Mar 05, 2016 07:36 UTC
  • Katibu Mkuu mstaafu wa EAC ataka wananchi wamuunge mkono Magufuli

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) aliyemaliza muda wake, Dk Richard Sezibera amewataka wananchi kuunga mkono jitihada za kupambana na rushwa zinazofanywa na viongozi wa jumuiya hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake wa sasa, Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dakta Sezibera aliyemaliza muda wake hivi karibuni na nafasi yake kuchukuliwa na Liberat Mfumukeko wa Burundi amesema kuwa, ili tatizo la rushwa limalizike, hatua za dhati za kufichua wala rushwa zinazofanywa na viongozi wakiongozwa na Rais Magufuli anayepambana bila woga kukabili watendaji wanaotumia vibaya madaraka na fedha za umma zinapaswa kuungwa mkono. Amesema kuwa, kuna umuhimu wa kila mwananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kukataa tabia ya rushwa na ufisadi ili kuwaunga mkono viongozi walioonesha uthubutu kukataa vitendo vya rushwa.

Katikati ya wiki hii, akiwa mjini Arusha kuongoza kikao cha wakuu wa umoja huo, Rais Magufuli alieleza jinsi rushwa inavyorudisha nyuma maendeleo na kuwataka viongozi wengine wa jumuiya hiyo kuungana `kutumbua majipu’ ya watendaji wanaojinufaisha kutokana na rasilimali za umma, badala ya kuwatumikia wananchi ambao wengi wao ni masikini.

Tangu aingie madarakani nchini Tanzania mwaka jana, Rais John Pombe Magufuli amechukua hatua kadhaa za kupambana na ufisadi ikiwemo kuwafuta kazi maafisa wa mashirika waliohusishwa na tuhuma za ufisadi nchini Tanzania.

Tags