May 13, 2019 10:36 UTC
  • Kuendelea mazungumzo kati ya jeshi la Sudan na wapinzani

Ikiwa ni mwezi mmoja umepita tokea Omar al-Bashir, aondolewe madarakani nchini Sudan, bado kuna tofauti kubwa kati ya Baraza la Kieshi la Mpito na muungano wa Uhuru na Mabadiliko kuhusiana na jinsi raia watakabidhiwa madaraka, kuandaliwa mazingira ya uchaguzi na kubuniwa serikali ya kidemokrasia nchini humo.

Kuhusu jambo hilo, duru mpya ya mazungumzo kuhusiana na namna ya kukabidhiwa madaraka kwa raia ilitazamiwa kufanyika kati ya pande hizo leo Jumatatu. Kufuatia kung'olewa madarakani Rais al-Bashir na jeshi, Baraza la Kijeshi la Mpito ndilo limejipa madaraka ya kuendesha mambo ya nchi hiyo. Limetangaza kwamba litakabidhi madaraka kwa raia baada ya miaka miwili kupitia serikali ya kidemokrasia itakayochaguliwa na wananchi katika uchaguzi huru, jambo ambalo limepingwa na wananchi wanaotaka baraza hilo liwakabidhi madaraka bila kupoteza wakati.

Awali, kuendelea malalamiko na maandamano ya watu wa Sudan kulipelekea baraza hilo la kijeshi kukubali kufanya vikao kadhaa na wapinzani ili kuchunguza njia za kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia. Katika vikao hivyo mapendekezo tofauti yalitolewa na kujadiliwa kuhusiana na njia za kuendesha nchi na hatimaye kukabidhiwa madaraka kwa rais, ambapo uamuzi wa kuundwa baraza jipya litakalojumuisha wanajeshi na raia ulichukuliwa. Hata hivyo kuzuka hitilafu kuhusiana na suala hilo kulipelekea kukwama na kutoendelea mazungumzo hayo. Hivyo maandamano yameendelea kufanyika nchini na hasa katika mji mkuu Khartoum, kwa kadiri kwamba viongozi wa upinzani wametishia kuwataka wafuasi wao wasiitii serikali.

Maandamano ya raia wa Sudan wanaotaka jeshi liwakabidhi madaraka

Waandamanaji wamesema kuwa wataendelea kufanya maandamano madamu Baraza la Kijeshi la Mpito halitaki kukabidhi madaraka kwa wananchi. Hii ni katika hali ambayo baraza hilo limeongeza vitendo vya mabavu na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji. Mohamed Hamdan Daqlu, Naibu Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan amewaambia waandamanaji: 'Baraza la Kijeshi la Mpito limewasilisha mapendekezo mengi kwa ajili ya kulinda usalama katika jamii ya Sudan, hata hivyo subira yetu ina mipaka.'

Namna ya kuunda serikali, muda wa serikali ya mpito na wanachama wa Baraza la Utawala ni miongoni mwa mambo yaliyozua utata mwingi katika duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya wapinzai na Baraza la Kijeshi la Mpito. Katika uwanja huo, Sateh Ahmed al-Hajj, msemaji wa muungano wa Uhuru na Mabadiliko amesema: Kuna tofauti tatu za msingi kati yetu na Baraza la Kijeshi la Mpito ambazo ni muundo wa serikali na je, serikali hiyo iongozwe kwa njia ya rais anayechaguliwa moja kwa moja na wananchi au kupitia bunge. Kuna tofauti nyingine mbili kuhusiana na muda wa serikali ya mpito na viongozi wa Baraza la Utawala.

Wanajeshi wanaotawala Sudan na ambao hawataki kukabidhi madaraka kwa raia

Hivi sasa mazungumzo mapya yamepangwa kufanyika kati ya Baraza la Kijeshi la Mpito na muungano wa Uhuru na Mabadiliko. Hata kama wengi wanatarajia kwamba pande mbili hizo zitaweza kutatua tofauti zao na kubuni serikali ya muda ambayo itaandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru wa kidemokrasia, lakini kuna wengine ambao hawana matumaini yoyote ya kufanikiwa mazungumzo hayo. Kwa mtazamo wao wanajeshi ambao wanatawala hivi sasa Sudan ima ni mabaki ya utawala wa Omar al-Bashir ambaye wangali wanamuunga mkono au wanaungwa mkono na baadhi ya nchi za eneo zikiwemo Imarati na Saudi Arabia, hivyo hawako tayari kukabidhi madaraka ya nchi hiyo kwa raia.

Mazungumzo kati ya Baraza la Kijeshi la Mpito na wapinzani wa Sudan yameanza tena katika hali ambayo inaoonekana kuwa waandamanaji wangali wanashikilia msimamo wao wa kutaka raia wakabidhiwe madaraka na baraza hilo, na kusisitiza juu ya udharura wa kutekelezwa haraka demokrasia nchini.

Tags