• Nyendo za Mtume SAW katika maisha ya Imam Khomeini MA

Assalaam Alaykum wasikilizaji wapenzi, karibuni kujiunga nami kwenye kipindi hiki maalumu ambacho kimetayarishwa kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kufariki dunia Imam Ruhullah Mussawi al Khomeini (MA) mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi tamati ya kipindi hiki, karibuni.

Tarehe 14 Khordad 1368 Hijria Shamsia inayosadifiana na tarehe 4 Juni 1989 ulimwengu wa Kiislamu ulimpoteza mtu mwenye maadili, akhlaki, ushujaa, utambuzi na imani na aliyeweza kusimama kidete kukabiliana na njama za mabeberu wote na hasa Marekani. Shakhsia huyo alikuwa pia mbeba bendera ya muqawama wa Kiislamu. Maisha yenye ikhlasi na ya ucha Mungu ya Imam Khomeini MA yaliweza kutoa mvuto maalumu uliotokana na nuru ya Mwenyezi Mungu na taathira chanya za Mtume Muhammad SAW. Imam Khomeini MA alikuwa shakhsia mwenye kufuata vigezo na nyendo za Mtume Mtukufu SAW, ambapo licha ya kukabiliana na utamaduni wa Kimagharibi na Kimashariki, alijenga moyo wa imani na umaanawi katika jamii ya Iran. Katika anga hiyo ya kimaanawi, vijana waliolelewa kiimani hawakusita hata kidogo kutoa rasilimali zao kubwa ambazo ni maisha yao yenye thamani kwa minajili ya kuunyanyua juu Uislamu. Wasikilizaji wapenzi, tukiwa tunakaribia siku za kubaathiwa na kupewa utume Mtume Mtukufu Muhammad SAW, tutafafanua kwa ufupi kwenye kipindi chetu hiki nyendo za shakhsia ya Imam Khomeini MA, ambaye alikuwa akifuata kikamilifu sira za Mtume SAW. Tunakuombeni muwe nami hadi mwisho wa kipindi ili tupate kusikiliza kwa pamoja sira na nyendo hizo za Imam Khomeini MA.

Imam Khomeini MA

 

Katika ulimwengu wa Magharibi, kazi za nyumbani zinaonekana kuwa ni shughuli isiyokuwa na umuhimu na maana yoyote, na hata wanawake wengi wanazichukulia kazi hizo kuwa zisizo na thamani na hivyo wanafandilisha kujishughulisha zaidi na kazi za nje. Imepokelewa riwaya kutoka kwa Mtume Muhammad SAW kwamba aliwauliza masahaba wake: 'Je, Ni wakati gani, mwanamke anakuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu?' Hakuna hata mmoja kati ya masahaba hao aliyeweza kujibu swali hilo, hadi pale alipojitokeza Bibi Fatimat Zahra Alayha Salaam binti kipenzi wa Mtume SAW na kujibu: 'Mwanamke huwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu wakati anapokuwa nyumbani na kufanya shughuli za kimaisha pamoja na kuwalea watoto'. Imam Khomeini alikuwa akifuata kikamilifu nyayo za Mtume Muhammad SAW. Daima alikuwa akitoa nasaha akiwa nyumbani na baadhi ya wakati watu waliomzunguka walikuwa wakimuuliza, je, ni kwa nini mwanamke anapaswa kubaki nyumbani? Alikuwa akijibu kwa kuwaambia: 'Msidharau kazi za nyumbani.  Suala la kulea watoto sio dogo, kama mtu atafanikiwa kutoa malezi bora kwa mtu mwingine atakuwa ametoa huduma kubwa katika jamii. Huruma na upendo wa mwanamke ni mkubwa zaidi na msingi pamoja na nguzo ya familia imesimama juu ya upendo'.  Imam Khomeini MA mwenyewe alikuwa msaidizi mkubwa kwa mkewe. Mke wa Imam Khomeini anasimulia kama ifuatavyo: "Kuna kipindi  watoto  wetu walikuwa wadogo na walikuwa  wakilia  sana nyakati za usiku, tulilazimika kukesha hadi asubuhi, hivyo Imam alipanga zamu, kwa mfano  masaa mawili alikuwa akiwaangalia watoto na mimi nikilala, na baada ya masaa mawili yeye alikuwa akilala na mimi kuchukua jukumu la kuwaangalia watoto."

Mtoto mwema ni matunda bora zaidi ya maisha. Kile ambacho wazazi wanapaswa kukitilia maanani ni kwamba kazi hazipasi kuwafanya waghafilike na jukumu la kuwalea watoto. Mtume Muhammad SAW anasema: 'Mtoto mwema, ni ua miongoni mwa maua ya peponi'. Kwa hivyo wazazi yaani baba na mama wanapasa kufanya juhudi za kuleta furaha, nguvu,  na ustawi kwa watoto wao.

Imam Khomeini MA alikuwa makini mno katika suala la kuwapa malezi bora watoto. Mmoja wa mabinti zake alimjia na kumlalamikia juu ya utundu wa mtoto wake, Imam alimpa jibu la kushangaza kwa kusema: 'Mimi niko tayari tubadilishane, thawabu za kustahamilia  utundu wa mtoto wako nipe mimi, na wewe uchukue thawabu za amali zangu zote.'   Mmoja wa watu wa karibu na Imam Khomeini MA anasema: 'Imam alikuwa akiamini kwamba mtoto lazima apewe uhuru, hadi atakapofikisha umri wa miaka saba na baada ya hapo lazima awekewe mipaka.'  Hali kadhalika anasema: 'Muwe wakweli kwa watoto wenu, ili nao wawe wakweli, kigezo cha mtoto ni baba na mama. Iwapo utaamiliana vyema na mtoto, atakuwa na tabia njema. Tekelezeni kila mnayoyasema mukiwa mbele ya watoto wenu.'

