Apr 06, 2019 07:50 UTC
  • Kiongozi wa upinzani Sudan amtaka Rais Bashir ajiuzulu

Kiongozi wa kambi ya upinzani nchini Sudan amemtaka Rais Omar Hassan al-Bashir wa nchi hiyo ajiuzulu.

Sadiq al Mahdi, kiongozi wa chama cha Umma cha Sudan amemtaka Rais Bashir mbali na kuachia ngazi, abatilishe sheria ya hali ya hatari sanjari na kuzivunja taasisi zote za kikakatiba.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mpinzani mkuu wa serikali ya nchi hiyo ametoa mwito wa kuundwa baraza la mpito la watu 25, litakalopewa jukumu la kuiongoza nchi hadi uchaguzi ufanyike.

Al Mahdi ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu nchini humo amebainisha kuwa, aliyasema hayo jana Ijumaa wakati wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Omdurman ambao ni wa pili kwa ukubwa baada ya Khartoum na kufafanua kuwa, huu ndio wakati wa mabadiliko kwani maandamano ya wananchi nchini Sudan yametokana na kurundikana matatizo mengi juu yao.

Sudan imekumbwa na maandamano tangu katikati ya mwezi Disemba 2018 na chanzo cha maandamano hayo kilikuwa ni kulalamikia kupanda bei za bidhaa muhimu hasa mkate na mafuta.

Wasudan wakishiriki maandamano mjini Khartoum

Maandamano hayo yameenea nchi nzima na sasa waandamanaji wanataka Rais Omar al Bashir aong'oke madarakani baada ya kuitawala nchi hiyo kwa takriban miaka 30 sasa, yaani tangu tarehe 30 Juni 1989.

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International, makumi ya watu wameshauawa na kujeruhiwa kutokana na ukandamizaji wa vikosi vya serikali ya nchi hiyo.

Tags