Jul 01, 2018 07:22 UTC
  • Rais wa Gambia alifanyia mabadiliko baraza la mawaziri

Rais Adama Barrow wa Gambia amelifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri sanjari na kumteua makamu wake mpya.

Katika mabadiliko hayo, Barrow amemjumuisha katika baraza hilo waziri mmoja aliyehudumu katika enzi za mtangulizi wake, Yahya Jammeh.

Momodou Tangara ameteuliwa kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Rais wa Gambia amemteua Ousainou Darboe, mkuu wa chama cha United Democratic Party UDP kuwa makamu wake, kuja kurithi mikoba ya Fatoumata Tambajang, ambaye sasa atahudumu kama mwanadiplomasia nje ya nchi.

Wadadi wa mambo wanasema mabadiliko hayo katika baraza la mawaziri yanaonesha kuwepo mpasuko mkubwa ndani ya muungano tawala nchini humo, huku vyama tanzu kwenye muungano huo vikivutana huku na kule.

Aliyekuwa rais wa Gambia Yahya Jammeh akiondoka nchini

Itakumbukwa kuwa, baada ya kuchachamaa kwa muda na kukataa kukabidhi hatamu za uongozi wa nchi, aliyekuwa rais wa Gambia Yahya Jammeh hatimaye alikubali matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Desemba Mosi mwaka 2016 na kungátuka madarakani, kufuatia mashinikizo ya kieneo na kimataifa.

Jammeh, ambaye aliitawala Gambia kwa muda wa miaka 22 aliondoka nchini humo kufuatia hali hiyo na sasa yuko uhamishoni nchini Equatorial Guinea.

 

Tags

Maoni