Mar 26, 2018 15:11 UTC
  • Magufuli awajibu maaskofu, awataka wahubiri viwanda na si mambo mengine

Rais John Magufuli wa Tanzania amejibu mapigo ya maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) akiwataka viongozi hao wahubiri kuhusu ujenzi wa viwanda vya dawa nchini humo ili Tanzania isinunue dawa nje ya nchi, badala ya kuhubiri mambo mengine.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Machi 26, 2018 katika hafla fupi ya ugawaji wa magari 181 ya Bohari Kuu ya Dawa nchini Tanzania (MSD) kwa ajili ya kusambaza dawa maeneo mbalimbali nchini humo.

Amesema kununua dawa nje ya nchi kunasababisha nchi kupoteza Sh bilioni 500. Amesisitiza kuwa asilimia 94 ya dawa zinanunuliwa nje ya nchi.  

Matamshi haya ya Rais John magufuli wa Tanzania yametolewa siku kadhaa baada ya Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri chini Tanzania (KKKT) kumesema kuwa, umoja na amani ya Tanzania viko hatarini. Baraza hilo limeoredhesha mambo kadhaa ambayo limeyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya Tanzania.

Waraka uliotolewa na baraza hilo umeyataja baadhi ya mambo hayo kuwa, ni pamoja na utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.

Tags