Jan 09, 2018 15:50 UTC
  • Lowassa ampongeza Rais Magufuli wa Tanzania, asema amefanya kazi nzuri

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA katika uchaguzi wa mwaka 2015 nchini Tanzania, Edward Lowassa leo amekutana na Rais John Magufuli wa nchi hiyo na kumpongeza kwa kazi nzuri iliyofanywa na serikali yake tangu aliposhika madaraka.

Akizungumza na waandishi habari katika Ikulu ya Rais Jijini Dar es Salaam Lowassa ameelezea namna anavyoiona Tanzania ya miaka mitano ijayo.

Amesema anaiona Tanzania yenye matumaini mapya kwa Watanzania. Edward Lowassa ambaye alichuana vikali na Rais Magufuli katika uchaguzi wa rais wa Oktoba 2015 nchini Tanzania amesema hayo wakati anajibu swali ambalo ameulizwa na waandishi habari kuhusu jinsi anavyoiona Tanzania ya miaka mitano ijayo?

Vilevile amempongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na ametaja baadhi ya maeneo ambayo kazi kubwa imefanyika kuwa ni kutoa elimu bila malipo, ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji, ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambavyo vinazalisha ajira nyingi kwa Watanzania.

Lowassa akiwa na Rais Magufuli wa Tanzania, Ikulu ya Dar es Salaam

Kwa upande wake Rais Magufuli amempongeza Edward Lowassa kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali na amesema Mhe. Lowassa ni mmoja wa viongozi ambao kwa wakati wake ametoa mchango wake katika nchi.

Rais Magufuli ameongeza kuwa Lowassa ni mwanasiasa mzuri na kwamba hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita wa kugombea kiti cha Urais, hakuwahi kumtukana.

Tags