Apr 28, 2019 07:14 UTC
  • Wahajiri 16 wa Kiafrika waaga dunia katika ajali ya barabarani Morocco

Kwa akali wahajiri 16 wanaotoka katika nchi za eneo la chini ya Jangwa la Sahara wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea katika eneo la Melilla, kaskazini mwa Morocco.

Shirika la habari la serikali ya nchi hiyo MAP limeripoti kuwa, ajali hiyo ilitokea jana Jumamosi, baada ya gari lililokuwa limewabeba wahajiri hao haramu kubingiria na kutumbukia kwenye dimbwi la kilimo cha unyunyizaji maji katika eneo hilo.

Shirika hilo limeongeza kuwa, watu wengine 17 wamejeruhiwa katika ajali hiyo na kukimbizwa katika hospitali ya eneo hilo la Melila, ambalo ni moja kati ya maeneo mawili ambayo yanahesabiwa kuwa mpaka wa pekee wa ardhini kati ya Ulaya na kaskazini mwa Afrika.

Hata hivyo shirika la kutetea haki za binadamu la Moroccan Association of Human Rights limeripoti kuwa, waliofariki dunia katika ajali hiyo ni wahajiri 19, na kwamba gari hilo lilikuwa limebeba wahajiri haramu 50.

Wahajiri haramu waliokamatwa nchini Morocco

Vyombo vya usalama nchini humo vimesema kuwa vimeanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo, sambamba na kutambua uraia wa wahajiri hao.

Mapema mwaka huu, serikali ya Morocco ilisema imezuia majaribio 88,761 ya uhamiaji haramu mwaka 2018, idadi ambayo iliongezeka kwa asilimia 37 kutoka mwaka juzi 2017.

Wahamiaji haramu waliozuiwa walikuwa wakijaribu kuvuka bahari kuelekea barani Ulaya.

 

Tags

Maoni