Mtume Mtukufu Muhammad SAW alikuwa mpole mno kwa watoto, mtukufu huyo alikuwa akiwabusu na kuwausia wengine wafuate mwenendo huo. Mtume Mtukufu amesema hivi kuhusiana na suala la kuwapenda watoto: "Kila mtu anayemfurahisha  binti yake mdogo, hupewa malipo ya kumuachia huru mtumwa miongoni mwa watoto wa Ismail. Na mtu anayemfurahisha mtoto wake mdogo wa kiume, huwa mithili ya mtu anayelia kutokana na hofu ya Mwenyezi Mungu na malipo ya mtu kama huyo ni pepo iliyo  juu kabisa."

Imam Khomeini alilipa umuhimu mkubwa sana suala la mshikamano na umoja baina ya Waislamu

 

Maisha ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW yalikuwa ya kawaida kabisa, na tunaweza kusema yalikuwa chini ya kiwango cha kawaida.  Imam Ali AS anatoa wasifu wa maisha ya Mtume SAW kwa kusema: "Wakati Mtume SAW alipokuwa akipewa mwaliko wa chakula, alikuwa akiketi chini na kula chakula hicho kwa kutumia mikono yake. Alikuwa mnyenyekevu kwa watu wake. Alikuwa akiwaheshimu watu na kukubali kutekeleza kazi na shughuli zilizokuwa ngumu." Imam Khomeini MA katika kipindi chote cha maisha yake, iwe ni wakati alipokuwa mwanafunzi wa kidini asiyejulikana katika Madrassa ya Faidhiyyah mjini Qum au wakati alipokuwa kiongozi wa mfumo wa Jamhuri ya  Kiislamu na marjaa wa Mashia duniani, alitosheka na maisha ya kawaida na ya chini na kamwe hakuwa tayari kubadilisha kiwango cha maisha yake, na  kuwa zaidi ya wananchi wa kawaida. Mmoja kati ya watu wa karibu na Imam Khomeini anasema: "Wakati Imam alipokuwa Najaf alikuwa akiishi kwenye nyumba ya kukodisha ambayo ilikuwa kuukuu na yenye kiwango kimoja na zile zilizokodishwa na watu wa kawaida na wanafunzi wa kidini.  Tunaweza kusema bila kusita kuwa, maisha ya Imam Khomeini yalikuwa katika kiwango cha mwanafunzi wa kawaida na hata chini kidogo ya hapo." Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuchukua jukumu la kuliongoza taifa la Iran, Imam Khomeini alikuwa akiishi kwenye nyumba ndogo hadi mwisho wa maisha yake, nyumba ambayo ilikuwa pambizoni mwa Husseiniya ya Jamaran, kaskazini mwa Tehran. Imam Khomeini  ambaye amevichukua vigezo vya maisha yake  kutoka kwa Mtume Mtukufu SAW, hakutoa fursa ya kufanyiwa marekebisho makubwa wala madogo nyumba hiyo, na hata wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam Hussein wa Iraq dhidi ya Iran, Imam aliendelea kubaki kwenye nyumba hiyohiyo hata wakati ndege za Iraq zilipokuwa zikiushambulia kwa mabomu mji wa Tehran. Jambo la kushangaza hapa ni hili kwamba, Imam Khomeini alikuwa akiwapokea na kuwakaribisha kwa mazungumzo wageni mbalimbali wakiwemo marais na mawaziri wa nchi mbalimbali kwenye chumba kidogo na cha kawaida kabisa, ambacho hakikuwa na fanicha wala samani zozote zile.

Unyenyekevu na usikivu ni miongoni mwa nyendo za Mtume Mtukufu SAW. Mtume Mtukufu SAW kamwe hakukaa sehemu maalumu wakati alipokutana na masahaba zake, bali alikuwa akizungumza nao akiwa ameketi mahala pa kawaida tu. Kamwe hakuwa mtu wa ghadhabu na hasira mbele ya jamii, bali alikuwa akifanya dhihaka na watu ili waweze kuwa huru na kueleza matatizo yao bila ya woga na hofu mbele ya kiongozi wao. Imam Khomeini naye alikuwa akifuata nyendo hizohizo. Ijapokuwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hayangekuwa na maana bila ya uongozi wake, amma unyenyekevu wa Imam Khomeini kamwe haukumfanya hata mara moja kulalamikia ugumu wa kazi zake. Mara zote alikuwa akijitambulisha mbele ya wananchi kuwa ni mtoa huduma kwa wananchi na kusema:  'Kama mkiniita mtoa huduma, ni bora zaidi kuliko mkiniita kiongozi.'

Naam wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu maalumu cha kukumbuka siku ya kufariki dunia Imam Khomeini MA mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran umefikia tamati.  Ni matarajio yetu kuwa mumenufaika vya kutosha kwa haya tuliyokuandalieni.

Wassalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.

 

Tags

Jun 05, 2017 09:27 UTC
Maoni