Jul 25, 2016 14:03 UTC
  • Waziri Mkuu wa Tanzania awataka mawaziri kuhamia Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa agizo kwa mawaziri na manaibu wote wahame mara moja kutoka Dar es Salaam na kuelekea Dodoma ambako kimsingi ndio makao makuu ya serikali.

Mandhari ya mji wa Dodoma

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema atahamia Dodoma ifikapo Septemba mwaka huu kuonyesha kuwa Serikali imedhamiria kutekeleza ahadi ilizotoa kwa wananchi. Majaliwa ametoa kauli hiyo leo  wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma na kuwashukuru kwa ushiriki wao kwenye maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yalizofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, mjini Dodoma.

Waziri Mkuu wa Tanzania amewataka wakazi wa Dodoma watumie fursa hiyo kutunza amani ya nchi na kudumisha umoja uliopo. Vilevile amewataka watumie fursa hiyo kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na hoteli za kitalii ili watu, watumishi na wageni wanapokwenda Dodoma wasipate taabu mahali pa kuishi.

Rais wa Tanzania, Dakta John Pombe Magufuli

Wakati huo huo, mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya leo ya Siku ya Mashujaa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.John Magufuli amerudia kusisitiza nia ya Serikali kuhamia  Dodoma katika kipindi chake cha uongozi ili kutekeleza ndoto ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kutaka makao makuu ya nchi yawe Dodoma.

Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Dodoma kwenye uwanja wa Mashujaa, Rais Magufuli amesema kuwa, atahakikisha Dodoma inakuwa makao makuu ndani ya miaka minne na miezi minne iliyobakia kwenye awamu ya kwanza ya uongozi wake.

Rais Magufuli akisalimiana na baadhi ya viongozi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Mashujaa

Aidha akihutubia katika maadhimisho hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametawaka Watanzania kuwaenzi kwa dhati mashujaa kwa kudumisha amani, umoja na utulivu uliojengwa na mashujaa hao.

 

Tags