Nov 15, 2018 14:05 UTC
  • UN: Kuna nakisi ya bajeti kwa ajili ya kikosi cha kusimamia amani magharibi mwa Afrika

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, unakabiliwa na nakisi ya bajeti kwa ajili ya kikosi chake cha kusimamia amani katika eneo la magharibi mwa Afrika.

Taarifa ya umoja huo imeeleza kuwa, askari wake wanaosimamia amani katika maeneo ya magharibi mwa Afrika wanakabiliwa na nakisi kubwa ya bajeti.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa ni kuwa, nakisi hiyo ya bajeti imetokana na nchi wafadhili kutotekeleza ahadi zao za kukisaidia kikosi hicho cha kusimamia amani.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa, nchi wafadhili zimetoa kiwango cha chini ya nusu ya ahadi zao ziliotoa kwa ajili ya kukisaidia kikosi cha kusimamia amani huko magharibi mwa Afrika.

Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa ambacho kinaundwa na nchi tano za magharibi mwa Afrika kimekuwa na jukumu la kukabiliana na makundi ya kigaidi katika eneo hilo.

Wanamgambo wa Boko Haram

Nchi za eneo la magharibi na Sahel Afrika katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa usalama kutokana na kuwa uwanja wa mashambulio ya kigaidi.

Mgogoro wa kaskazini mwa Mali na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram ni sehemu tu ya changamoto kubwa yya usalama inayozikabili nchi za magharibi mwa Afrika.

Mashambulio hayo hadi sasa yamesababisha mamia ya raia na wanajeshi kuuawa huku mamia ya maelfu ya raia wakilazimika kuwa wakimbizi.

Tags