Apr 11, 2019 01:02 UTC
  • Maelfu ya watu wawa wakimbizi kutokana na mapigano nchini Libya

Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba mapigano ya hivi sasa ya nchini Libya yameshapelekea watu 4500 wa nchi hiyo kuwa wakimbizi.

Umoja huo umesema kuwa, mapigano yaliyoanzishwa na wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli, yamepelekea watu 4500 kukimbilia kwenye viunga vya mji mkuu huo wa Libya hadi hivi sasa.

Wapiganaji wa Khalifa Haftar wamepiga kambi katika umbali wa kilomita mbili kusini mwa Tripoli na wamefunga barabara ya kuelekea mjini humo kwa magari ya deraya yenye bunduki za rashasha.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Tripoli Libya wakitafuta sehemu salama ya kukimbilia

 

 

Watu walioshuhudia wamesema kuwa, ndege za ijeshi za Khalifa Haftar zimeruka juu ya anga ya Tripoli na kumesikika sauti za miripuko katika viunga vya mji huo.

Umoja wa Mataifa umelazimika kuakhirisha mkutano wa amani wa Libya uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 14 hadi 16 mwezi huu wa Aprili baada ya kuzuka mapigano hayo.

Siku ya Alkhamisi ya tarehe 4 Aprili, Jenerali Khalifa Haftar alitoa amri kwa wafuasi wake kuushambulia mji mkuu wa Libya, Tripoli, na kuwataka wakazi wa mji huo wajisalimishe kwake.

Fayez Mustafa al Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa na jamii ya kimataifa ametoa amri ya kukabiliana na vitisho vyovyote vinavyotolewa na Khalifa Haftar.

Tags