Nov 27, 2018 15:10 UTC
  • Magufuli: Wapinzani watulie la sivyo wataishia gerezani

Rais John Magufuli wa Tanzania amempa ujumbe Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Edward Lowasa awaambie viongozi wengine wa vyama vya upinzani kwamba watulie “la sivyo wataishia magerezani”.

Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Novemba 27, katika uzinduzi wa maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) baada ya kumsifia Lowassa, kuwa ni mwanasiasa mstaarabu ambaye alionyesha utulivu hata baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa urais mwaka 2015. Rais wa Tanzania amesema vyama vya siasa havipaswi kuwa chanzo cha kututenganisha bali viwe chachu ya maendeleo, hivyo washauri unaowaongoza watulie, la sivyo wataishia kwenye magereza ili wakajifunze namna ya kuheshimu sheria za nchi".

Hadi sasa, viongozi kadhaa wa upinzani nchini Tanzania hasa Chadema wana kesi za aina tofauti katika mahakama mbalimbali; baadhi wakishtakiwa kwa uchochezi, wengine kwa kutoa maneno yasiyofaa dhidi ya Rais na wengine kwa kufanya mikusanyiko bila ya kibali.

Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko walifutiwa dhamana mahakamani Kisutu kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili ya kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria, uchochezi na uasi.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Wengine wanaoshtakiwa katika kesi hiyo, ni Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji, Naibu Katibu MKuu Bara, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mch. Peter Msigwa, John Heche, Halima Mdee, Esther Bulaya.

Jana pia Mahakama ya Kisutu ilielezwa kuwa upelelezi wa kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe umekamilika na sasa itaanza kusikilizwa mahakamani.

Tags