Jun 30, 2018 04:08 UTC
  • Salva Kiir atangaza usitishaji vita wa kudumu Sudan Kusini

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ametangaza usitishaji vita wa kudumu kote nchini humo.

Salva Kiir amesema kuwa vita vinasimamishwa daima katika maeneo yote ya Sudan Kusini hadi litakapotolewa tangazo jingine. 

Hata hivyo amelitaka jeshi la nchi hiyo kuwa macho na kuhifadhi haki ya kulinda nchi.

Alkhamisi iliyopita Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan,  Al-Dardiri Mohammed Ahmed alitangaza kuwa pande mbili hasimu katika nchi jirani ya Sudan Kusini zimefikia makubaliano ya kusitisha mapigano na vita vya ndani. 

Salva Kiir kulia na Riek Machar kushoto.

Mazungumzo kati ya mahasimu wawili wa kisiasa yaani Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na makamu wake wa zamani, Riek Machar kwa ajili ya kufikia mapatano ya kusitisha vita na kukomesha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalianza Jumanne iliyopita katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum chini ya upatanishi wa Rais wa Sudan, Omar al Bashir. 

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kutokana na mashinikizo na ushawishi wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Nchi hiyo changa zaidi duniani ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013 baada ya kiongozi wa sasa wa nchi hiyo, Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kuwa alifanya jaribio la kupindia serikali yake. 

Tags

Maoni