Mar 01, 2018 15:31 UTC
  • Maelfu ya wahajiri walioko Libya kurejea kwao Gambia

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limetangaza kuwa shirika hilo lina mpango wa kuwarejesha kwao Gambia maelfu ya wahajiri waliokwama nchini Libya.

Shirika hilo limesema, maelfu ya wahajiri haramu raia wa Gambia watarejeshwa nchini kwao baada ya kupata matatizo mengi magumu ikiwa ni pamoja na kufungwa jela nchini Libya.

Vile vile limesema, mwaka 2017, raia elfu mbili na 500 walioingia Libya kinyume cha sheria walikuwa wamefungwa katika jela za nchi hiyo na hivyo kuyeyuka ndoto zao za kufika barani Ulaya.

Tamaa mbele mauti nyuma, watu wanaoacha nchi zao kwa ajili ya kukimbilia maisha bora Ulaya huishia kwenye magenge maovu nchini Libya

 

Miongoni mwa masaibu yaliyowakumba wahajiri hao haramu ni kupigwa mnada na kuuzwa kama bidhaa katika masoko ya Libya.

Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji inaonesha kuwa, hata kurejea maelfu ya wahamiaji hao nchini kwao Gambia kuna matatizo mengi kwao kwani kiwango cha ukosefu wa kazi katika nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika ni asilimia 40.

Libya ndiyo njia kuu inayotumiwa na wahajiri haramu kutoka nchi mbalimbali hususan za Afrika kwa atamaa ya kufika Ulaya ambako wanadangaywa kuwa kuna maisha mazuri. 

Tags

Maoni