Apr 08, 2019 14:58 UTC
  • Serikali ya Sudan yatishia kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo

Serikali ya Sudan imetahadharisha kuhusu kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo na kugawanyika mapande mawili muundo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Waziri wa Habari wa Sudan, Hassan Ismail, ametoa tahadhari hiyo katika mahojiano aliyofanyiwa na mtandao wa habari wa al Shuruq na kuzituhumu taasisi na jumuiya za kigeni kuwa zinagharamia kifedha maandamano ya wapinzani wanaomtaka Rais Omar al Bashir ang'oke madarakani.

Waziri huyo wa Sudan aidha amewatuhumu wapinzani kuwa wamekataa kufanya mazungumzo na serikali akisema, kwa muda wa siku kumi sasa wapinzani na waitifaki wao wanatumia mbinu mbalimbali za kumimina mitaani wafuasi wao kwa shabaha ya kuiangusha serikali iliyoko madarakani.

Rais Omar al Bashir wa Sudan

 

Ameonya kuhusu hatari ya kutokea vita vya ndani nchini Sudan akisisitiza kwamba njia pekee ya kuiokoa nchi hiyo isitumbukie kwenye shimbo la kambi mbili za kisiasa ni kufikiwa mapatano baina ya wanasiasa na kuiepusha Sudan na vurugu na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Tangu tarehe 19 Disemba 2018 hadi hivi sasa Sudan imetumbukia kwenye dimbwi la maandamano makubwa ya wananchi wanaotaka Rais Omar al Bashir ang'oke madarakani. Cheche ya maandamano hayo ilitokana na kulalamikia kupanda bei za bidhaa na mahitaji muhimu ya watu hasa mkate na mafuta.

Kwa mujibu wa shirika la Human Rights Watch, watu wasiopungua 37 wameshauawa katika maandamano hayo hadi hivi sasa.

Tags