Mar 06, 2019 07:20 UTC
  • UN: Burkina Faso inasumbuliwa na ongezeko la wakimbizi

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, idadi ya wakimbizi wanaosumbuliwa na machafuko ya ndani nchini Burkina Faso imeongezeka na kufikia zaidi ya watu laki moja.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema kuwa, zaidi ya nusu ya wakimbizi hao wamelazimika kukimbia makazi yao katika miezi miwili ya mwanzoni mwa mwaka huu wa 2019.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Wakimbizi, Ursula Mueller amesema kuwa wimbi kubwa la wakimbizi limeitumbukiza Burkina Faso katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo. 

Taarifa za Umoja wa Mataifa zinasema kuwa, karibu raia laki tisa wa Burkina Faso wameathiriwa sana na mgogoro wa ndani na kwamba kunahitajika kiasi cha dola milioni mia moja kwa ajili ya misaada ya watu hao. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, zaidi ya shule 1100 za Burkina Faso zimefungwa kutokana na ghasia na machafuko ya ndani na wanafunzi laki moja na 57 elfu wamelazimika kuacha masomo. 

Vilevile raia karibu laki saba wa nchi hiyo wanasumbuliwa na uhaba wa chakula, na watoto laki moja na 30 elfu wanakabiliwa na utapiamlo.

Tangu mwaka 2015 Burkina Faso inasumbuliwa na mashambulizi ya wanachama wa kundi la Boko Haram hususan katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na nchi za Niger, Mali na Benin.   

Tags