Mar 05, 2018 12:49 UTC
  • Hali mbaya ya wakimbizi wa Libya; kushindwa asasi za ndani na za kimataifa

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu inayowakabili wakimbizi wa Libya katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Ripoti zinaonyesha kuwa, mamia ya maelfu ya wakimbizi ndani ya Libya wanahitajia misaada ya dharura ya kibinadamu.

Maria do Valle Ribeiro, mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa alitangaza hivi karibuni kwamba, zaidi ya raia laki moja na elfu themanini wa Libya wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na hofu ya ukosefu wa usalama na machafuko yanayoendelea kushuhudiwa katika nchi yao. Aidha kwa mujibu wa mratibu huyo wa masuala ya misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ni kuwa, takribani wakimbizi laki tatu na 35 elfu ambao hivi karibuni walirejea katika miji na vijiji vyao, wanahitajia misaada ya kibinadamu.

Libya ingali inasubiria itifaki ya kitaifa ambayo kidhahiri inaonekana kuwa, si watu wa ndani wenye nafasi muhimu katika matukio ya kisiasa ya nchi hiyo wala wale wa kigeni ambao wameweza kulitekeleza hilo. Katika mazingira kama haya, wananchi wa Libya ndio ambao wamekuwa wahanga wakuu wa ukosefu wa amani na usalama pamoja na hali mbaya ya ukosefu wa uthabiti wa kisiasa.

Maria do Valle Ribeiro, mratibu wa masuala ya kibginadamu wa Umoja wa Mataifa

Moja ya matokeo mabaya ya hali hiyo mbaya ya kisiasa na kiusalama ya Libya ni kuwa wakimbizi raia wa nchi hiyo ndani ya nchi yao au wengine kulazimika kuikimbia nchi kwa kutumia boti wakitaka kuvuka maji ya Bahari ya Mediterenia ambapo aghalabu hatima na majaaliwa yao huwa ni kufa maji. Licha ya kuwa Baraza la Uongozi la Libya mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Februari  lilitoa idhini ya kurejea wakimbizi katika miji na vijiji vyao na hata maelfu ya wakimbizi hao wakafunga safari na kuanza kurejea katika makazi yao, lakini makundi ya wabeba silaha yaliwazuia na kuwa kikwazo kwao.

Kwa hakika uwepo wa makundi ya wabeba silaha nchini Libya ni moja ya sababu kuu za wananchi wa nchi hiyo kuyahama makazi yao na kulazimika kuwa wakimbizi. Licha ya kuwa, hakuna  takwimu za kuaminika kuhusiana na idadi kamili ya makundi ya wabeba silaha nchini Libya,  lakini inaelezwa kuwa, idadi ya makundi hayo inafikia 1700,

Cécile Pouilly, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ametangaza kuwa, kushadidi vitendo vya utumiaji mabavu na mapigano baina ya makundi ya wabeba silaha katika maeneo mbalimbali ya Libya kumekuwa chanzo cha wananchi wa nchi hiyo kuwa wakimbizi na filihali hakuna uwezekano wa kurejea wakimbizi hao katika makazi yao.

Cécile Pouilly, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR)

Hapana shaka kuwa, uwepo wenye wigo mpana wa makundi ya wabeba silaha ya Libya unatokana na kutokuweko serikali ya kitaifa yenye nguvu katika nchi hiyo. Kimsingi ni kuwa, kutokuweko serikali ya kitaifa yenye nguvu nchini Libya ni moja ya sababu kuu za kuibuka wimbi la wakimbizi katika nchi hiyo. Wasiwasi wa usalama na uhaba wa vyanzo vya fedha ni jambo jingine ambalo limezifanya asasi zenye mfungamano na Umoja wa Mataifa zishindwe kuwasaidia wakimbizi ndani ya Libya.

Mjumuiko wa mazingira haya umeandaa uwanja wa kuibuka na kushika kasi biashara chafu kama ya magendo ya binadamu na utumwa nchini Libya. Magenge yanayojihusisha na magendo ya binadamu yamekuwa yakitumia vibaya hali ya shaghalabaghala na mparaganyinyiko inayohushudiwa nchini Libya kushadidisha hali mbaya ya wakimbizi. Akthari ya raia wa Libya wanafadhalilisha kuikimbia nchi yao kuliko kubakia katika mazingira hayo mabaya ya ukosefu wa usalama.

Pamoja na kuwa vita vya kuwania madarakana baina ya makaundi mbalimbali ya Libya vimekuwa na nafasi kubwa katika kuvuruga hali ya kisiasa, kiusalama na kuwafanya raia wa nchi hiyo kuwa wakimbizi, lakini walimwengu hawapaswi kughafilika na nafasi ya madola makubwa ya Magharibi katika mgogoro wa nchi hiyo na hata hali mbaya inayotawala hivi sasa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Tags