Apr 28, 2019 01:14 UTC
  • Watu 39,000 wakimbia makazi yao kufuatia mapigano Tripoli, Libya

Kufuatia kushadidi mapigano katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, watu 39,000 wameripotiwa kukimbia makazi yao katika mji huo.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, kuendelea mapigano mjini humo kunaweza kuibua maafa ya kibinadamu. Aidha ameashiria ripoti za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR na kusema tokea mapigano mapya yaanze mjini Tripoli mapema mwezi huu watu 39,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kushambulia makazi ya raia kwa kutumia mizinga na maroketi ni jambo lisilokubalika. Ametoa wito kwa pande zinazozozana kulinda maisha ya raia.

Jenerali muasi nchini Libya, Khalifa Haftar alianzisha oparesheni ya kutaka kuuteka mji wa Tripoli mnamo Aprili nne. Jenerali huyo anaaminika kupata uungaji mkono wa Ufaransa, Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Khalifa Haftar

Siku kadhaa kabla Haftar kuanzisha hujuma dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli, Saudi Arabia ilikuwa imekabidhi mamilioni ya dola ili kutekeleza oparesheni hiyo.

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao makuu yake mjini Tobruk, iliyo karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.

Tags