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma, Mrehemevu, Mwenye nguvu na utukufu, Mwenye ilimu na kudra na kujua kwamba Yeye ni Muweza wa kila kitu Ambaye macho hayawezi kumuona lakini yeye anayaona macho na wenye macho. Kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu na kwamba Muhammad SAW ni mja na Mtume wake na aliyokuja nayo ni haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu SWT na yasiyo hayo ni batili na upotofu...."

Imam Sajjad Pia amenukuliwa akisema: "Mtu yeyote atakayeyafanyia kazi mambo manne yafuatayo, basi imani yake itakuwa kamilifu na Mwenyezi Mungu atakuwa radhi naye. Mosi, atekeleze ahadi na mikataba kati yake na watu wengine. Pili, awe mkweli katika maongezi yake. Tatu, atambue kuwa Mwenyezi Mungu anamwona katika kila hali kwa hivyo asifanye vitendo viovu. Na nne awe na akhlaki njema na kuifanyia wema familia yake."

 

Wapenzi wasikilizaji kama tulivyotangulia kusema, Imam Sajjad AS mbali na mawaidha na nasaha zake nyingi, alifanikisha malengo yake mengi kupitia dua na kunong'ona na Mola wake. Kama tulivyosema, kitabu cha Sahifatus Sajjadiyyah ni miongoni mwa urithi bora kabisa aliotuachia mtukufu huyo. Vile vile alihuisha na kubakisha hai kumbukukmbu za mashahidi wa Karbala na kuvirithisha vizazi vya baada yake, malengo makubwa ya Imam Husain AS katika mapambano yake huko Karbala. Siku moja mtu mmoja alimwendea Imam Sajjad AS na kumuuliza: Hivi majonzi na huzuni zako hazina mwisho? Imam akamjibu kwa kumwambia: Ole wako! Mtume wa Mwenyezi Mungu Yaakub AS ambaye mwanawe mmoja tu kati ya wanawe 13 ndiye aliyepotea, lakini alilia mno kwa kuwa mbali na mwanawe huyo mmoja kiasi kwamba hata alikuwa kipofu kutokana na kumlilia mwanawe Yusuf. Tena Yusuf alikuwa yuko hai! Lakini mimi nilishuhudia namna baba yangu, kaka yangu, maami zangu na watu 17 wa familia yangu wakiuawa kikatili mbele ya macho yangu. Vipi inawezekana majonzi na huzuni zangu kuwa na mwisho?!

*******

Kwa mara nyingine tunatoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuuawa shahidi Imam Sajjad AS. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Tags

Maoni