Feb 07, 2018 08:07 UTC
  • Ecowas yawawekea vikwazo makumi ya wanasiasa wa Guinea-Bissau

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika Ecowas imetangaza kuwawekea vikwazo wanasiasa na wafanyabishara 20 wa Guinea-Bissau ikiwatuhumu kuwa wanakwamisha jitihada za kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo kwa muda mrefu sasa.

Katika taarifa, Ecowas imesema vikwazo hivyo vinajumuisha zuio la kusafiri pamoja na kuzuiwa kwa mali za shakhsia hao wa kisiasa, akiwemo mtoto wa kiume wa rais, Emerson Goudiaby Vaz.

Jumuiya hiyo ya kikanda imesema imechukua hatua hiyo kutokana na hatua ya mwezi jana ya Rais Jose Mario Vaz wa nchi hiyo kumteua  Augusto Antonio Artur da Silva kuwa Waziri Mkuu wa nchi, jambo ambalo linakiuka makubaliano ya amani ya mwaka 2016. 

Wafuasi wa vyama vya upinzani nchini Guinea Bissau wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara ya kushinikiza kujiuzulu serikali ya Rais Jose Mario Vaz wa nchi hiyo.

Maandamano ya wafuasi wa upinzani dhidi ya serikali mjini Bissau

Mgogoro wa kisiasa nchini Guinea Bissau uliibuka Agosti mwaka 2015 baada ya Rais José Mário Vaz kumuuzulu Waziri Mkuu Domingos Simoes Pereira na kumchagua mtu mwingine kushika wadhifa huo.

Rais  Vaz alimuuzulu Pereira akimtuhumu kwa ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma;  tuhuma ambazo zilikanushwa vikali na makundi ya kisiasa ambayo ni wafuasi wa mwanasiasa huyo.

Tags